IQNA

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu: Kadhia ya Palestina Ndiyo Kadhia Muhimu Zaidi ya Ulimwengu wa Kiislamu

13:34 - September 11, 2010
Habari ID: 1991386
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ijumaa, Mosi Shawwal 1431 H amesema katika khutba za sala ya Idi ‘l-Fitr iliyosaliwa kwenye viwanja vya Chuo Kikuu cha Tehran kuwa suala la Palestina ndilo suala kuu la ulimwengu wa Kiislamu na kwamba mikutano inayodaiwa ni ya amani inafanyika tu kwa lengo la kuficha jinai za utawala wa Kizayuni.
Amesema, Marekani na nchi za Magharibi zimekaa na kuangalia kwa macho tu jinsi taifa la Palestina linavyokandamizwa na halafu zinajifanya kuitisha mikutano eti ya amani. Amehoji akisema ni amani ya aina gani inayodaiwa kutafutwa na nchi hizo? Ni mazungumzo na akina nani yanayoitishwa na nchi hizo?
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, taifa la Palestina ni taifa lililosimama kidete mbele ya mashinikizo ya maadui na kusisitiza kuwa, mashinikizo hayawezi kulifanya taifa hilo imara lilegeze kamba katika misimamo yake.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia pia kuwa taifa la Palestina hivi sasa limeimarika zaidi ikilinganishwa na miaka 20 na 30 iliyopita na kubainisha kwamba, Wapalestina wanao uwezo wa kukata mikono ya mabeberu na kuufuta kabisa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, mabeberu wanataka kuififiliza na kuisahaulisha kadhia ya Palestina lakini maadhimisho makubwa ya Siku ya Kimataifa ya Quds yamethibitisha kuwa hamasa na matumaini ya Waislamu duniani yanaongezeka siku baada ya siku.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, katika Siku ya Kimataifa ya Quds (Ijumaa ya mwisho ya kila mwezi mfukutu wa Ramadhani) tulishuhudia ongezeko kubwa la wimbi la matumaini na hamasa za watu katika pembe mbali mbali duniani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile amelishukuru taifa kubwa la Iran kutokana na harakati adhimu liliyoionyesha katika Siku ya Quds na amesema, taifa la Iran lilionyesha nishati, hamasa, azma, irada na jinsi inavyoujua vizuri wakati uliopo kupitia maandamano makubwa ya siku hiyo.
Amekumbusha kuwa, Wakati Imam Khomeini (quddisa sirruh) alipotangaza Ijumaa ya mwisho ya kila mwezi wa Ramadhani kuwa ni Siku ya Quds miaka 31 iliyopita, maadui walidhani kuwa kadiri siku zinavyokwenda mbele ndivyo siku hiyo itakavyozidi kukosa umashuhuri na hatimaye itasahaulika kabisa lakini Alhamdulillah kadiri siku zinavyosonga mbele ndivyo umashuhuri na hamasa za siku hiyo adhimu zinavyoongezeka na kuwa kubwa zaidi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbusha pia kuwa, mwaka huu Siku ya Kimataifa ya Quds imeadhimishwa katika nchi mbali mbali duniani, barani Asia, Afrika, Ulaya, Marekani na Mashariki ya Kati ambapo taifa la Iran ambalo ndiyo nembo ya harakati hiyo ya Kiislamu liliiadhimisha vizuri mno siku hiyo na limethibitisha kuwa wakati mazingingira ya kimataifa yanaporuhusu, taifa la Iran linajua kutekeleza vizuri mno majukumu yake.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, ukatili wa utawala wa Kizayuni umechupa mipaka na umekuwa wa kiwango cha juu kabisa na kadiri sauti ya kulitetea taifa la Palestina inavyozidi kupaa angani ndivyo utawala huo unavyozidisha kiburi na kujifanya hausikii sauti hizo lakini taifa la Iran mwaka huu limeadhimisha Siku ya Quds kwa hamasa kubwa zaidi na kwamba njama za kiadui za Marekani na nchi za Magharibi zinazidi kuwatia nguvu na mori mkubwa zaidi wananchi wa Iran katika kulinda na kutetea misimamo yao.