IQNA

Utawala Bahrain wamfunga Sheikh Qassim mwaka moja gerezani, wananchi waandamana kulaani hukumu

14:05 - May 21, 2017
Habari ID: 3470987
TEHRAN (IQNA)-Utawala wa Aal Khalifa wa Bahrain umemuhukumu mwanazuoni wa Kiisalmu Sheikh Issa Qasim kifungo cha mwaka mmoja na kuibuaasira za wananchi ambao wameandamana wakiwa wamevaa sanda, kupinga hukumu hiyo ya kidhulma.

Hukumu hiyo imetolewa katika hali ambayo wananchi wa Bahrain wameitikia mwito wa maulamaa wa nchi hiyo wa kujitokeza kwa wingi misiktini na kuonesha hamasa nyingine ya kuihami dini yao na kumuunga mkono Sheikh Issa Qassim aliyepewa adhabu hiyo na mahakama ya nchi hiyo baada ya kufungwa kifungo cha nyumbani kwa muda wa wiki 44.

Kabla ya hapo mahakama ya Bahrain ilikuwa imepanga kusoma hukumu hiyo tarehe saba mwezi huu wa Mei, hata hivyo iliakhirisha jambo hilo kwa kuhofia hasira za wananchi.

Tokea tarehe 14 Februari mwaka 2011, Bahrain imekuwa ikishuhudia harakati ya mwamko wa Kiislamu dhidi ya ukandamizaji na mbinyo wa watawala wa ukoo wa Aal Khalifa. Wananchi hao wanataka kuweko uhuru, uadilifu, kuondolewa ubaguzi na kuingia madarakani serikali iliyochaguliwa na wananchi. Utawala huo ukiwa na lengo la kuzima sauti na cheche za moto wa malalamiko hayo umewatia mbaroni wanaharakati wa kisiasa, vijana na raia wengine wa nchi hiyo na kuwahukumu vifungo vya muda mrefu jela.

Kwa hakika matukio ya Bahrain ni kiashiria cha kuzidi kutokota hali ya kisiasa ya nchi hiyo. Hali hiyo inatokana na hatua zisizo na nadhari na za utumiaji mabavu za utawala wa ukoo wa Aal Khalifa. Mwenendo huo umezusha wasiwasi mtawalia miongoni mwa fikra za waliowengi ulimwenguni. Hii ni katika hali ambayo, wananchi wa Bahrain licha ya kukabiliwa na mbinyo na ukandamizaji wa utawala wa kifamilia wa Aal Khalifa pamoja na madola yanayouunga mkono, wangali wamesimama kidete na wameazimia kuendelea na harakati yao hadi watakapofanikiwa kupata haki zao.

3462897

captcha