IQNA

Sheikhe Mkuu wa Al Azhar

Uislamu unapinga ugaidi

20:04 - May 21, 2016
Habari ID: 3470327
Sheikhe Mkuu wa Chuo cha al Azhar nchini Misri, Dk Ahmad Muhammad al Tayyib amesema kuwa, kwa mujibu wa aya ya 32 ya Suratul Maida ya Qur'ani Tukufu, dini ya Kiislamu inapiga marufuku kumshambulia mwanadamu yeyote kutoka dini yoyote ile.

Sheikh al Tayyib amelaani pia vitendo vya magenge ya kigaidi vya kujichukulia sheria mikononi mwao na kutenda jinai mbaya kwa jina la Uislamu na kusisitiza kuwa, magenge hayo ya kigaidi hayana uhusiano wowote na dini tukufu ya Kiislamu.

Amesema hayo wakati alipoonana na wakurugenzi wa vyombo zaidi ya 40 vya habari pamoja na wahariri kutoka nchi 23 za Afrika ambao walimtembelea katika Chuo Kikuu cha al Azhar, mjini Cairo, Misri.

Amesema, dini tukufu ya Kiislamu, ni dini ya amani na kupendana, na inapinga vikali jinai za kukata watu vichwa na utegaji mabomu unaofanywa na magenge ya kigaidi kwa lengo la kuharibu sura ya dini ya Kiislamu.

Wakurugenzi wa zaidi ya vyombo 40 vya habari na wahariri kutoka zaidi ya nchi 23 za Afrika, hivi sasa wako Cairo, mji mkuu wa Misri kwa ajili ya mafunzo ya mwezi mmoja kuhusiana na vyombo vya habari barani Afrika.

Chuo Kikuu cha al Azhar ni moja ya vyuo vikuu vikongwe katika ulimwengu wa Kiislamu na vimekuwa vikipokea wanafunzi kutoka kona zote za dunia.

3499996
captcha