IQNA

Spika wa Bunge la Iran

Syria iko mstari wa mbele katika vita dhidi ya ugaidi

9:53 - November 08, 2016
Habari ID: 3470663
IQNA-Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa daima Syria imekuwa katika mstari wa mbele wa muqawama na mapambano dhidi ya ugaidi na Uzayuni.

Ali Larijani amesema hayo Jumatatu mjini Tehran katika mazungumzo yake na Faisal Mekdad, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Syria na kuongeza kuwa Damascus imekuwa ikifanya mambo kwa mizani na hekima kwa ajili ya kuupatia ufumbuzi wa kisiasa mgogoro wa nchi hiyo.

Akiendelea kubainisha kuhusu masuala ya Mashariki ya Kati hususan Syria na mapambano dhidi ya makundi ya kitakfiri na kigaidi Larijani amesema uhusiano wa Iran na Syria ni tajiri na wa kiistratejia na kwamba, Tehran itaendelea kuiunga mkono serikali ya Damascus.

Amesisitiza kwamba, uhusiano wa nchi mbili hizi ni mkongwe, wa kirafiki na wa kihistoria. Ameongeza kuwa, katika mazingira ya sasa ambapo kuna hujuma kubwa dhidi ya Syria, kuna haja ya kuongezwa ushirikiano wa nchi hizo katika uwanja wa kisiasa na kiuchumi.

Dakta Ali Larijani amesisitiza pia juu ya udharura wa kuimarishwa zaidi uhusiano wa kisiasa na kieneo na Syria na kuongeza kuwa, siasa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kupambana na ugaidi na kuhakikisha amani na uthabiti unarejea katika eneo la Mashariki ya Kati.

Katika upande mwingi Spika wa Bunge la Iran amesema kuna haja ya kudumishwa umoja na ushirikiano baina ya nchi za Kiislamu kwa ajili ya kupambana na matatizo yaliyoko ndani ya Ulimwengu wa Kiislamu na kutanabahisha kwamba, madola makubwa na ya kikoloni ndiyo yanayonufaika na hitilafu baina ya nchi za Waislamu.

Wakati huo huo Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Kistratejia cha Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo wa Kiislamu wa Iran amesema kuwa, ndoto za maadui za kutaka kuanzisha eneo salama kwa ajili ya Wazayuni katika Mashariki ya Kati hazitatimia.

Ali Akbar Velayati alisema hapo jana alipokutana na kufanya mazungumzo hapa mjini Tehran na Faisal Mekdad, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Syria na kubainisha kwamba, Iran inaipongeza serikali na taifa la Syria kutokana na kuwa mstari wa mbele katika kupambana na kambi ya ukoloni, Uzayuni na nchi zinazpinga mwamko katika Mashariki ya Kati hususan Saudi Arabia.

captcha