IQNA

Imam Khamenei:

Wazayuni wana lengo la kuzusha hitilafu katika Umma wa Kiislamu

22:24 - February 27, 2013
Habari ID: 2503640
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa matatizo mengi ya Umma wa Kiislamu ni ya kutwishwa na yaliyobuniwa na maadui wa Uislamu.
Ayatullah Khamenei ameyasema hayo leo katika mazungumzo yake na Rais Asif Ali Zardari wa Pakistan aliyeko safarini hapa nchini na kuongeza kuwa, kuhuishwa uwezo na vipawa vya kibinadamu, kimaumbile na kijiografia vya ulimwengu wa Kiislamu kunaweza kuwa na taathira kubwa katika kuondoa matatizo hayo.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa kuimarishwa na kupanuliwa zaidi uhusiano wa nchi za Kiislamu ni sababu ya pili muhimu inayoweza kusaidia juhudi za kutatua matatizo ya Waislamu. Ameongeza kuwa moja ya malengo ya Wazayuni na mabeberu wengine ni kuzusha hitilafu na mifarakano katika Umma wa Kiislamu.
Ameashiria uhusiano mzuri na wa kidugu uliopo kati ya Iran na Pakistan na akasema: "Tunaamini kwamba uhusiano wetu wa kiuchumi, kimiundombinu, kisiasa, kijamii na katika masuala ya usalama unapaswa kuimarishwa zaidi."
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa bomba la kusafirisha gesi kati ya Iran na Pakistan ni mfano mzuri wa ushirikiano wa Tehran na Islamabad. Ameashiria uadui na upinzani uliopo dhidi ya uhusiano mzuri wa nchi hizo mbili na akasema kuwa, kuna ulazima wa kuvuka upinzani huo kwa nguvu zote.
Amesema suala la kupata chanzo cha kuaminika na thabiti cha nishati lina umuhimu wa daraja la kwanza kwa nchi yoyote ikiwemo Pakistan na kuongeza kuwa, katika eneo hili Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndiyo nchi pekee yenye vyanzo vya kuaminika vya nishati na iko tayari kukidhi mahitaji ya Pakistan katika uwanja huo.
Ayatullah Ali Khamenei amekitaja kitendo cha kuzusha hitilafu za kimadhehebu nchini Pakistan kuwa ni vijidudumaradhi hatari kutoka nje ya nchi hiyo. Amesema kuwa mauaji yanayofanywa dhidi ya wafuasi wa madhehebu tofauti nchini Pakistan yanasikitisha mno na kuna udharura wa kukabiliana nayo ili yasivuruge umoja wa kitaifa wa Pakistan.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema ana matumaini kwamba serikali ya Pakistan itatatua matatizo hayo na kuongeza kuwa, anatarajia kuwa serikali ya Rais Asif Ali Zardari itaimarisha umoja kati ya madhehebu na kaumu tofauti na kupata mafanikio katika masuala ya ustawi.
Kwa upande wake Rais Asif Zardari wa Pakistan ameeleza kufurahishwa kwake na kukutana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na akasema kuwa anaamini kwamba uhusiano wa pande hizo mbili unapaswa kuimarishwa zaidi.
Rais wa Pakistan amesema kuwa njama za madola makubwa za kutaka kuzuia juhudi za kuimarishwa uhusiano wa Iran na Pakistan zimegonga mwamba kwa sababu mataifa hayo mawili yameelewa jinsi ya kukabiliana na maadui wa Uislamu.
Asif Zardari amesema kuwa maadui wanafanya njama za kuanzisha vita vya ndani nchini Pakistan na kuongeza kuwa serikali yake haitaruhusu njama hizo. 1196321
captcha