IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Kulinda na kuimarisha anga ya dini ndiyo sababu ya maendeleo halisi ya nchi

21:21 - April 30, 2011
Habari ID: 2114734
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amesema sababu kuu ya maendeleo ya nchi na harakati za kuelekea kwenye izza na utukufu wa kweli ni kulinda na kuimarisha anga ya dini na kushikamana na mafundisho ya dini katika miji na vijiji.
Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo mapema leo akihutubia wanachama wa Baraza Kuu la Mikoa na mameya wa miji. Ametaja Mabaraza ya Kiislamu ya Miji na Vijiji kuwa ni miongoni mwa fahari za utawala wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na taasisi zinazotokana na kura, mitazamo mbalimbali na matakwa ya wananchi. Amesisitiza juu ya udharura wa kuwepo uratibu na ushindani chanya kwa ajili ya kuhudumia wananchi na akasema hatua yoyote inayowafurahisha maadui na kuwakasirisha marafiki haikubaliki na kuna udharura wa kujiepusha nayo. Ameongeza kuwa iwapo kutakuwepo ushirikiano, uwiano na upendo hapana shaka kwamba rehema na baraka za Mwenyezi Mungu pia zitaongeza zaidi.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa taasisi ya mabaraza ni miongoni mwa masuala muhimu na nyeti mno na yenye maana pana. Amesisitiza kuwa kifungu kinachohusu Mabaraza ya Miji na Vijiji katika Katiba ya Iran ni alama ya jinsi Jamhuri ya Kiislamu inavyozingatia na kutoa kipaumbele kwa fikra mbalimbali, mashauriano na mitazamo tofauti katika uendeshaji wa masuala ya nchi. Ameongeza kuwa maudhui hiyo inakabiliana na mifumo na tawala za kidikteta.
Ayatullah Khamenei amekumbusha kwamba miongoni mwa fahari za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kwamba ilizingatia na kutilia maanani mitazamo, fikra na matakwa ya wananchi tangu hapo mwanzoni.
Akizungumzia mitazamo tofauti iliyopo kuhusu kazi na majukumu ya Mabaraza ya Kiislamu, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema mizani na kipimo kikuu kuhusu kazi na majukumu ya mabaraza hayo ni Katiba na marejeo pekee ya tafsiri ya Katiba ni Baraza la Walinzi wa Katiba.
Amesisitiza kuwa mtazamo wa Baraza la Walinzi wa Katiba ndiyo huja daima na kuongeza kuwa mtazamo wa baraza hilo pia ndio unaopaswa kuzingatiwa katika mjadala unaohusu suala kwamba je, kazi za Mabaraza ya Kiislamu ni kusimamia shughuli za serikali tu au ni usimamizi na utekelezaji?
Ayatullah Ali Khamenei amesisitiza juu ya mchango mkubwa wa Mabaraza ya Kiislamu hapa nchini na udharura wa kulindwa na kuimarishwa mabaraza hayo na akasema kuwa moja ya mambo muhimu kuhusu mabaraza hayo ni uwezo wake wa kutoa majibu kwa matatizo yote ya kieneo na kikaumu hapa nchini.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa moja ya kazi muhimu za Mabaraza ya Kiislamu na halmashauri za miji ni kutilia maanani masuala ya kiutamaduni katika miji na vijiji. Amesema huduma mbalimbali zinazofanyika katika miji na vijiji zikiwemo za ujenzi wa nyumba, barabara, majina ya mitaa na kadhalika zinapaswa kwenda sambamba na teknolojia ya kisasa, na kuzingatia usanifu majengo wa Kiislamu, itikadi za kidini na kijamii na mazingira ya kila eneo.
Ayatullah Khamenei amesema moja ya sifa kuu za utawala wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuwa uhuru na kujitawala kwake. Amesisitiza kuwa: "Kwa baraka za Uislamu tumeweza kulinda utambulisho wetu wa Kiirani na uhakika huo unapaswa kuonekana katika huduma zote na masuala ya miji."
Amesema sababu kuu ya maendeleo ya nchi na harakati za kuelekea kwenye izza na utukufu wa kweli ni kulinda na kuimarisha anga ya dini na kushikamana na mafundisho ya dini katika miji na vijiji.
Ayatullah Khamenei ametilia mkazo udharura wa kuwepo ushirikiano na uratibu kati ya mabaraza na vyombo vyote vya dola na akasema, kutokuwepo ushirikiano na ushindani hasi vitakuwa na madhara kwa taifa.
Akikumbusha moja ya vigezo vya hayati Imam Khomeini aliyesema kuwa hatua au kazi yoyote inayomfurahisha adui haikubaliki, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuna ulazima wa kujiepusha na kila kazi au hatua inayomfurahisha adui na kuwachukiza marafiki.
Mwanzoni mwa mkutano huo Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Mikoa Bwana Chamran alitoa hotuba fupi akisema kuwa kuwepo wajumbe laki moja na elfu kumi kutoka nchini kote katika Mabaraza ya Kiislamu ya Miji na Vijiji na wajumbe 75 wa mabaraza hayo kutoka mikoa 31 katika Baraza Kuu la Mikoa ni dhihirisho maridadi la demokrasia ya kidini. Amesema moja ya matatizo ya sasa ya mabaraza hayo ni nafasi na wajukumu yake ambayo yamebanywa katika suala la kusimamia tu shughuli za serikali.
Meya wa jiji la Tehran Qalibaf pia alitoa hotuba kwa niaba ya mameya wa miji mingine akizungumzia masuala yanayopewa kipaumbele katika shughuli na kazi za halmashauri za miji. 783786
captcha