IQNA

Ayatullah Khamenei:

Vyombo vya habari na wasanii wanapaswa kutangaza jihadi kubwa ya wanawake wa Iran

22:03 - March 06, 2013
Habari ID: 2507533
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei ametuma ujumbe katika kongamano la "Mashahidi Elfu Saba wa Kike" akiutaja mchango wa wanawake Waislamu wa Iran katika kuonesha kigezo bora na kipya kuwa ni wa kihistoria.
Ameashiria kujitokeza wanawake wenye moyo wa Kikarbala katika harakati ya Mapinduzi ya Kiislamu na kujitetea kutakatifu na akasema kuwa, kumejitokeza uwezo na mvuto mpya katika zama za sasa kwa baraka ya damu ya wanawake hao ambao utakuwa na taathira katika hatima na nafasi ya wanawake duniani.
Katika ujumbe huo ambao umesomwa na mwakilishi wa Faqihi Mtawala katika Taasisi ya Shahidi, Hujjatul Islam Walmuslimin Rahimian, Ayatullah Khamenei amewakumbuka mashahidi wa kike wa Iran ya Kiislamu ambao walitoa mchango mkubwa katika kubadili historia ya Uislamu na akasema kuwa, askari hawa malaika ambao walisabilia roho zao tukufu kwa ajili ya Uislamu waliingia katika uwanja wa jihadi na kudhihiri kama wahandisi wa Iran mpya.
Ameashiria mtazamo wa sasa wa mifumo ya Mashariki na Magharibi kuhusu mwanamke ambaye anatambuliwa kama kitu cha daraja la pili au chombo cha kushibisha matamanio ya ngono ya wanaume na ameweka wazi mchango wa mashujaa hao wa kike wa Iran katika Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini na katika vita vya kujitetea kutakatifu. Amesema wanawake hao wamekuwa kigezo kipya cha kaulimbiu ya "Mwanamke Asiyekuwa wa Mashariki wala Magharibi".
Akiweka wazi sifa makhsusi za kigezo hicho, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa: "Mwanamke Muislamu wa Kiirani amefungua historia mpya mbele ya macho ya wanawake duniani na kuthibitisha kwamba, inawezekana kuwa mwanamke, kulinda utakasifu, vazi la hijabu na heshima na wakati huo huo kushiriki katika medani ya mapambano na kutoa mchango mkubwa."
Amesema kuwa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na vita vya kujitetea kutakatifu ulikuwa uwanja wa kujitokeza na kudhihiri wanawake ambako kumechanganya pamoja hisia, huruma na rehma za kike na roho ya jihadi, kufa shahidi na mapambano, na kushinda vita katika medani za wanaume kwa ushujaa, ikhlasi na kujitolea kwao. Amesema wanawake hao wanaweza kushinda vizuizi vikubwa.
Vilevile ameashiria athari nyingi za jihadi ya wanawake waliouawa shahidi na kusema kumejitokeza uwezo na mvuto mpya katika zama za sasa kwa baraka ya damu ya wanawake hao ambao kwanza umewaathiri wanawake katika ulimwengu wa Kiislamu na utakuwa na taathira katika hatima na nafasi ya wanawake duniani.
Amekumbusha mchango na nafasi ya wanawake adhimu katika historia ya Uislamu na kusema kuwa, maadamu jua angavu la Bibi Khadija, Fatimatu Zahraa na Zainab Kubra bado linang'ara, basi njama za kale na mpya zinazofanywa dhidi ya wanawake hazitakuwa na mafanikio.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa maelfu ya wanawake wetu waliofuata sera za Karbala si tu kwamba wameweza kushinda dhulma za kidhahiri bali pia wameshinda dhulma za kisasa dhidi ya wanawake, kuzifichua na kuzifedhehesha na kuonesha kuwa, haki za utukufu wa mwanamke alizopewa na Mwenyezi Mungu ndio haki za juu zaidi za mwanamke ambazo hazijaeleweka katika dunia eti iliyostaarabika na sasa ni wakati wa kueleweka kwake.
Ayatullah Khamenei amesisitiza juu ya udharura wa kuwadhihirishia walimwengu jihadi kubwa iliyofanywa na wanawake Waislamu wa Iran na kusema anatajia kuwa, kwa baraka za damu ya wanawake hao sharifu na wapiganaji wa jihadi, vyombo vya habari, wasanii, wasomi na wadau wa sekta ya filamu wataweza kutangaza jihadi kubwa ya mwanamke Muislamu wa Iran kwa walimwengu. 1200280

captcha