IQNA

Ayatullah Ali Khamenei:

Nara na kaulimbiu za taifa la Iran zimeenea katika Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika

21:41 - February 08, 2012
Habari ID: 2271558
Ayatullah Ali Khamenei ameitaja Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni mama wa mwamko wa Kiislamu wa Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika na kusema utawala wa Kiislamu wa Iran umo katika harakati ya kuelekea kwenye utambulisho halisi, wenye kudumu, imara na unaoweza kutetewa mbele ya hujuma mbalimbali.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo leo asubuhi katika kikao cha makamanda, maafisa na wafanyakazi wa Jeshi la Anga la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran waliokwenda kuonana naye katika Husainiya ya Imam Khomeini. Ayatullah Khamenei amesema kuwa darsa muhimu zaidi ya hatua ya kishujaa na kubwa ya Jeshi la Anga tarehe 19 Bahman 1357 (8 Februari 1979) ni kuelewa taathira za kuchukua hatua kwa wakati mwafaka na ulazima wa kufanya harakati ya kusonga mbele kwa matumaini ya mustakbali mwema. Ameongeza kuwa mabadiliko ya sasa katika nchi Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika na mwamko wa Kiislamu katika mataifa mbalimbali ni kielelezo cha kuwa na haki taifa la Iran na kudumishwa harakati ya taifa hilo ambayo ingali inasonga mbele kuelekea kwenye malengo yake makuu kwa nishati na kasi kubwa zaidi hata baada ya kupita miaka 33 sasa.
Katika kikao hicho ambacho kimefanyika kwa mnasaba wa kuadhimisha siku ya tarehe 19 Bahman 1357 (8 Februari 1979) ambapo kundi moja la makamanda wa Jeshi la Anga la Iran lilijitenga na utawala wa Shah na kutangaza utiifu wake kwa Imam Khomeini, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja siku hiyo kuwa ni tukio litakalokumbukwa siku zote na nukta ya kung’ara katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu. Amesema kuwa miongoni mwa masomo na ibra za tukio hilo la kihistoria ni somo la kuchukua hatua, kuwa na ubunifu, kusimama kidete na kufanya kazi kwa wakati unaofaa na taathira zake katika harakati ya jamii na nchi.
Amekumbusha hali nyeti ya kipindi cha mwezi Bahman 1357 (Februari 1979) na kusema, hatua iliyochukuliwa na makamanda wa Jeshi la Anga ya kumpa Imam Khomeini mkono wa utiifu katika kipindi hicho kigumu ilikuwa kazi kubwa sana iliyokuwa na taathira na iliyozidisha kasi ya gurudumu la mageuzi.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa nchi yoyote inayotaka kupata heshima, utambulisho, amani na kudhamini maslahi yake inahitajia ubunifu, uchapakazi na bidii.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa sababu kuu ya kubakia nyuma nchi za Kiislamu katika nyanja za maendeleo katika kipindi cha miaka mia moja iliyopita ni kughafilika na kutokuwa na harakati ya kusonga mbele inayonasibiana na zama husika na mustakbali. Ameongeza kuwa jambo linalokabiliana na mghafala ni mwamko ambao huleta harakati, na katika uwanja huo tunapaswa kufanya juhudi kubwa na kuhakikisha kwamba harakati yetu inakwenda kwa kasi zaidi kuliko ile ya kambi ya adui.
Amesema ili kuweza kuwa na kasi hiyo katika harakati inayosonga mbele kunahitajika juhudi kubwa zaidi za watu wote wa jamii hususan serikali, viongozi wa sekta mbalimbali na vikosi vya jeshi.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa mwamko wa Kiislamu katika Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika ni kielelezo cha kuwa katika haki Jamhuri ya Kiislamu na maendeleo ya harakati ya utawala wa Kiislamu. Ameongeza kuwa hii leo nara na kaulimbiu za taifa la Iran zimeenea katika maeneo hayo na nchi zilizokuwa tegemezi na waitifaki wa kambi ya ubeberu sasa ziko bega kwa bega na taifa la Iran na zinafuatilia malengo na nara za taifa hili.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa mabadiliko yaliyotokea kwenye eneo hili yameonyesha kwamba katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita taifa la Iran limeweza kupata wenza, wasaidizi na washirika.
