IQNA

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu asema taifa la Iran liko imara

14:15 - January 11, 2011
Habari ID: 2062511
Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kwamba kuwa na muono wa mbali na kuchanganua mambo kwa njia sahihi, vile vile kuwajibika na kujitokeza kwenye medani katika wakati unaofaa ni sababu kuu za za kupata mafanikio na kufaulu kwenye mitihani ya Mwenyezi Mungu na mambo hayo huandaa mazingira ya kupatikana maendeleo ya kimaada na kimaanawi
Amesisitiza kuwa, taifa la Iran limeweza kuvuka na kufaulu vizuri kwenye mitihani mbalmbali ya Mwenyezi Mungu katika kipindi chote cha miaka 32 iliyopita na kwamba taifa hilo hivi sasa liko imara zaidi kuliko wakati mwingine wowote, lina nia na azma kubwa na ya kweli zaidi, liko macho na limeshikamana vilivyo katika njia yake kwa ajili ya kufikia vilele vya ufanisi na ukamilifu na kwa ajili ya kupata maisha bora ya duniani na Akhera.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyasema hayo , Jumapili, Januari 9, 2011, katika mkutano na maelfu ya wananchi wa Qum kwa mnasaba wa maadhimisho ya harakati ya wananchi wa Qum ya tarehe 19, mwezi Dey, 1356 kwa mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsia (sawa na Januari 9, 1978, Miladia).
Ayatullahil Udhma Khamenei ameitaja harakati ya wananchi wa Qum ya Dey 19, 1356 Hijria Shamsia, kuwa ni tukio kubwa lililothibitisha kuweko mstari wa mbele wakati wote wananchi wa Qum, tabasuri na kuona kwao mbali, kuhisi wajibu wa kubebeba majukumu na kuingia kwao kwa wakati kwenye medani.
Ameongeza kuwa, harakati hiyo ilikuwa ni pigo kubwa kwa utawala wa taghuti (wa kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu) na kambi ya kibeberu duniani. Amesema, harakati ya Dey 19 ilitoa mchango mkubwa wa kupatikana ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya tarehe 22 Bahaman 1357 Hijria Shamsia (Februari 11, 1979) kwa uongozi wa hekima wa Imam Khomeini (Quddisa sirruh).
Amekumbusha kuwa, mabeberu na maadui wana hisia kali mbele ya wananchi wa Qum na Hawza (Chuo Kikuu cha kidini) kutokana na tabasuri na muono wa mbali wa wananchi na Hawza, moyo wao wa kuhisi wajibu wa kubeba majukumu na kujitokeza kwao kwenye medani katika wakati unaofaa.
Amesema radiamali zilizoonyesha na maadui wakati wananchi wa Qum walipoonyesha nguvu zao na wakati Hawza, maulamaa na vijana wa Qum walipodhihirisha mapenzi yao makubwa kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu wakati alipotembelea mji huo mtukufu, (mwezi Oktoba 2010) ni jambo linalozidi kuthibitisha udhaifu wa maadui na jinsi walivyoshindwa katika uadui wao dhidi ya taifa la Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na jinsi ulimwengu wa makafiri na maadui ulivyoupokea ushindi huo miaka 32 iliyopita ni mfano mwingine wa udhaifu wa wapinzani na maadui wa mfumo wa Kiislamu na adhama ya harakati ya taifa la Iran.
Ameongeza kuwa, hatua ya kuasisiwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran na kusimama kwake imara mbele ya tawala mbaya zaidi za kibeberu duniani, ilikuwa ni kuonyesha njia mpya iliyosimama juu ya misingi ya Uislamu wa kweli jambo ambalo ni muhali kuweza kukubaliwa na kambi ya dhulma na ubeberu na ndiyo sababu kuu inayowafanya mabeberu na madhalimu duniani waifanyie uadui kiasi chote hiki Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei amekumbushia kazi kubwa na za kujivunia zilizofanywa na taifa la Iran katika medani tofauti na kuongeza kuwa, kwa baraka za mafanikio liliyopata kwenye mitihani mbali mbali ya Mwenyezi Mungu, taifa hili limeweza kujipandisha juu katika upande wa vigezo vya kimaanawi na kimaada na kwamba maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia pamoja na kazi nyingine mbalimbali muhimu zinazofanyika kote nchini Iran ni mfano wa wazi maendeleo hayo ya kimaada.