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amezungumzia janga la mafuriko la nchini Pakistan akisema kuwa janga hili ni msiba mkubwa ambao inabidi ulimwengu wa Kiislamu uchukue hatua za haraka za kuwasaidia ndugu zao wa Pakistan.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaka ulimwengu wa Kiislamu, mataifa duniani na Waislamu wote popote walipo pamoja na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC kuwasaidia ndugu zao wa Pakistan.
Akizungumza katika khutba ya pili ya sala ya Idi ‘l-Fitr iliyosaliwa kwenye viwanja vya Chuo Kikuu cha Tehran Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, suala ambalo linahitajia kuchukuliwa hatua za haraka hivi sasa ni suala la kuwasaidia Waislamu walioathiriwa vibaya na mafuriko nchini Pakistan na kusisitiza kuwa jambo hilo linahitajia hatua za haraka hivi sasa kuliko masuala mengine yote kieneo na kimataifa.
Amesema licha ya kukumbwa na janga hilo kubwa, lakini pamoja na hayo imani za wananchi wa Pakistan hazikutetereka na wamefunga mwezi mzima wa Ramadhani katika mazingira magumu kabisa.
Amesema hivi sasa tumo katika sikukuu ya Idi ‘l-Fitr, ambayo ni siku ya kuonyesha mapenzi, ni siku ya umma wa Kiislamu na kwamba wananchi wanapaswa kutia hima ya kuwasaidi wananchi wa Pakistan. Amesema ni jambo lililo wazi kwamba serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeshapeleka misaada yake huko na tayari baadhi ya wananchi nao wameshatuma misaada yao lakini misaada hiyo haitoshi hivyo misaada zaidi inabidi itumwe kwa Waislamu wa Pakistan.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, maneno yake hayo hayawahusu wananchi wa Iran tu bali yanauhusu ulimwengu mzima wa Kiislamu, mataifa yote duniani, Waislamu wote pamoja na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu OIC.
Ayatullah Udhma Khamenei amefafanua zaidi kuhusu mafuriko ya Pakistan akisema, kidhahiri jina lake yanaitwa ni mafuriko lakini ukweli wa mambo ni kuwa hilo ni balaa adhimu na ni msiba mkubwa uliowakumba wananchi wa Pakistan wananchi waumini ambao ni sehemu isiyotenganishika na uma wa Kiislamu na ni wananchi ambao siku zote wako mstari wa mbele kudhihirisha misimamo yao imara katika mambo na matukio mbali mbali ya kidini yanayojiri duniani.
Amesema, mto wa Sind uliofurika kutoka kaskazini hadi kusini mwa Pakistan na kutoka kwenye mipaka ya Uchina hadi kaskazini mwa Pakistan na kufika hadi kwenye Bahari ya Hindi huko kusini mwa Pakistan imeisababishia hasara kubwa nchi hiyo ya Kiislamu inayokadiriwa kufikia karibu dola bilioni 40 hadi 50.
Ameongeza kuwa, wananchi milioni 20 wa Pakistan wameathiriwa na mafuriko hayo wakiwemo wanawake, watoto wadogo, vizee na watu wasiojiweza.
Amesema madola ya kibeberu duniani na watu wanaopenda kutumia vibaya fursa zinazojitokeza, wana nia ya kutumia vibaya hali iliyo nayo Pakistan hivi sasa kwa ajili ya kufanikishia malengo yao haramu na kwamba baadhi ya madola ya kibeberu yanataka kuigeuza Pakistan kuwa kambi yao ya kijeshi.
Amesema huo ni wasiwasi mwingine uliopo kuhusu maafa hayo ya Pakistan na ana matumaini taifa lililopevuka la Pakistan linaijua vizuri hatari hiyo. Amesema bila ya shaka serikali ya Pakistan inajua vyema majukumu yake na Inshaallah Mwenyezi Mungu atawasaidia kuvuuka vizuri sana kipindi hiki kigumu kinachoikabili nchini hiyo.


16929
captcha