Ayatullah Khamenei amesema: “Hatudai kuwa taifa la Iran ndilo lililofanya mabadiliko ya sasa katika Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika lakini halitakuwa jambo la kimantiki kupuuza taathira za mwamko wa taifa kubwa la Iran katika mwamko wa mataifa ya maeneo hayo.”
Ameitaja Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni mama wa mwamko wa Kiislamu wa Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika na kusema utawala wa Kiislamu wa Iran umo katika harakati ya kuelekea kwenye utambulisho halisi, wenye kudumu, imara na unaoweza kutetewa mbele ya hujuma mbalimbali.
Akifafanua zaidi suala hilo, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, miongoni mwa malengo aali na halisi ya mfumo wa Kiislamu hapa nchi ni kuwa na utambulisho wa Kiislamu, kumtegemea Mwenyezi Mungu Mtukufu, kuhisi fahari ya kuwa Muislamu, kutegemea uwezo na vipawa vya mtu binafsi, vya kijamii na kitaifa na maliasili tulizopewa na Mwenyezi Mungu na kuwalingania walimwengu thamani za kiroho na kimaanawi.
Ayatullah Khamenei amesema, ustaarabu wa kimaada wa Magharibi haukuweza kumtunuku mwanadamu hali bora na saada halisi na kuongeza kuwa, ulimwengu wa Magharibi na nchi zinazowafuata Wamagharibi hazikufaidi lolote katika mwenendo wao wa kughiriki katika umaada, kuenea uhuru wa maingiliajo ya kingono, kutupilia mbali masuala ya kiroho na kuchupa mipaka ya Mwenyezi Mungu; kwani mbali na kuwa hazikuweza kudhamini uadilifu, hali bora ya jamii nzima na usalama, mfumo wao wa familia na malezi ya vizazi vijavyo pia unakabiliwa na matatizo makubwa sana.
Amesisitiza kuwa ujumbe wa Jamhuri ya Kiislamu ni ujumbe wa masuala ya kiroho, thamani za Mwenyezi Mungu na kujikomboa kutoka kwenye harakati inayosababisha hali mbaya katika ulimwengu wa Magharibi.
Amesema pamoja na hayo, Uislamu sambamba na masuala ya kiroho, unatoa mazingatio makhsusi katika suala la kudhamini mahitaji ya kimaada ya mwanadamu kwa kiwango cha wastani na chenye mlingano.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa sherehe ambazo zimekuwa zikifanywa na wananchi wa Iran kuadhimisha Mapinduzi ya Kiislamu katika kipindi chote cha miaka 33 iliyopita hazina kifani duniani kote. Amesema kila mwaka na hata katika hali mbaya kabisa na hewa, mamilioni ya watu kote nchini hujitokeza mitaani tarehe 22 Bahman (11 Februari) na kusherehekea ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, suala ambalo ni ishara ya kuendelea harakati ya mapinduzi ya wananchi.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa tarehe 11 Februari mwaka huu, kwa taufiki yake Allah na uongozi wake, dunia nzima itaona jinsi wananchi wa Iran watakavyomiminika katika medani.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameliusia jeshi la Iran kustawisha zaidi masuala ya kiroho, kutakasa nafsi na kuboresha mafunzo na nidhamu. Amesema kuwa moja ya sifa za jeshi la Kiislamu ni kuwa na nidhamu sambamba na kuimarisha moyo wa udugu na kuwa tayari kwa ajili ya kujitolea na kujitoa mhanga katika njia ya Mwenyezi Mungu.
Mwanzoni mwa mkutano huo Brigedia Jenerali Shah Safi, Kamanda wa Jeshi la Anga la Iran ametoa mkono wa baraka kwa mnasaba wa kukumbuka tukio la kihistoria na hatua ya jeshi hilo kutangaza utiifu wake kwa mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu hayati Imam Khomeini na amewasilisha ripoti kuhusu mafanikio ya jeshi hilo. Brigedia Jenerali Shah Safi amesema kuwa utengenezaji wa makombora ya aina mbalimbali ya anga kwa ardhi, makombora dhidi ya rada, makombora ya leza na mabomu yanayolenga shabaha kwa ustadi mkubwa, kuzidishwa uwezo wa ndege ya kivita iliyotengenezwa hapa nchini na Swaiqa na kadhalika ni sehemu ndogo tu ya uwezo wa Jeshi la Anga la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 950437


captcha