IQNA

Ndege za kivita za Saudia zadondosha mabomu msikitini Yemen, watano wauawa

16:38 - September 23, 2019
Habari ID: 3472144
TEHRAN (IQNA) – Ndege za kivita za Saudi Arabia zimeushambulia kwa mabomu msikiti katika mkoa wa Amran nchini Yemen na kusababisha vifyo vya watu watano wa familia moja.

Kwa mujibu wa taarifa, ndege za kivita za Saudia zimetekeleza hujuma hiyo Jumatatu katika eneo la al-Sawad ambapo watu watano kutoka familia moja waliokuwa wamekimbilia hifadhi katika Msikiti wa Salih Muqfah ili kukwepa mabomu wamepoteza maisha baada ya msikiti huyo kuhujumiwa.

Imedokezwa kuwa watu hao walikuwa katika hema wakati ndege za kivita za Saudia zilipoanza kudondosha mabomu na hivyo wakaamua kukimbilia msikiti kwa dhana kuwa ni sehemu salama zaidi ambayo haiwezi kushambuliwa kwa mabomu lakini ndege za kivita za muungano wa Saudia ziliushambulia pia msikiti huo.

Hivi karibuni ilibainika kuwa, muungano wa kivita unaoonogzwa na Saudi Arabia umebomoa zaidi ya misikiti 1,024 tangu uanzishe vita dhidi ya Yemen mwaka 2015, amesema afisa wa ngazi za juu wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen.

Katika mahojiano na IQNA akiwa katika Maonyesho ya 27 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Tehran mwezi Mei mwaka huu, Bw. Adnan Qafla, afisa wa ngazi za juu wa masuala ya kigeni katika Harakati ya Ansarullah alisema kati ya misikiti ambayo imebomolewa katika hujuma za Saudi na waitifaki wake dhidi ya Yemen ni misikiti iliyojengwa na maswahaba wa Mtume SAW na Maimamu Watoharifu AS.

Inafaa kuashiria kuwa, Saudia ilianzisha mashambulizi dhidi ya Yemen mwishoni mwa mwezi Machi 2015 kwa lengo la kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kumrejesha usukani Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kukimbilia Riyadh.

Hata hivyo Saudi Arabia na washirika wake wameshindwa kufikia malengo yao hayo huku wakisababisha maafa makubwa ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na kuwaua raia wasio na hatia. Zaidi ya watu 16,000 wanaripotiwa kupoteza maisha katika vita vya Saudia dhidi ya Yemen. Idadi kubwa ya watoto na wanawake ni miongoni mwa waliopoteza maisha moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja kutokana na vita dhidi ya Yemen vinavyoongozwa na Saudia kwa himaya ya madola ya Magharibi hasa Marekani na utawala haramu wa Israel.

3844156

captcha