IQNA

Ayatullah Khamenei:

Matukio ya sasa ya ulimwengu wa Kiislamu ni bishara ya mustakbali mwema

10:59 - September 16, 2011
Habari ID: 2187920
Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa, mabadiliko yanayotokea katika dunia ya Kiislamu yanatoa bishara ya mustakbali mwema, na dalili za mustakbali huo mwema na mabadiliko makubwa zimeanza kudhihiri.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei aliyasema hayo Jumanne iliyopita alipokutana na maulamaa, wanafikra na wasomi wanaoshiriki katika mkutano wa tano wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Ahlul Bait AS na pia wambata wa utamaduni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika nchi mbalimbali. Ayatullah Khamenei ameashiria uwezo mkubwa wa wafuasi wa Ahlul Bait AS na vitisho vinavyoukabili ulimwengu wa madhehebu ya Shia na umma wa Kiislamu na akasema kuwa harakati adhimu za Kiislamu za hivi sasa katika ulimwengu wa Kiislamu ni utangulinzi wa mabadiliko makubwa zaidi na utawala wa Uislamu; na wafuasi wa Ahlul Bait AS wanaunga mkono harakati hizo za Kiislamu.
Katika mkutano huo uliofanyika ndani ya Haram ya Imam Ridha AS mjini Mash’had huko kaskazini mashariki mwa Iran, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza uwezo na sifa za kipekee za mfumo wa Ahlul Bait AS na kusema kuwa taifa na nchi ya kwanza kabisa iliyoweza kuanzisha mfumo wa utawala kwa mujibu wa Uislamu na Qur’ani ni taifa na nchi inayofuata Ahlul Bait wa Mtume Muhammad SAW.
Ayatullah Khamenei amesema: “Leo hii vijana wa nchi za Kiislamu wanaelekea kwenye mafunzo ya Uislamu kwa ajili ya kufikia matumaini na matarajio yao badala ya kuelekea kwenye mifumo ya kimaada, na fahari hii imepatikana kwa baraka za harakati ya taifa la Iran.”
Amezitaja harakati za hivi karibuni katika nchi za Misri, Tunisia, Libya, Bahrain na Yemen kuwa ni miongoni mwa rehma za Mwenyezi Mungu na kuongeza kuwa: “Msimamo wetu sisi ni kuunga mkono harakati hizo na kuziimarisha zaidi na ni matarajio kwamba, harakati hizo za Kiislamu zitapelekea kukatwa kikamilifu udhibiti wa maadui wakuu, yaani Wazayuni na Marekani.”
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa sambamba na uwezo na sifa hizo za kipekee kuna udharura wa kuwa macho mbele ya vitisho na madhara ya aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na njama za kuzusha hitilafu kati ya madhehebu mbalimbali ya Kiislamu hususan baina ya Shia na Suni.
Ayatullah Khamenei amesema, njama za kuzusha hitilafu baina ya Shia na Suni zinafanyika kwa malengo ya kisiasa ya kimataifa. Amesema, sambamba na kutekelekeza siasa za kuwatisha watu kuhusu Uislamu, ulimwengu wa kibeberu unatekeleza pia sera makhsusi za kuwatisha watu kuhusu Ushia na tunapaswa kuwa waangalifu kikamilifu mbele ya njama hizo.
Amesisitiza juu ya itikadi kubwa ya wafuasi wa Ahlul Bait kuhusu umoja katika umma wa Kiislamu na akaongeza kuwa, saada na ufanisi wa umma wa Kiislamu hususan ufanisi wa Mashia, umo katika umoja wa umma wa Kiislamu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia ameashiria suala la kufeli mifumo ya kimaada katika kukidhi mahitaji ya mwanadamu na kutoa majibu mapya na akasisitiza kuwa maarifa ya kidini hususan elimu na maarifa ya Ahlul Bait AS, yanapaswa kuenezwa kati ya Waislamu na jamii zisizokuwa za Kiislamu kwa mujibu wa mahitaji ya kila zama.
Mwishoni mwa hotuba yake Ayatullah Khamenei amesema kuwa, mabadiliko yanayotokea katika dunia ya Kiislamu yanatoa bishara ya mustakbali mwema, na dalili za mustakbali huo mwema na mabadiliko makubwa zimeanza kudhihiri.
Mwanzoni mwa mkutano huo Naibu Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon Sheikh Naim Qasim, Sheikh Hassan Sultan kutoka Bahrain, Hujjatul Islam Walmuslimin Akbari kutoka Afghanistan, Sayyid Ammar al Hakim ambaye ni Mwenyekiti wa Majlisi Kuu ya Kiislamu ya Iraq, Hujjatul Islam Walmuslimin Sheikh al Amri kutoka Saudi Arabia na Bibi Hajar Hussaini kutoka Marekani walitoa hotuba wakieleza mitazamo yao kuhusu matukio ya sasa katika eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika, mwamko wa Kiislamu na kasi kubwa ya watu kuelekea kwenye dini ya Uislamu ulimwenguni. Shakhsia hao wamesisitiza juu ya udharura wa kuwa macho katika kukabiliana na vitisho vya maadui wa umma wa Kiislamu na ulazima wa kuwepo umoja na mashikamano zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu.
Vilevile Hujjatul Islam Walmuslimin Muhammad Akhtari Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul Bait AS ametoa ripoti kuhusu mkutano wa tano wa Baraza Kuu la jumuiya hiyo uliohudhuriwa na zaidi ya wasomi, wanafikra na maulamaa 500 kutoka nchi 110 duniani. 859954


captcha