IQNA

Utawala wa Kizayuni wabomoa tena msikiti wa Wapalestina huko Negev

11:27 - January 30, 2016
Habari ID: 3470097
Utawala haramu wa Israel umebomoa mskiti katika kijiji kimoja cha Wapalestina katika Jangwa la Negev, ikiwa ni mara ya pili kubomolewa msikiti huo mwezi huu.

Imearifiwa kuwa, wanajeshi wa Israel wakiwa na mabuldoza jana waliubomoa kikamilifu msikiti wa kijiji cha Rakhama pamoja na kuharibu vitu vyote vilivyokuwemo ndani ya msikiti huo ikiwa ni pamoja na vitabu na nakala za Qur'ani tukufu. Msikiti huo ulikuwa umebomolewa mapema mwezi huu lakini wakaazi waliujenga upya. Ripoti zinasema, askari wa Kizayuni hawakuwaruhusu wakaazi hao wa kijiji cha Rakhama hata kuzishamisha nakala za Qur'ani zilizokuwemo msikitini humo.

Utawala haramu wa Israel umesema hautambui kijiji hicho kilichoko katika mji wa Yeruham na hivyo kimenyimwa suhula za kielimu na kiafya.

Mbunge wa Palestina Abu Arar ameukosoa utawala haramu wa Israel kwa kutotambua vijiji 40 katika Jangwa la Negev ambalo liko katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu tangu mwaka 1948 na kupewa jina la Israel.

Israel inatumia ardhi ilizozipora za Wapalestina kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni, hatua ambayo Umoja wa Mataifa umesema ni kinyume cha sheria.

Zaidi ya Waisraeli nusu milioni wanaishi katika vitongoji 230 haramu vilivyojengwa katika ardhi za Palestina zilizoghusubiwa mwaka 1967 katika Ukingo wa Magharibi na Quds Mashariki.

3471132

captcha