IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Kuna udharura wa kuchunguzwa hatari zinazoyakabili mapinduzi ya wananchi na mwamko wa Kiislamu

0:11 - September 18, 2011
Habari ID: 2188801
Mamia ya wanazuoni, wasomi, wanafikra, wataalamu wa masuala ya kijamii na wanahistoria kutoka nchi mbalimbali duniani hususan ulimwengu wa Kiislamu leo wameanza mkutano wa kuchunguza taathira za mwamko wa Kiislamu katika mkutano wa kwanza wa kimataifa wa Mwamko wa Kiislamu uliofunguliwa kwa hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa mwamko wa Kiislamu na utambuzi wa umma wa Kiislamu vimevunja mzingiro wa kidikteta na kibeberu. Amechunguza kwa kina utambulisho wa harakati na mapinduzi yanayoendelea Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika na kuweka wazi matatizo na hatari zinazokabili harakati hizo kubwa. Vilevile amebainisha njia za kuweza kushinda matatizo na hatari hizo. Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, mwamko wenye baraka wa Kiislamu umezitokomeza kete hatari sana za kambi ya adui kwa kuwashtukiza mashetani wa kieneo na kimataifa; hata hivyo tunapaswa kuongoza vyema harakati inayoendelea hivi sasa na kuifikisha kwenye malengo yake kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu, kujifunza kutokana na uzoefu wa historia ya sasa ya ulimwengu wa Kiislamu na kwa kutumia busara, azma na ushujaa.
Akiashiria kwamba matukio makubwa ya kijamii hutegemea masuala ya kihistora na kiustaarabu, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kuwepo shakhsia wa kifikra na kijihadi katika medani ya matukio ya miaka 150 iliyopita kwenye nchi za Kiislamu na kufeli tajiriba ya serikali tegemezi kwa mifumo ya Mashariki na Magharibi ni miongoni mwa sababu zilizochangia katika kujitokeza hali ya sasa. Ameongeza kuwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na taathira za mfumo uliobakia hai, madhubuti, shujaa na unaopiga hatua za maendeleo wa Jamhuri ya Kiislamu ni ukurasa muhimu katika upembuzi na uandishi wa historia ya masuala ya zama hizi ya ulimwengu wa Kiislamu.
Amebainisha utambulisho wa harakati na mapinduzi yanayoendelea katika maeneo ya Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika na kusema kuwa mahudhurio ya kweli ya wananchi katika medani ya kazi, mapambano na jihadi ndio sababu muhimu zaidi ya mageuzi yanayoshuhudiwa kwa sasa. Ameashiria tofauti kubwa iliyopo baina ya mageuzi yanayofanywa na wananchi na harakati nyingine za kijamii na akasema kuwa, mageuzi yanayofanywa na wananchi huwa kama neno jema la Mwenyezi Mungu, na mahudhurio muhimu ya wananchi katika mageuzi hayo huchora ramani ya mustakbali mwema na kuwanyima viongozi waliopotea na vibaraka wa adui fursa ya kupotosha na kulegeza kamba mbele ya maadui.
Ayatullah Khamenei amezungumzia suala la kujitokeza taratibu siri takatifu "yaani irada na azma ya mapinduzi" katika fikra za wananchi wa Misri na kudhihiri siri hiyo katika mahudhurio makubwa ya wananchi shujaa, wenye maarifa na fahari wa Misri katika Medani ya Tahrir na medani nyingine. Amesema hukumu hiyo ya Mwenyezi Mungu inajiri pia kuhusu wananchi wa Tunisia, Yemen, Libya na Bahrain.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kaulimbiu, na mienendo ya wananchi wa Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika inaakisi misingi, thamani na malengo ya mapinduzi yanayoendelea sasa katika maeneo hayo. Amesisitiza kuwa: "Miongoni mwa nguzo na misingi ya daraja la kwanza ya mapinduzi ya sasa ni kuhuisha utukufu na heshima ya kitaifa iliyokanyagwa na madikteta waovu na tegemezi kwa Marekani na Magharibi."
Ameashiria pia nara na kaulimbiu zinazotolewa na mataifa ya Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika na kusema kuwa, kupeperusha bendera ya Uislamu ambayo ni dhihirisho la itikadi kubwa na za kale za wananchi pia ni miongoni mwa nguzo na misingi ya mapinduzi ya sasa. Ameongeza kuwa, wananchi wa maeneo hayo wanaamini kwamba, kuwa na usalama wa kifikra, uadilifu, maendeleo na ustawi haviwezi kupatikana isipokuwa chini ya kivuli cha sheria za Kiislamu.
