IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Bibi Fatima alikuwa dhihirisho la ukamilifu wa mwanamke wa Uislamu

23:19 - March 19, 2017
Habari ID: 3470901
TEHRAN (IQNA)-Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema Bibi Fatima SA alikuwa dhihirisho la ukamilifu wa mwanamke wa Uislamu na alifikia daraja la juu la 'mwanamke wa Kiislamu' yaani kiasi cha kuitwa 'kiongozi'.
Ayatullah Sayyed  Ali Khamenei, Kiongozi wa Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo leo mjini Tehran kwa mnasaba wa sherehe ya siku ya kuzaliwa Bibi Fatima Zahraa SA binti wa Mtume Muhammad SAW alipokutana na wasomaji wa tungo za kumsifu Mtume na Ahlu Baiti wake AS. Amesisitizia pia umuhimu wa kuelewa nafasi chanya ya mwanamke wa Kiislamu. 
Kiongozi Muadhamu amesema kuna uwezekano mkubwa kwamba kumfanya mwanamke kuwa chombo cha anasa katika ulimwengu wa Magharibi, ni sehemu ya njama za Wazayuni kwa ajili ya kusambaratisha jamii ya mwanadamu.
Sambamba na kubainisha sababu ya kuenezwa nara za kama ile ya 'uadilifu na usawa wa kijinsia' katika nchi za Magharibi, amesema kuwa uadilifu ni kutambua vipawa na tunu alizopewa na Mwenyezi Mungu kuzistawisha.
Kiongozi Muadhamu amesema kuwa, hii leo wasomi wa Magharibi na watu wanaonadi usawa wa kijinsia wanajutia hatua yao hiyo kutokana na makosa mengi yanayosababishwa na suala hilo. Vilevile ameashiria sira na harakati adhimu ya Bibi Fatima Zahraa AS, mwanamke mtukufu wa Kiislamu katika nafasi ya kiongozi halisi na wakati huo huo kama mke na mama wa aina yake na kumtaja kuwa ni kiigizo chema na kamili kwa ajili ya Waislamu.' 

Itakumbukwa kuwa, siku kama ya leo miaka 1446 iliyopita yaani sawa na tarehe 20 Jamadu th-Thani mwaka wa nane kabla ya Hijiria, alizaliwa Bibi Fatima Zahraa SA Binti ya Mtukufu Mtume Muhammad SAW. Tangu utotoni mwake, Bibi Fatima alikulia katika nyumba ya wahyi na chini ya malezi bora ya baba yake Nabii wa Allah na hivyo kufikia daraja la juu la ukamilifu katika elimu na ubora. Aidha Bibi Fatimah SA alikuwa na nafasi muhimu katika kupunguza machungu na tabu zilizokuwa zikimkumba baba yake katika harakati za kueneza mafundisho ya dini ya Uislamu, kutoka kwa washirikina.

 Mwaka wa pili Hijiria binti huyo mtukufu wa Mtume alifunga ndoa kwa sherehe nyepesi sana na Imamu Ali Bin Abi Twalib, ambaye naye ni dhihirisho la haki, uadilifu na uchaji-Mungu. Akiwa na Imamu Ali SA  Bibi Fatimah aliishi kwa Amani na furaha ya juu huku akitekeleza majukumu ya mke na mama mwema kwa watoto wake watukufu, yaani Imamu Hassan AS, Imamu Hussein AS na Bibi Zainab SA.

captcha