IQNA

Hafla za Tasua ya Imam Hussein AS zafanyika kote duniani

10:30 - September 09, 2019
Habari ID: 3472121
TEHRAN (IQNA) – Waislamu kote duniani usiku wa kuamkia leo tarehe 9 Mfunguo Nne Muharram wameshiriki katika vikao, majlisi na shughuli za maombolezo na kukumbuka misiba na masaibu yaliyomkuta mjukuu wa Mtume wetu Muhammad SAW, Imam Hussein bin Ali AS, ndugu na mswahaba zake waaminifu huko Karbala nchini Iraq mwaka 61 Hijria.

Katika shughuli hiyo ya Tasua, mamilioni ya Wairani wapenzi na maashiki wa Imam Hussein na watu wa familia ya Mtume Muhammad SAW waliokuwa wamevaa nguo nyeusi kama ishara ya huzuni na maombolezo wamemkumbuka Abul Fadhl Abbas bin Ali, ndugu yake Imam Hussein ambaye ndiye aliyekuwa mbeba bendera na kamanda wa jeshi la mtukufu huyo katika mapambano ya siku ya Ashura.

Mjini Tehran majlisi za maombolezo na kuwakumbuka mashujaa wa Karbala hususan Abul Fadhl zimefanyika katika maeneo mbalimbali ikiwemo ile iliyofanyika katika Husseiniya ya Imam Khomeini na kuhudhuriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei.

Katika siku ya 9 ya mwezi Muharram mahatibu na wazungumzaji humkumbuka zaidi Abbas, Abul Fadh ambaye alionesha ushujaa, wa hali ya juu katika mapambano ya Karbala na kuwakumbusha watu ushujaa usio na kifani wa baba yake, Ali bin Abi Twalib AS.

Abul Fadhl al Abbas aliuawa shahidi siku ya tarehe kumi Muharram baada ya kukatwa mikono miwili na maadui wa Watu wa Nyumba ya Mtume wetu Muhammad SAW wakiongozwa na Yazid bin Muawiyah.

Tarehe 9 Muharram mwaka 61 Hijria wakati majeshi ya Yazid yalikuwa yamejiandaa kikamilifu kumshambulia Imam Hussein AS na masahaba zake katika ardhi ya Karbala, Imam alimtuma ndugu yake aliyesifika kwa ushujaa mkubwa yaani Abul Fadhl Abbas akawaombe maadui hao wampe fursa aupitishe usiku huo, kwa Swala na kunong'ona na Mola wake. Usiku huo Imam Hussein AS aliwakusanya wafuasi wake na baada ya kumhimidi Mwenyezi Mungu na kumsalia Mtume, aliwaambia: ''Kila anayetaka, aitumie fursa iliyobakia ya giza la usiku kwa ajili ya kuyanusuru maisha yake, kwani hakuna atakayebaki hai hapo kesho tutakapokabiliana na jeshi la Yazid.'' Hata hivyo masahaba na wafuasi waaminifu na waumini wa kweli wa mtukufu huyo walikuwa wameshakata shauri la kujitolea mhanga kwa ajili ya Mwenyezi Mungu hadi tone la mwisho la damu zao. Usiku huo wa kuamkia Ashuraa yaani tarehe 10 Muharram, uwanja wa Karbala ulikuwa medani ya ibada kwa mashujaa ambao licha ya kuwa wachache kwa idadi lakini walisimama imara kama mlima na hawakumuacha Imam na kiongozi wao hata dakika moja.

Watu 72 waliokuwa katika kambi ya Imam Hussein AS huko Karbala wote waliuawa shahidi wakiwa pamoja na kiongozi wao katika mapambano ya haki dhidi ya dhulma na uonevu na hivyo wakaweza kuunusuru Uislamu.

/3840866  

 

captcha