IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Maadui wanapaswa kuelewa kwamba wananchi ndio walinzi wakuu wa mfumo wa Kiislamu

11:13 - December 30, 2010
Habari ID: 2055890
Ayatullah Khamenei ameitaja hamasa ya tarehe 30 Disemba mwaka jana kuwa ilikuwa ni alama ya mwamko na kuwa macho wananchi na kusema kuwa maadui wa taifa la Iran na wale waliodhani kwamba wanaweza kutenganisha baina ya wananchi na utawala wa Kiislamu hapa nchini wanapaswa kuelewa ujumbe huo wa tarehe 9 Dei na kujua kwamba utawala wa Kiislamu ni mali ya wananchi na wao ndio walinzi wakuu wa mfumo wa Kiislamu wa Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei mapema leo amehutubia maelfu ya wananchi wa matabaka mbalimbali ya mkoa wa Gilan akisema kuwa hima, uwezo wa kumaizi baina ya mambo, maarifa na kuwa macho daima ndio sababu kuu ya maendeleo ya taifa kuelekea kwenye vilele vya juu. Amesema kuwa taifa la Iran kama ambavyo liliweza kumshinda adui katika vita vya kulazimishwa vya miaka minane kwa kutumia ubunifu, kujitolea, ushujaa na kuingia katika medani, vilevile limeonyesha uhodari mkubwa katika vita laini vya miezi minane kutokana na msaada wa Mwenyezi Mungu na tarehe 9 Dei (30 Disemba 2009) liliweza kukunja kabisa jamvi la wafitini kwa baraka za kukumbuka Bwana wa Mashahidi (sa) kwa hima, kuona mbali na kuwa macho.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa kufidia hasara za kubakia nyuma kimaendeleo na taifa la Iran kufika kwenye nafasi linayostahiki ya kielimu na kisayansi kunahitaji hima, azma kubwa na kuwa na matarajio ya mustakbali mwema. Amesisitiza kuwa katika kipindi cha miaka 30 iliyopita taifa la Iran limethibitisha kuwa lina uwezo wa kupiga hatua kubwa za maendeleo.
Akiashiria kuwa nara na kaulimbiu za taifa la Iran ni za kimataifa na lengo lake ni kukata kikamilifu mikono ya mabeberu, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: "Hiyo ndiyo sababu kuu ya chuki na njama za mabeberu dhidi ya taifa hili na fitina za mwaka jana zilikuwa dhihirisho dogo la njama hizo."
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa lengo la fitina za mwaka jana lilikuwa kupotosha wananchi kwa kutoa nara na kaulimbiu za haki lakini zenye muhtawa na madhumuni batili. Amesisitiza kuwa tarehe 9 Dei mwaka jana (30 Disemba 2009) taifa la Iran lilizima njama za wafitini kupitia harakati ya kujitolea na kutoa kipigo kikali kwa kundi hilo.
Ayatullah Khamenei ameitaja hamasa ya tarehe 30 Disemba mwaka jana kuwa ilikuwa ni alama ya mwamko na kuwa macho wananchi na kusema kuwa maadui wa taifa la Iran na wale waliodhani kwamba wanaweza kutenganisha baina ya wananchi na utawala wa Kiislamu hapa nchini wanapaswa kuelewa ujumbe huo wa tarehe 9 Dei na kujua kwamba utawala wa Kiislamu ni mali ya wananchi na wao ndio walinzi wakuu wa mfumo wa Kiislamu wa Iran.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa viongozi wa madola ya kibeberu wakiongozwa na Marekani, wanatumia mbinu tofauti katika kukabiliana na mfumo wa Kiislamu hapa nchini kama njama, matamshi ya urongo, uadui wa waziwazi na nara eti za kuwatetea wananchi, na yote hayo yanaonesha kwamba hadi sasa mabeberu hao bado hawajaweza kuchambua na kulielewa vyema taifa la Iran.
Amesisitiza juu ya udharura wa kulindwa hima ya taifa na akasema katika mwaka huu ambao umepewa jina la mwaka wa Hima na Juhudi Mara Dufu kunaonekana ishara za hima hiyo hapa nchini na maafisa wa serikali wanatekeleza kazi nzuri katika nyanja na sekta mbalimbali. Amesema, hata hivyo hima hiyo inapaswa kudumishwa na kuendelezwa katika miaka ijayo ili taifa la Iran liweze kumvunja moyo adui kwa kufika kwenye kilele cha maendeleo na ukamilifu wa kimaada na kiroho.
Amesema njia pekee ya kuwashinda maadui ni kuwavunja moyo na akaongeza kuwa: "Dhambi kubwa ya baadhi ya wahusika wa fitina za mwaka jana ni kumtia moyo na kumpa matumaini adui."