Ameashiria pia juu ya misaada na rehema za Mwenyezi Mungu katika mafanikio yote hayo na kusisitiza kuwa, taifa la Iran limekuwa likishuhudia misaada ya Mwenyezi Mungu katika medani tofauti linazoingia.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekutaja kushindwa fitna ya mwaka jana (ya baada ya uchaguzi wa Rais wa Iran) kuwa kumetokana na rehema na msaada ya Mwenyezi Mungu na kuongeza kuwa, kwa rehema na uwezo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, wananchi wa Iran waliamka na kujitokeza vilivyo kwenye medani na hivyo kufanikiwa kuishinda njama kubwa iliyokuwa inalikabili taifa lao.
Ayatullah Udhma Khamenei amekumbusha kuwa, hadi hivi sasa pembe za fitna ya mwaka jana hazijajulikana zote na bado kuna uwanja mpana wa kuweza kuchunguza na kubainisha vipengee vya fitna hiyo kwani adui alikuwa amejipanga vizuri na alipangilia njama hiyo kwa kina na kwa mahesabu makubwa.
Amesema, wapangaji wakuu wa fitna ya mwaka jana walitoka nje na kwamba wale watu ambao leo hii wananchi wanawataja kuwa ni viongozi wa fitna hiyo, kwa kweli sio wapangaji wake wakuu bali adui aliwaburuza uwanjani tu watu hao ambapo tab'an watu hao nao inabidi wajitenge na maadui kwani kama hawakufanya hivyo watakuwa wamefanya madhambi makubwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, mtu yeyote hapaswi kukubali kugeuzwa kuwa mwanasesere na kama ataghafilika lakini katikati ya njia akatambua kosa lake, basi anatakiwa atangaze msimamo na njia yake haraka iwezekanavyo na bila ya kuchelewa.
Ayatullah Udhma Khamenei amebainisha pembe mbali mbali za fitna ya mwaka jana iliyolikabili taifa la Iran na kusisitiza kuwa, watu wengine ndio wahusika wakuu wa fitna hiyo ambao walipanga njama zao kwa mahesabu makubwa huku lengo lao hasa lilikuwa ni kuifuta kikamilifu Jamhuri ya Kiislamu na kubadilisha mfumo wa uongozi nchini Iran.
Ameongeza kuwa, mpango mkuu wa maadui ulikuwa ni kusambaratisha Jamhuri ya Kiislamu pamoja na uhakika na kaulimbiu ya kidini katika jamii ya Iran na kubadilisha mfumo wa utawala kwa namna wanayopenda maadui hao.
Ayatullah Udhma Khamenei amekumbusha kuwa, waendeshaji wakuu wa fitna hiyo walipanga mambo meingine kwamba kama watashindwa kufikia wanachotaka, basi waitumbukize Iran katika machafuko na watumie Mapinduzi ya Kiislamu kwa kuyafanya kikatuni kama njia ya kufanikishia malengo yao.
Ameongeza kuwa: "Hata hivyo wananchi wa Iran waliijua vizuri hali ya mambo, wakahisi wajibu wa kubeba majukumu, wakajitokeza kwenye medani katika wakati unaofaa na hivyo kutoa pigo kubwa kwa wapangaji wa njama hiyo na kuifutilia mbali njama yao."
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha ameyataja mafanikio liliyopata taifa la Iran katika mtihani huo mkubwa na tata kuwa yameandaa mazingira ya kuzidi kuimarisha njia ya dini na ya Mapinduzi nchini Iran, huku uwezo na uimara wa Jamhuri ya Kiislamu ukizidi kuongezeka siku baada ya siku.
