IQNA

Kiongozi Muadhamu:

Kusimama kidete kwa taifa la Iraq mbele ya Marekani ni ukurasa wa dhahabu katika historia ya nchi hiyo

15:49 - October 30, 2011
Habari ID: 2214518
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei mapema leo amemkaribisha ofisini kwake Kiongozi wa eneo la Kurdistan la Iraq Bwana Mas'ud Barzani na ujumbe anaoandamana nao hapa nchini.
Ayatullah Khamenei ameashiria suala la usalama na kujitawala Iraq ya sasa na akasema kuwa, kusimama kidete kwa kaumu na madhehebu yote ya Iraq mbele ya mashinikizo ya Marekani, kupinga suala la kuwapa kinga ya kufikishwa mahakamani askari vamizi wa nchi hiyo na hatimaye kulazimika Marekani kuondoa majeshi yake huko Iraq ni ukurasa wa dhahabu katika historia ya nchi hiyo.
Amesema kuwa licha ya kuwepo kijeshi na kisiasa kwa Marekani huko Iraq na mashinikizo ya nchi hiyo, lakini Wairaqi wote Waarabu kwa Wakurdi na Shia na Suni wamesema "hapana" kwa Marekani, suala ambalo lina umuhimu mkubwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria hali ya kuishi pamoja kwa amani watu wa kaumu na madhehebu tofauti nchini Iraq na akasema: "Hali ya sasa ya uthabiti na utulivu ya Iraq inaifurahisha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na watu wa kaumu na madhehebu zote wanapaswa kushikamana kwa ajili ya kujenga Iraq mpya."
Amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono Iraq moja, iliyoungana na yenye utulivu na kuna udharura wa kukarabatiwa haraka uharibifu wote uliufanyika nchini humo ili Iraq iweze kurejea katika nafasi yake halisi.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa watu wa kaumu na madhehebu mbalimbali za Iraq ni ndugu wa karibu wa Iran na wana uhusiano wa kihistoria na wenzao wa Iran. Ametilia mkazo kwamba uhusiano wa sasa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Iraq ni mzuri lakini unapaswa kustawishwa zaidi siku baada ya siku.
Kwa upande wake Kiongozi wa eneo la Kurdistan la Iraq Mas'ud Barzani ameelezea kufurahishwa na kukutana kwake na Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu na ameitaja Iran kuwa ni nchi rafiki na iliyokaribu mno na wananchi wa Iraq. Amesema kuwa Wairaq kamwe hawatasahau ukarimu na misaada ya serikali na wananchi wa Iran katika kipindi kigumu cha Iraq.
Bwana Barzani amesisitiza kuwa kaumu na madhehebu mbalimbali za Iraq zinawajibika kufanya jitihada kubwa za kulinda ushindi wao na kwamba Iraq itaendelea kuhitajia misaada na mwongozo wa Iran. 889940
captcha