IQNA

Marekani yalaaniwa vikali kwa kuivamia Syria kijeshi

19:28 - April 07, 2017
Habari ID: 3470921
TEHRAN (IQNA)-Marekani imelaaniwa vikali kwa kutekeleza hujuma iliyo kinyume cha sheria dhidi ya Syria Ijumaa alfajiri na kulenga kituo cha kijeshi ambacho hutumiwa na ndege zinazowashambulia magaidi wa ISIS.

TEHRAN (IQNA)-Marekani imelaaniwa vikali kwa kutekeleza hujuma iliyo kinyume cha sheria dhidi ya Syria Ijumaa alfajiri na kulenga kituo cha kijeshi ambacho hutumiwa na ndege zinazowashambulia magaidi wa ISIS.

Ikulu ya Rais Bashar al-Assad wa Syria imesema kuwa, mashambulizi ya Marekani dhidi ya kambi ya kikosi cha anga cha nchi hiyo katika eneo la Shayrat, mashariki mwa Syria ni hatua ya kijinga na inayotokana na mtazamo finyu wa kisiasa na kijeshi.

Taarifa iliyotolewa leo na ikulu ya rais wa Syria imesema kuwa, hujuma hiyo ya Marekani ni uvamizi wa kidhalimu ulio wazi na kwamba, mienendo ya kindumiakuwili ya Washington ndiyo imeifanya nchi hiyo kufanya kitendo hicho cha kijinga nchini Syria. Wakati huo huo Bouthaina Shaaban, Mshauri wa Rais wa Syria katika masuala ya Habari na Siasa amesema kuwa, shambulizi la Marekani nchini humo limemuondolea shaka kila mtu kwamba Washington iko safu moja na magaidi katika kupambana na serikali ya Syria.

Mashambulio hayo ya Marekani kwa kisingizio cha kuhusika serikali ya Syria katika shambulio la silaha za kemikali kwenye mji wa Khan Sheikhoun yamefanywa katika hali ambayo, akijibu tuhuma hizo zisizo na msingi zilizowasilishwa na wawakilishi wa Marekani, Ufaransa na Uingereza katika Umoja wa Mataifa, Mundhir Mundhir, naibu wa mwakilishi wa kudumu wa Syria katika huo alisema hapo jana kuwa serikali ya Damascus imeuandikia Umoja wa Mataifa barua zaidi ya 90 ambazo ndani yake zimeonyesha ushahidi kamili kuhusu utumiaji silaha za kemikali unaofanywa na magaidi dhidi ya raia madhulumu wa Syria.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali hatua ya Marekani kuushambulia kwa makombora mkoa wa Homs ulioko magharibi wa Syria, kwa kisingizio cha 'kuiadhibu' Syria kwa shambulio la silaha za kemikali inayodai lilifanywa na serikali ya Damascus katika mji wa Khan Sheikhoun.

Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, kitendo hicho cha Marekani ni uvamizi hatari unaokanyaga sheria za kimataifa, na kwamba huenda hatua hiyo ikayapa nguvu magenge ya kigaidi katika nchi hiyo ya Kiarabu.

Wakati huohuo, Dmitry Peskov, Msemaji wa Rais wa Russia amesema Vladimir Putin anaamini kuwa mashambulizi hayo ya Marekani dhidi ya Syria ni kinyume cha sheria za kimataifa na kuonya kuwa yumkini hatua hiyo ikawa na taathira hasi kwa uhusiano wa Washington na Moscow.

Amekariri kuwa, serikali ya Syria haina silaha za kemikali na kwa msingi huo, Marekani imebuni tu madai yasiyo na msingi ili iweze kuishambulia nchi hiyo.

Kadhalika baadhi ya wabunge wa Kongresi ya Marekani wamekosoa vikali mashambulizi hayo dhidi ya Syria, na kusisitiza kuwa operesheni hiyo ni sawa na Washington kutangaza vita huku wakisisitiza udharura wa bunge hilo kuitisha kikao cha dharura kujadili kadhia hiyo.

Huku hayo yakiarifiwa, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, Benjamin Netanyahu amempongeza Rais Donald Trump kwa alichokiita 'ujasiri' wa kuagiza kutekelezwa mashambulio hayo dhidi ya Syria. Wakati huohuo, Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan naye amesema Ankara iko tayari kushirikiana na Marekani iwapo itaamua kuishambulia kijeshi Syria. Saudi Arabia pia sawa na magaidi wa ISIS kwa pamoja wamepongeza hujuma hiyo ya Marekani dhidi ya Syria.

3587510
captcha