Amekutaja kusimama kidete mbele ya ushawishi na udhibiti wenye hasara kubwa na wa kudhalilisha wa Marekani na Ulaya na kupambana na utawala ghasibu na dola bandia la Kizayuni kuwa ni nguzo na msingi mwingine wa mapinduzi ya Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika. Ayatullah Khamenei amewaambia wageni wanaoshiriki katika mkutano wa kwanza wa kimataifa wa Mwamko wa Kiislamu kuwa nchi za Magharibi na Uzayuni zinafanya kila liwezekanalo kwa ajili ya kukanusha misingi na malengo hayo, hata hivyo uhakika hauwezi kubadilishwa kwa kukanushwa na kuukadhibisha.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amekemea vikali hatua ya madola ya kigeni ya kutaka kupewa hisa katika mapinduzi ya maeneo haya na kuongeza kuwa, mabeberu waliotumia uwezo wao wote kwa jili ya kuwalinda watawala madikteta, waovu na tegemezi hawana haki ya kujitambulisha kama sehemu iliyochangia katika mapinduzi ya sasa.
Akiendeleza maudhui hiyo, Ayatullah Khamenei amesema, uingiliaji wa majeshi ya NATO na Marekani huko Libya umepelekea kuharibiwa miundombinu ya nchi hiyo na kusababisha hasara ambayo haiwezi kufidika. Amesema kuwa iwapo uingiliaji huo usingekuwepo, yamkini kwamba wananchi wa Libya wangepata ushindi kwa kuchelewa, lakini wakati huo wasingeuawa watu wengi wasiokuwa na hatia kiasi hiki, na washirika wa zamani wa Gaddafi na maadui wa siku nyingi wa wananchi wa Libya wasingeweza kudai haki ya kuwa na hisa katika mapinduzi ya nchi hiyo iliyodhulumiwa na kuharibiwa na vita.
Akitoa tathmini ya sehemu hii ya hotuba yake kuhusu utambulisho wa mapinduzi yanayoendelewa katika maeneo ya Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika, Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa wananchi na shakhsia wanaotokana na wananchi ndio wamiliki halisi wa mapinduzi haya na watayalinda na kuweka ramani ya njia ya mustakbali inaoelekea katika ukamilifu wa harakati hii ya kihistoria.
Sehemu ya pili ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mkutano wa kwanza wa kimataifa wa Mwamko wa Kiislamu imechunguza matatizo na hatari zinazokabili mageuzi yanayofanywa na wananchi.
Ameashiria uzoefu wenye mafanikio wa taifa la Iran katika kukabiliana na hatari kama hizo na akasema, hatari zinazoukabili mwamko wa Kiislamu zinaweza kugawanywa katika sehemu mbili: Hatari zinazotokana na udhaifu wa ndani, na hatari zinazotokana na mipango na njama za moja kwa moja za maadui.
Ayatullah Khamenei amesema, kuridhika na hali ya mambo na kuwa na hisia za ushindi ambazo hufuatiwa na hali ya kupoteza hamasa na kudhoofika kwa azma ndio hatari ya kwanza ya ndani inayoukabili mwamko wa Kiislamu. Ameongeza kuwa hatari hiyo huwa kubwa zaidi wakati baadhi ya watu wanapoanza kudai ngawira za ushindi na kutaka kupewa hisa makhsusi.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kwamba, kuwa na woga mbele ya nguvu ya kidhahiri ya mabeberu, kumwamini adui na kutumbukia katika mitego ya tabasamu na ahadi zake, kutotambua mbinu tata za tawala za mabeberu na kughafilika nao, kupatwa na kiburi na ghururi, hitilafu kati ya wanamapinduzi na kujitokeza pengo katika kambi ya mapambano ni miongoni mwa hatari za ndani zinazoyakabili mapinduzi ya wananchi. Amesisitiza juu ya udharura wa kujiweka mbali na hatari hizo kwa kutumia uwezo wote na kutumia neema zote za Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kudumisha mwamko wa Kiislamu kwa kuchanganya pamoja ushujaa, tadbiri, irada na azma kubwa.
