IQNA

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu: Mwamko wa Kiislamu duniani ni bishara njema

14:24 - November 15, 2010
Habari ID: 2032612
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Waliul Amr wa Waislamu duniani Ayatullahil Udhma Sayyed Ali Khamenei ametoa ujumbe kwa mnasaba wa msimu wa Hija mwaka 1431 H na kusema kuzidi kuwa kubwa wimbi la mwamko wa Kiislamu katika dunia ya leo ni uhakika ambao unatoa bishara njema ya mustakbali bora kwa umma wa Kiislamu.
Matini kamili ya ujumbe huu ni kama ifuatavyo:

Bismillahir Rahmanir Rahim

Na hamdu zote ni za Mwenyezi Mungu Bwana wa viumbe pia. Na rehema na amani ziwe juu ya Bwana wetu Muhammad al Mustafa na Ahlul Bayt wake watoharifu na masahaba wateule.
Alkaaba ambayo ni nembo ya umoja na heshima na ni nembo ya tawhidi na umaanawi, ni mwenyeji wa nyoyo zilizojaa mapenzi na matumaini kutoka kila kona ya dunia ambazo zimeitika labeka mwito wa Mola Mlezi katika eneo hilo tukufu ambalo ni chimbuko la Uislamu. Hivi sasa umma wa Kiislamu unaweza kushuhudia taswira jumla ya ukubwa na upana wa umma huo pamoja na imani kubwa na thabiti ya wafuasi wa dini hii tukufu kupitia wajumbe wa umma huo waliokusanyika Makkah kutoka pembe zote nne za dunia na sasa umeweza kuilewa vyema rasilimali yake hiyo adhimu na kubwa sana.
Kujitambua huko kupya kunatusaidia sisi Waislamu kuelewa nafasi yetu tunayostahiki kuwa nayo katika dunia ya leo na kesho Akhera na kujibidiisha vyema kuelekea huko.
Kuzidi kuwa kubwa wimbi la mwamko wa Kiislamu katika dunia ya leo ni uhakika ambao unatoa bishara njema ya mustakbali bora kwa umma wa Kiislamu. Wimbi hilo kubwa la mwamko Kiislamu limeanza katika kipindi hiki cha miaka 30 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuundwa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran, hivi sasa umma wetu mkubwa umekuwa ukipiga hatua za kimaendeleo bila ya kusita, umekuwa ukiondoa vizuizi vyote vinavyojitokeza mbele yake na kufanikiwa kupata ushindi mkubwa. Mbinu za maadui mabeberu zimezidi kuwa tata hivi sasa na wametenga fedha nyingi sana kwa ajili ya kukabiliana na Uislamu. Yote hayo yanatokana na kuwa, maaadui hawapendi kuona umma wa Kiislamu ukipata maendeleo. Adui anafanya propaganda kubwa za kueneza chuki dhidi ya Uislamu, anafanya hila mbalimbali za kuzusha hitilafu na mizozo kati ya makundi ya Kiislamu sambamba na kupalilia taasubu na utesi wa kimadhehebu, kuzusha uadui bandia kati ya Waislamu wa Kishia na Kisuni, kuchochea kitali na ugomvi kati ya tawala za nchi za Waislamu, kujaribu kushadidisha hitilafu na kuzigeuza kuwa uadui usioweza kutatuka, kutumia mashirika ya kijasusi kwa ajili ya kueneza vitendo vya ufisadi na uasherati yote hayo zikiwa ni radiamali za pupa zinazoonesha kuchanganyikiwa maadui mbele ya harakati makini na hatua madhubuti za umma wa Kiislamu za kuelekea kwenye mwamko, heshima na ukombozi.
Leo hii, tofauti na miaka 30 iliyopita, utawala wa Kizayuni silo tena lile zimwi lisiloshindika; tofauti na miongo miwili iliyopita, Marekani na Magharibi sio tena wale wachukuaji wa maamuzi wasio na wapinzani katika Mashariki ya Kati; kinyume na miaka 10 iliyopita, teknolojia ya nyuklia na teknolojia nyinginezo nzito na tata, haziko tena mbali na mikono ya mataifa ya Kiislamu ya eneo hili na wala hazihesabiwi tena kuwa ni kioja. Leo hii taifa la Palestina ni bingwa wa muqawamah, taifa la Lebanon peke yake limeweza kuzima haiba na utukufu bandia wa utawala wa Kizayuni kwa kulishinda vibaya dola hilo la Kizayuni katika vita vya siku 33; na taifa la Iran nalo ni mbeba bendera na muongoza njia ya kuelekea kwenye vilele vya mafanikio.
