IQNA

Vijana wanamapinduzi wa Libya wakaribisha matamshi ya Ayatullah Khamenei

15:25 - September 18, 2011
Habari ID: 2189123
Vijana wanamapinduzi wa Libya wamekaribisha matamshi yaliyotolewa hivi karibuni na Ayatullahil Udhma Ali Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika kikao cha kwanza cha kimataifa cha Mwamko wa Kiislamu kinachoendelea hapa mjini Tehran.
Akizungumza katika mazungumzo na televisheni ya al-Alam Ashraf Qareh Bululi, mwakilishi wa vijana wanamapinduzi wa Libya amesema kwamba vijana hao wanakubaliana moja kwa moja na matamshi yaliyotolewa na Kiongozi Muadhamu katika kikao hicho cha kimataifa kuhusiana na Libya na kuongeza kuwa uingiliaji wa nchi za Magharibi nchini Libya umezidi kuharibu hali ya nchi hiyo na kupelekea kumwagika zaidi damu ya Walibya.
Bululi amesema kwamba vijana wanamapinduzi wa Libya wamekuwa na nafasi muhimu katika kufanikisha mapinduzi ya nchi hiyo. Amesema, nchi za Magharibi zinataka kuteka nyara mapinduzi yao kwa kutaka kuonyesha kwamba zimechangia sehemu kubwa katika kuyafanikisha katika hali ambayo fikra na uongozi wa maulamaa wa Kiislamu wa Libya ndio uliokuwa na nafasi kubwa zaidi katika kuyafanikisha.
Ametahadharisha dhidi ya njama zinazofanywa na wageni kwa ajili ya kupotosha malengo ya mapinduzi ya Libya na kuwataka Walibya wote kuwa macho ili kuvunja njama hizo. Amesema taifa la Libya halitaruhusu washirika au wafuasi wa dikteta aliyeng'olewa madarakani Muammar Gaddafi kuchukua tena madaraka ya nchi hiyo, kutokana na jinai kubwa walizotenda huko nyuma dhidi ya Walibya.
Katika hotuba yake aliyotoa jana katika ufunguzi wa kikao cha kimataifa cha Mwamko wa Kiislamu mjini Tehran, Ayatullah Ali Khamenei aliyataka mataifa ya kieneo yanayoshuhudia mapinduzi ya Kiislamu kutoiamini Marekani wala Nato na kufuatilia kwa karibu na makini malengo ya mapinduzi yao. 862680
captcha