Akibainisha sehemu ya pili ya hatari zinazoyakabili mapinduzi ya mataifa ya Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika, Ayatullah Ali Khamenei ameashiria mipango ya maadui kwa ajili ya kuwasimika vibaraka na viongozi tegemezi kwa Marekani na nchi za Magharibi na akasema kuwa, iwapo njama hiyo itang'amuliwa kutokana na kuwa macho wananchi, mabeberu watafanya juhudi za kubuni mbinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa pendekezo la mifumo mbalimbali ya serikali, katiba zinazoifanya nchi kuwa tegemezi na njia nyingine potofu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kupenya na kuwa na ushawishi miongoni mwa wanamapinduzi, kuuimarisha kifedha na katika vyombo vya habari mrengo makhsusi usioaminika na kuutenga mrengo halisi wa mapinduzi ya wananchi, ni mbinu nyingine zinazotumiwa na maadui kwa ajili ya kudhibiti tena hali ya mambo.
Amewahutubu maulamaa, wasomi na wanafikra wa ulimwengu wa Kiislamu akisema kuwa: "Iwapo mbinu hizo zitafeli, mabeberu huanza kutumia mbinu za kuzusha machafuko, kufanya mauaji ya kigaidi, kuzusha mapigano kati ya wafuasi wa dini na kaumu mbalimbali na hata kuanzisha vita kati ya nchi zinazopakana; na hufanya njama za kuwavunja matumaini wananchi na kuwachosha na hatimaye kufelisha mapinduzi yao kwa kutumia mbinu za kuwawekea vikwazo vya kiuchumi, kufanya hujuma za kila upande za kipropaganda na za vyombo vya habari, kuwachafulia jina skakhsia na watu wema na kuwanunua watu dhaifu."
Baada ya kubainisha hatari zinazoyakabili mapinduzi ya wananchi katika Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amewapa nasaha wasomi, wanafikra, maulamaa na wataalamu wa masuala ya kisiasa, kidini, kijamii na kiutamaduni za jinsi ya kushinda hatari hizo kwa kutegemea uzoefu wa taifa la Iran na uchunguzi wa kina kuhusu hali ya nchi nyingine.
Kutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu, kuwa na matumaini ya nusra yake, kutumia busara, kuwa na azma, ushujaa, kuwepo kwenye medani ya mapambano siku zote, kutoacha jihadi na kujitolea katika njia ya Mwenyezi Mungu, kujiepusha na ghururi na mghafala na kumshukuru Mwenyezi Mungu ndiyo mambo yaliyosisitizwa zaidi katika sehemu hii ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Ametilia mkazo suala na kuandika na kutangaza waziwazi misingi na nguzo za mapinduzi, kuzipitia mara kwa mara, kufanyia marekebisho misingi na nara na kuzioanisha na misingi na sheria za Uislamu. Amesema kuwa malengo ya mapinduzi kama kujitawala, uhuru, kupigania uadilifu na kutosalimu amri mbele ya siasa za kiimla na kikoloni, kupinga ubaguzi wa kikaumu na kikabila na kupinga waziwazi Uzayuni ambavyo ni nguzo za harakati za sasa za nchi za Kiislamu, vyote vimetolewa katika Uislamu na Qur'ani.
Ayatullah Khamenei amewataka maulamaa na wanafikra wa ulimwengu wa Kiislamu kushikamana barabara na kikamilifu na misingi na akasema: "Kamwe musiiamini Marekani na NATO na tabasamu na ahadi zinazovutia kidhahiri za tawala zinazotenda uhalifu na jinai kama Uingereza, Ufaransa na Italia; zikataeni njia za ufumbuzi za wageni na badala yake tafuteni njia za utatuzi kutoka kwenye chemchemi inayotiririka ya Uislamu."
Suala jingine lililousiwa na Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa wasomi na wanafikra wanaoshiriki katika mkutano wa kwanza wa Mwamko wa Kiislamu mjini Tehran ni kujiepusha na hitilafu za kimadhehebu, kikaumu, kikabila na hitilafu za mipaka.
Amesema: "Tambueni hitilafu zenu lakini ziongozeni vyema na muelewe kwamba, maelewano kati ya madhehebu ya Kiislamu ndio ufunguo wa uokovu." Amesisitiza kuwa watu wanaochochea moto wa mifarakano na hitilafu za kimadhehebu ni vibaraka wa shetani kwa kutambua au bila ya kutambua.
