IQNA

Kiongozi Muadhamu katika Baraza la Idul Fitri:

Umma wa Kiislamu unapasa kurejesha adhama na utukufu wake

11:03 - September 01, 2011
Habari ID: 2179852
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei mapema leo amehutubia hadhara ya viongozi wa serikali na matabaka mbalimbali ya wananchi katika Husainiya ya Imam Khomeini mjini Tehran akiutaja mwamko wa sasa wa Kiislamu kuwa ni harakati ya Waislamu kurejea kwenye utambulisho wao wa asili.
Amesisitiza kuwa adhama na utukufu wa umma wa Kiislamu umo katika kurejea kwenye nguvu ya Uislamu, kumtegemea Mwenyezi SW na kutambua uwezo wake mkubwa.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa mwamko wa Kiislamu katika eneo la Mashariki ya Kati ya kaskazini mwa Afrika na kuwepo wananchi katika medani mbalimbali kwa ajili ya kushika hatamu za kujiamulia mambo yao wenyewe ni uzoefu muhimu sana na wenye thamani kubwa katika historia ya Uislamu. Ameongeza kuwa matukio yanayojiri kwa sasa katika nchi za Misri, Tunisia, Yemen, Libya, Bahrain na katika nchi nyingine yana umuhimu mkubwa kwa mataifa ya Waislamu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa iwapo irada na azma ya mataifa ya Waislamu itawashinda wale wanaofanya njama za kuingilia masuala ya nchi za Kiislamu, basi nchi za Kiislamu zitapiga hatua mbele kwa kipindi kirefu. Hata hivyo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamum ametahadharisha kuwa iwapo dunia ya kibeberu na viongozi wa Uzayuni wa kimataifa ukiwemo utawala dhalimu na wa kibeberu wa Marekani utaweza kudandia mawimbi hayo na kushika hatamu za harakati ya mwamko wa mataifa ya Kiislamu, hapana shaka kuwa ulimwengu wa Kiislamu utakabiliwa na matatizo makubwa kwa kipindi cha miongo mingi.
Amelitaja jukumu la umma wa Kiislamu hususan shakhsia wa kisiasa na kiutamaduni katika dunia ya Kiislamu kwa ajili ya kuzuia kutokea hali kama hiyo ya kusikitisha kuwa ni muhimu na nyeti mno. Ameongeza kuwa leo ni siku ya mtihani mkubwa kwa nchi na mataifa ya Kiislamu, kwani mataifa ya Waislamu yametambua vyema uwezo wa nguvu zake kubwa.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja utendaji wa taifa kubwa la Iran katika kipindi cha miaka 30 iliyopita kuwa ni mfano wa wazi wa kusimama kidete na kutumia vyema uwezo wote katika njia iliyonyooka. Ameongeza kuwa, matunda ya kusimama kidete huko katika kipindi cha miaka 30 iliyopita yanaonekana wazi na kipindi cha sasa ni moja ya vipindi vinavyong’ara zaidi katika historia ya taifa la Iran.
Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa, katika kipindi cha miaka 30 iliyopita vizazi mbalimbali vimesimama imara mbele ya mashinikizo ya ubeberu ikiwa ni pamoja na vikwazo, vitisho vya kijeshi, kisiasa na kiusalama na hii leo taifa la Iran ni taifa lenye heshima, nguvu, linalopiga hatua mbele, lenye matumaini ya mustakbali mzuri na lenye dira na mwelekeo uliowazi.
Mwanzoni mwa mkutano huo Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa mkono wa Idul Fitri kwa Waislamu wote na kusema kuwa, mazoezi ya ikhlasi na kuwa mja halisi wa Mwenyezi Mungu, upendo na kusamehe na kuwa na matumaini ya mustakbali mwema ni masomo na darsa tatu kubwa zilizopatikana katika mwezi mtukufu wa Ramadhani. Ameongeza kuwa, Idul Fitri ni sikukuu ya utawala wa thamani za mafundisho ya Mwenyezi Mungu, ni idi ya Wilayat, upendo na matumaini.
Rais Ahmadinejad ameashiria dhulma na jinai zinazofanywa na mabeberu dhidi ya wanadamu hususan uhalifu unaoendelea kufanywa na serikali ya Marekani na Wazayuni waovu katika ardhi ya Palestina, na akasisitiza kuwa ni wajibu kwa watu wote wanaompwekesha Mwenyezi Mungu na waumini kishikamana barabara na suala la kuikomboa Palestina kutoka kwenye makucha ya Wazayuni makatili ili kwa rehma zake Mola, ukombozi wa Quds Tukufu uwe utangulizi wa serikali ya watu wema na kutekelezwa uadilifu kote duniani. 852895


captcha