Amekumbusha kuwa, uimara na nguvu zinazozidi kuongezeka za Jamhuri ya Kiislamu ni bakhshishi ya Mwenyezi Mungu kutokana na mafanikio liliyopata taifa la Iran katika mtihani huo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameyataka matabaka yote ya wananchi kulinda mwamko na uwezo wao wa kuchanganua kwa njia iliyo sahihi masuala makuu mbele ya masuala madogo madogo na kutoyachanganya pamoja na ameongeza kuwa, kutokuwa na tabasuri na kushindwa katika mitihani ya Mwenyezi Mungu hupelekea kutetereka na kusambaratika jamii kama ilivyotokea baada ya wananchi wa zama za Imam Ali AS kushindwa kwenye mtihani wa Mwenyezi Mungu. Amekumbusha kuwa, kufeli wananchi wa zama za Imam Ali AS kwenye mtihani wa Mwenyezi Mungu kulipelekea mtu muovu kabisa kupata fursa ya kumuua shahidi mtukufu huyo kwenye kibla cha ibada na kulipeleka pia kutokea janga kubwa la Karbala la kuuawa shahidi Bwana wa Mashahidi Imam Husain AS na wafuasi wake.
Ameongeza kuwa, nafasi bora waliyo nayo wananchi wa Iran hivi sasa na mafanikio wanayopata katika masuala mbali mbali ya ndani, pamoja na umuhimu wao katika eneo na kwenye masuala ya kimataifa ni matunda ya kufaulu kwao kwenye mitihani mbali mbali ya Mwenyezi Mungu.
Ametanabahisha kuwa, adui anafanya njama nyingi ili kwa kutumia mashinikizo ya kiuchumi, kipropaganda na kueneza uongo mkubwa sambamba na kuzitisha tawala na mataifa mengine yasiwe na uhusiano mzuri na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aweze kuizuia Iran isifanikiwe katika mambo yake, lakini njama zote hizo zimeshindwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia kushindwa siasa za Marekani katika masuala ya Palestina, Lebanon, Afghanistan na Iraq na kuongeza kwamba, Wamarekani, wanadai kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndiyo sababu kuu iliyopelekea kushindwa kwa siasa zao wakati ambapo mwamko na siasa sahihi za mataifa mengine ya dunia ndizo zilizowafanya Wamarekani washindwe kwenye siasa zao hizo za kibeberu.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, nguvu na athari za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika eneo na kati ya mataifa mbali mbali duniani ni athari za kimaanawi kwani mfumo wa Kiislamu umepelekea kuamka mataifa mengine na ni kwa sababu hiyo ndio maana Marekani inafanya juhudi zake zote ili kuhakikisha kuwa serikali ya hivi sasa ya Iraq haiundwi lakini kutokana na mwamko wa wananchi, serikali hiyo itaundwa na Marekani haiwezi kufanya chochote kuzuia kuundwa serikali hiyo.
Ameongeza kuwa, taifa la Iran litaendelea na njia yake ya maendeleo na ufanisi hadi kufikia kwenye vilele vya maisha bora ya duniani na Akhera.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema, wananchi na viongozi wa Iran wametia nia ya kweli ya kuendelea na njia hiyo na kutanabahisha kuwa, kuleta mwamko na kutomdharau adui ndiyo njia ya kuweza kupata maendeleo na kuwa na uwezo unaotakiwa.
Ameongeza kuwa, matabaka yote ya wananchi na hususan vijana, watu wa dini, watu wa Vyuo Vikuu na viongozi nchini, wanapaswa kulinda maradufu sifa yao ya kuwa macho.
Mwishoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kwa kusisitiza kwamba, mwamko wa viongozi, kuwatumikia vilivyo wananchi na kulinda umoja na mshikamano baina yao kutaendelea kuwa mwiba kwenye jicho la adui.
Mwanzoni mwa mkutano huo, Hujjatul Islam Walmuslimin Saidi, Mdhamini wa Haram Tukufu ya Bibi Maasuma (Alayhas Salaam) ya mjini Qum, ameashiria juu ya harakati ya kihistoria ya Dey 19, 1356 Hijria Shamsia na kusisitiza kuwa, wananchi wa Qum wako mstari wa mbele wakati wote na wamethibitisha kivitendo kuwa ni waungaji mkono wa kweli wa Utawala wa Fakihi (Wilayatul Faqih).
Vile vile amemshukuru Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa niaba ya wananchi wa mkoa wa Qum, Hawza na Maulamaa wa mji huo mtukufu, kwa hatua yake ya kutembelea mkoa huo mwezi Oktoba mwaka jana.
727539
captcha