Ayatullah Khamenei amesisitiza juu ya kusimama kidete dhidi ya mifumo ya kutwishwa kama mifumo ya kilaiki, uliberali wa Magharibi, utaifa (nationalism) uliofurutu mipaka na mirengo ya kushoto ya Kimaxi kwa ajili ya kudumisha mwamko wa Kiislamu. Amewausia pia wanafikra hao wa ulimwengu wa Kiislamu kufanya kazi ngumu ya kubuni mfumo wa utawala na kuongeza kuwa kuna ulazima wa kuainisha lengo la mwisho kuwa ni kujenga umma mmoja wa Kiislamu, kutengeneza ustaarabu mpya wa Kiislamu na kusimamisha dini, mantiki, elimu na maadili mema.
Amekutaja kuikomboa Palestina kutoka kwenye makucha ya Wazayuni kuwa ni miongoni mwa malengo makuu na kusema kuwa, kizazi cha vijana wa nchi za Kiislamu kinaweza kufanya kazi hizo kubwa na kuna udharura wa kuhuishwa moyo wa kujiamini kati ya kizazi hicho cha vijana.
Hotuba muhimu ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika hadhara ya mamia ya maulamaa, wasomi, wanafikra na wataalamu wa masuala ya jamii na wanahistoria kutoka nchi mbalimbali hususan ulimwengu wa Kiislamu imemalizika kwa kuusia mambo mawili muhimu:
1- Udharura wa kushiriki wananchi katika kuendesha masuala ya nchi kwa kutekeleza mfumo wa demokrasia ya Kiislamu.
2- Udharura wa kutenganisha na kuweka mipaka kati ya misimamo ya Kiislamu na misimamo mikali.
Kuhusu suala la kwanza, Ayatullah Khamenei amesema, mataifa yaliyofanya mapinduzi yanataka fikra na mitazamo yao ishirikishwe katika uendeshwaji wa masuala ya nchi, na kwa kuwa wananchi hao ni Waislamu, hapana shaka kwamba wanataka mfumo wa demokrasia ya Kiislamu, yaani mfumo wa utawala ambao viongozi wake wanachaguliwa na wananchi na sheria zinazotawala jamii zijengeke kwa mujibu wa maarifa na sheria za Kiislamu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa mfumo wa demokrasia ya Kiislamu unaweza kuwa na sura na miundo mbalimbali kulinga na mazingira ya nchi tofauti; hata hivyo tunapaswa kuwa macho kikamilifu ili mfumo huo wa demokrasia usifananishwe kimakosa na demokrasia ya kilaiki na uliberali wa Magharibi ambao mara nyingine huwa dhidi ya dini.
Ayatullah Khamenei ameashiria pia udharura wa kutenganishwa na kutofautishwa kikamilifu kati ya misimamo ya Kiislamu na taasubi za kijahili. Ameongeza kuwa, misimamo mikali ya kidini ambayo mara nyingi huambatana na utumiaji mabavu na ukatili, ni sababu ya kubakia nyuma na kuwa mbali na malengo aali ya mapinduzi na mwamko wa Kiislamu, suala ambalo pia huwafanya wananchi wajitenge na hatima yake ni kushindwa mapinduzi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amemalizia kwa kusema kuwa, mwamko wa Kiislamu ni uhakika ulioenea katika anga nzima ya eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika. Amesisitiza juu ya udharura wa kuongozwa matukio na mageuzi yanayojiri katika maeneo hayo na kuongeza kuwa, takwa (uchamungu) kwa maana yake halisi na ya kina, kuasi na kukataa amri za makafiri na wanafiki, kutawakali na kumtegemea Mwenyezi Mungu ndiyo mwongozo wenye taathira kubwa wa kufanyia kazi wa Mola Muumba kwa ajili ya nyakati zote hususan kipindi hiki nyeti na muhimu cha umma wa Kiislamu, ambao iwapo utatekelezwa, basi mwamko wenye baraka wa Kiislamu utafikia malengo yake na kutengeneza historia.
Baada ya hutuba hiyo katika mkutano wa kwanza wa kimataifa wa Mwamko wa Kiislamu, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alijiunga na wasomi, maulamaa na wanafikra wanaohudhuria mkutano huo na kufanya mazungumzo nao. 861859




captcha