Leo hii dola la kibeberu la Marekani ambalo linadai kuwa ni kiongozi wa eneo hili la Kiislamu sambamba na kuwa kwake muungaji mkono mkuu wa utawala wa Kizayuni, limekwama kwenye kinamasi lilichojitumbukiza lenyewe huko Afghanistan; na huko nchini Iraq nako dola hilo limetengwa kutokana na jinai zake nyingi lililowafanyia wananchi wa nchi hiyo na katika nchi iliyokumbwa na majanga ya Pakistan, dola hilo la Marekani linachukiwa mno. Kambi iliyo dhidi ya Uislamu ambayo imeyakandamiza kidhulma mataifa na tawala za Kiislamu kwa karne mbili, na kupora utajiri wa mataifa hayo, hivi sasa inashuhudia yenyewe jinsi ushawishi wake unavyozidi kutoweka huku ikikabiliwa na muqawamah wa kishujaa kutoka kwa mataifa ya Kiislamu.
Katika upande wa pili pia, harakati ya mwamko wa Kiislamu inazidi kuimarika na kupata nguvu.
Mambo hayo yenye kuleta matumaini na kutoa bishara njema, inabidi yatufanye sisi mataifa ya Kiislamu kwa upande mmoja: tuwe na matumaini makubwa zaidi kwamba, mustakbali wetu ni bora, na kwa upande mwingine tupate funzo kutokana na mambo hayo na tuzidi kuwa macho kuliko wakati mwingine wowote. Mwito huu unaowahusu watu wote, inabidi uwafanye maulamaa wa kidini, viongozi wa kisiasa, wasomi na vijana, wapate nguvu zaidi za kutekeleza inavyopasa majukumu yao, kama ambavyo mwito huu unawataka pia watu wa namna hiyo waongeze jitihada zao na waweko mstari wa mbele wakati wote katika juhudi za kuuletea maendeleo umma wa Kiislamu.
Kitabu kitakatifu cha Qur’ani kilicho hai wakati wote kinabainisha wazi kwamba:
كُنتُمْ خَیْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللَّهِ
Nyinyi mmekuwa bora ya umma waliotolewa watu, kwa kuwa mnaamrisha mema na mnakataza maovu, na mnamuamini Mwenyezi Mungu. Aal Imran (3:110)
Aya hiyo inautaja umma wa Kiislamu kuwa ni umma wenye heshima na bora kuwahi kutolewa kwa ajili ya wanaadamu. Lengo la kuleta umma huu ni kumwokoa mwanaadamu na ni kwa ajili ya kuwatakia kheri watu.
Jukumu kubwa la umma huo nalo, ni kuamrisha mema na kukataza maovu na kuwa na imani thabiti ya Mwenyezi Mungu. Hakuna jambo bora kabisa kama kuyakomboa mataifa ya wanaadamu kutoka katika makucha ya kishetani ya madola ya kibeberu na hakuna jambo baya na la kuchukiza mno kuliko kuwa kibaraka wa kuwatumikia mabeberu. Leo hii suala la kulisaidia taifa la Palestina na wakazi waliozingirwa wa Ghaza, kuyahurumia na kuyaunga mkono mataifa ya Afghanistan, Pakistan, Iraq na Kashmir, kusimama kidete na kukabiliana vilivyo na dhulma ya Marekani na utawala wa Kizayuni, kulinda umoja na mshikamano wa Waislamu na kupambana na mikono michafu na ndimi za vibaraka na mamluki wanaotaka kuvunja umoja wa Waislamu sambamba na kufanyika juhudi maradufu za kueneza mwamko na hisia za kuwajibika kati ya vijana Waislamu katika maeneo yote ya Kiislamu ni majukumu makubwa ambayo inabidi watu wenye ushawishi na muhimu katika ulimwengu wa Kiislamu wayabebe na kuyasimamia vilivyo.
Mandhari tukufu na ya kipekee ya Hija, inatuonyesha njia nyingi na bora za kuweza kutekeleza majukumu hayo na inatutaka tufanye juhudi kubwa zaidi na hima maradufu kwa ajili ya kufanikisha majukumu hayo.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullah
Sayyid Ali Husaini Khamenei
1 Dhulhijjah 1421
17 Aban 1389

695935
captcha