IQNA

Wasio Waislamu wakaribishwa kwa kikombe cha chai Misikitini Ufaransa

10:45 - January 11, 2016
Habari ID: 3470030
Idadi kubwa ya misikiti nchini Ufaransa imefungua milango yake kwa ajili ya raia wa dini zote nchini humo. Mamia ya misikiti nchini Ufaransa imesema kuwa, watu wa dini zote wanaruhusiwa kwenda kwenye misikiti hiyo Jumamosi na Jumapili, ikiwa ni hatua ya kipekee ambayo itatoa mwanya kwa wasio Waislamu kuona upendo wa dini tukufu ya Uislamu na hutuma zake.

Hatua hiyo ya kujenga mapenzi kati ya wananchi wa dini zote nchini Ufaransa imepewa jina la "kikombe cha chai cha udugu."

Waislamu nchini Ufaransa wamesema kuwa, wameanzisha kampeni hiyo ili kutia nguvu hisia za udugu wa kitaifa na kuwaeleza wasio Waislamu, uhakika wa dini tukufu ya Kiislamu.

Kampeni hiyo imefanyika baada ya kutokea mashambulizi matatu ya kigaidi yaliyodaiwa kufanywa na watu wenye majina ya Kiislamu nchini humo.

Mkuu wa Baraza la Waislamu nchini Ufaransa amenukuliwa na shirika la habari la nchi hiyo AFP akisema: Lengo letu ni kuleta anga ya umoja na mshikamano katika taifa la Ufaransa, na Wafaransa wote waishi pamoja kwa salama wakiwemo Waislamu na wasio Waislamu.

Amesema, kampeni hiyo imeendeshwa na misikiti ya Ufaransa ili kuonesha upendo wa kweli uliojikita ndani ya dini tukufu ya Kiislamu ikiwa ni pamoja na kuzima chokochoko za kuuhusisha Uislamu na vitendo viovu na ugaidi.

http://iqna.ir/fa/news/3466088/

captcha