Amekumbusha uchaguzi adhimu wa Rais wa mwaka jana hapa nchini na mahudhurio makubwa ya wananchi katika zoezi hilo na akasema mahudhuria hayo makubwa ya wananchi yangeiwezesha serikali kupata mafanikio katika nyanja nyingi za kisiasa lakini wafitini walitoa pigo kwa Mapinduzi ya Kiislamu na taifa kwa fitina zao na kumpa matumaini adui.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa fitina za mwaka jana zilikuwa changamoto kubwa na akaongeza kuwa katika changamoto hiyo kubwa wa upande mmoja adui alikuwa akiwaunga mkono wafitini na hata kuwataja kwa majina, na katika upande mwingine taifa la Iran lilihudhuria kwa nguvu zote katika medani.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa kama ambavyo taifa la Iran lilihudhuria katika medani kwa uhodari, ushujaa na kujitolea na kumshinda adui katika vita vya kulazimishwa vya miaka minane, vilevile limeonesha uhodari mkubwa katika vita laini (vita vya kipropaganda na hujuma za vyombo vya habari) kwa kuhudhuria katika medani ya mapambano kwa hima, uoni wa mbali na kuwa macho katika nyanja mbalimbali.
Amesema yaliyotukia ulikuwa mkono wa kudra ya Mwenyezi Mungu ambao ulizivutia nyoyo za wananchi na kuzielekeza katika njia ya haki.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza juu ya kulindwa na kuimarishwa uhusiano na Mwenyezi Mungu sambamba na kuzidisha hima, kuona mbali na umakini na akasema: "Tarehe 9 Dei mwaka jana (30 Disemba 2009) ni moja ya matukio yaliyovutia rehma za Mwenyezi Mungu na wananchi walimiminika katika medani ya mapambano kwa baraka za Bwana wa Mashahidi Imam Hussein (sa) na kulikunja kabisa jamvi la wafitini."
Ayatullah Khamenei amesema kuwa wajibu wa wananchi hususan viongozi na tabaka lililoamka na lililo macho la vijana ni mzito. Amesema daima tunapaswa kutegemea rehma na mwongozo wa Mwenyezi Mungu na kufanya jitihada za kufikia hatima nzuri iliyokadiriwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya taifa la Iran.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria historia ya kushikamana na dini na ya mapambano ya wananchi wa Gilani na akasema hima ya watu wa eneo hilo ni sehemu ya mfano wa kuigwa wa hima ya taifa la Iran. Amesema licha ya juhudi kubwa zilizofanywa na utawala fasidi uliong'olewa madarakani za kujaribu kuharibu itikadi za wananchi wa Gilan lakini wananchi hao walisimama kidete na kwa hima kubwa dhidi ya njama hizo. Ameongeza kuwa mkoa wa Gilani ni miongoni mwa mikoa iliyopiga hatua kubwa katika kushikamana na dini, ikhlasi, jihadi na katika kuhudhuria kwenye medani mbalimbali hapa nchini.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesifu shakhsia ya mwanamapambano na mpigana jihadi mkubwa Shahidi Mirza Kuchak Khan Jangali. Ameelezea pia historia inayong'ara ya wananchi wa mkoa wa Gilan na akasema kuwa kukabiliana na makundi ya kilahidi na yanayokanusha dini, kuhudhuria kwa wingi katika medani za Mapinduzi ya Kiislamu, ushujaa wa vijana waumini na basiji wa mkoa huo katika vita vya kujitetea kutakatifu na mchango mkubwa wa wanafikra, wasomi wa vyuo vikuu na maulama wa Gilani katika vipindi mbalimbali ni sehemu ya historia ya kidini, kimapinduzi na kielimu ya wananchi wa mkoa huo.
Vilevile amekumbusha mchango mkubwa wa wananchi wa Rasht katika kukabiliana na fitina za mwaka jana na kusema mchango huo ni ishara ya hima na kuwa macho wananchi wa Gilan. Amesema Rasht ni miongoni mwa maeneo machache yaliyojitosa katika medani ya kukabiliana na wafitini siku moja mapema zaidi kabla ya harakati ya taifa katika siku ya tarehe 9 Dei mwaka 1388 (30 Disemba 2009).
Mwanzoni mwa hotuba hiyo, mwakilishi wa Faqihi Mtawala katika mkoa wa Gilan na Imam wa Ijumaa wa Rasht Hujjal Islam Walmuslimin Qurbani alieleza historia fupi ya mapenzi ya wananchi wa Gilan kwa Ahlul Baiti wa Mtume Muhammad (saw) na kueneza mafundisho ya watukufu hao. Sheikh Qurbani ameashiria maulama na marjaa wakubwa waliotokea katika eneo hilo na akasema wananchi wenye imani kubwa wa Gilan daima wamekuwa wakibeba bendera ya mapambano dhidi ya ukoloni na udikteta na kwamba Mirza Kuchak Khan ni mfano mkubwa wa wanamapambano hao. Amesisitiza kuwa katika kipindi cha miaka minane ya kujitetea kutakatifu mkoa wa Gilan ulitoa mashahidi elfu nane kwa ajili ya Mapinduzi ya Kiislamu. 720964
captcha