IQNA

Mwanamke Mwislamu aliyevaa Hijabu New York achomwa moto

19:30 - September 14, 2016
Habari ID: 3470562
Katika kitendo kingine cha chuki dhidi ya Waislamu, mwanamke aliyekuwa amevaa Hijabu ameshambuliwa na kuchomwa moto mjini New York, Marekani.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Bi. Nemariq Alhinai mwenye umri wa miaka 35 na ambaye ni daktari wa meno kutoka Scotland alikuwa akinunua bidhaa mjini New York wakati aliposhambuliwa na mtu aliyeiwasha moto nguo aliyokuwa amevalia. Daktari Alhinai anasema akiwa anatembea nje ya maduka alihisi joto katika nguo aliyokuwa amevalia na kisha akagundua nguo yake ilikuwa inateketea moto uliowashwa kwa makusudi na mwanaume aliyekuwa anatembea karibu naye. Polisi wamesambaza video kutoka kamera za usalama (CCTV) ambazo zinaonyesha taswira ya mtenda jinai aliyekuwa amekusudia kumdhuru mwanamke huyo Mwislamu kutokana na vazi lake la Hijabu.

Daktari Alhinai alifanikiwa kuzima miale ya moto na hakupata majeruhi katika shambulizi hilo ambalo lilijiri Jumamosi, siku moja tu kabla ya maadhimisho ya hujuma za Septemba 11 miaka 15 iliyopita. Kufuatia tukio hili Bw. Albert Cahn Mkurugenzi wa Sheria katika Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani CAIR amebainisha wasiwasi wa kundi hilo kutokana na ongezeko la mashambulizi dhidi ya Uislamu Marekani.

"CAIR ina wasi wasi kutokana na ongezeko la mashambulizi dhidi ya Waislamu mjini New York na kote Marekani. Hili ni jambo ambalo sit u kuwa linapaswa kuwatia wasiwasi Waislamu, bali pia Wamarekani wote," amesema Cahn.

3460932

captcha