IQNA

Ayatullah Imam Khamenei:

Maadui wameshindwa katika vita vya kidiplomasia mbele ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

23:13 - September 07, 2012
Habari ID: 2406712
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamemei mapema leo amekutana na kuhutubia Baraza la Wataalamu wanaomchagua kiongozi wa juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambapo amesema nchi hii kwa ujumla inapiga hatua nzuri za maendeleo.
Ameutaja mkutano wa viongozi wa nchi wanachama katika Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) uliofanyika siku chache zilizopita mjini Tehran kwamba ulikuwa maonyesho ya uwezo, ustawi na adhama ya utawala wa Kiislamu hapa nchini na kusema kuwa, maadui wa taifa la Iran walitumia ujahili wao na kuufanya mkutano huo kuwa vita vya kidiplomasia dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na matokeo yake ni kushindwa kwa fedheha na madhila maadui hao.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza juu ya udharura wa kuwa na mtazamo sahihi na wa kimantiki kuhusu hali ya Iran na kusema kuwa kutathmini masuala katika pembe mbalimbali ni ishara ya hali nzuri na inayofaa ya nchi hii na alama ya adhama ya Uislamu.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, kufanyika kwa mafanikio mkutano wa viongozi wa NAM mjini Tehran ni mfano mzuri wa hali bora ya mfumo wa kifikra iliyodhihirishwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa walimwengu.
Amesisitiza kuwa mkutano wa NAM mjini Tehran ulikuwa maonyesho ya nguvu, uwezo na adhama na kuongeza kuwa, chanzo na asili ya adhama hiyo ni fikra zilizohuishwa hapa nchini na Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) kutokana na mafundisho ya Uislamu na akazipanda na kuzikuza.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, mkutano wa viongozi wa nchi wanachama katika Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote wa mjini Tehran ungeweza kufanyika kama mikutano mingine ya kawaida ya kimataifa, lakini hali ya kisiasa ya dunia na wakati na mahala mkutano huo ulikofanyika na vilevile upumbavu wa wale wanaolitakia mabaya taifa la Iran vimeufanya mkutano huo kuwa tukio lenye taathira kubwa na kupewa mazingatio maalumu duniani na hata kuwa vita vya kidiplomasia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ayatullah Khamenei amesema zimefanyika jitihada na njama za kipropaganda za kufanyia sensa habari za mkutano huo na kuilazimisha Jamhuri ya Kiislamu isitangaze misimamo yake hususan dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel lakini mkutano huo umefanyika kwa mafanikio makubwa na njama hizo hazikuzaa matunda.
Ayatullah Khamenei amesema kushiriki kwa karibu thuluthi mbili ya nchi za dunia katika mkutano wa Tehran na kutayarishwa uwanja mzuri wa kutangazwa misimamo ambayo haitangazwi katika mikutano mingine ya kimataifa, ni miongoni mwa sifa kuu ya mkutano huo. Ameongeza kuwa misimamo iliyotangazwa na baadhi ya viongozi wa nchi na ujumbe mbalimbali katika mkutano huo hususan ukosoaji wa muundo wa Umoja wa Mataifa na baraza lake la usalama na vilevile udikteta wa kimataifa unaotawala dunia haijawahi kushuhudiwa katika mikutano mingine kama huo ya kimataifa.
Ayatullah Khamenei amesema moja ya matunda ya mkutano wa viongozi wa NAM mjini Tehran ni kuzima propaganda zinazodai kuwa Iran imetengwa. Amesema kuwa marais na ujumbe za ngazi za juu zilizoshiriki katika mkutano huo zimeshuhudia kwa karibu maisha ya kawaida na yaliyojaa nishati ya wananchi wa Iran katika mji mkuu Tehran na miji mingine hapa nchini na wameshauriana na maafisa wa Iran pambizoni mwa mkutano huo kuhusu mikataba mbalimbali.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa matokeo ya vita vya kidiplomasia vya wanaolitakia mabaya taifa la Iran yalikuwa kushindwa kwa fedheha na wapinzani wa utawala wa Kiislamu na vyombo vyao vya habari vikikiri uhakika huo.
Ayatullah Ali Khamenei ameashiria baadhi ya ibara zilizotumiwa na vyombo vya habari vya nchi za Magharibi vikisifu kushindwa kidiplomasia kwa nchi hizo kama vile “Iran yawazaba kibao wapinzani” na “Iran yatoa pigo kwa wale waliotaka kuitenga”, na akasema kuwa, kwa mujibu wa kanuni ya Qur’ani kila kazi na hatua inayomkasirisha adui huwa ni amali njema, kwa msingi huo kufanyika kwa mafanikio mkutano wa NAM mjini Tehran ilikuwa kazi na amali njema.
Ametadharisha kuwa katika masuala mbalimbali yakiwemo ya ndani ya nchi viongozi wanapaswa kuwa waangalifu ili wasitumbukie katika makosa kwenye uchambuzi wao.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kwa mujibu wa tathmini yake kuhusu mazingira ya sasa nchi hii inapiga hatua nzuri za maendeleo kwa ujumla.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa yumkini kukawapo udhaifu katika baadhi ya masuala ya kiutendaji na ya kifikra lakini tathmini ya masuala ya nchi inafanyika kwa kutilia maanani mambo yote chanya na maendeleo na nukta za udhaifu na hasi.
Mwanzoni mwa mkutano huo Mwenyekiti wa Baraza la Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatullah Mahdavi Kani amepongeza mijadala iliyozungumziwa katika mkutano wa 12 wa baraza hilo na akasema kuwa vikao hivyo vilikuwa na umuhimu kwani vimehudhuriwa na maulamaa wakubwa na wenye ushawishi kutoka maeneo yote ya nchi ambao wametoa maoni yao kuhusu masuala mbalimbali ya kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kimataifa.
Baada ya hapo Makamu Mwenyekiti wa baraza hilo Ayatullah Muhammad Yazdi ametoa ripoti kuhusu masuala muhimu yaliyojadiliwa kwenye mkutano huo. Amepongeza mafanikio ya mkutano wa NAM mjini Tehran na akasisitiza juu ya kukarabatiwa haraka maeneo yaliyoharibiwa na mtetemeko wa ardhi katika mkoa wa Azarbaijan Mashariki. 1092915
captcha