IQNA

14:39 - September 13, 2017
News ID: 3471171
TEHRAN (IQNA)-Halima Yacob amechaguliwa Jumatano kuwa mwanamke wa kwanzi rais wa Singapore.

Bi. Halima, ambaye aliwahi kuwa spika wa bunge la nchi hiyo ametangazwa kuwa mshindi baada ya kukosekana mpinzani aliyetimiza masharti ya kuchuana naye katika kinyang'anyiro cha urais wa Singapore.

Kwa lengo la kuleta maelewano na kuwafanya wote wahisi wanajumuishwa katika utawala, Bunge la Singapore limepitisha sheria kuwa nafasi ya urais mara hii ipewe watu wa jamii ya waliowachache wa Malay ambao aghalabu ni Waislamu.

Akizungumza baada ya kutangazwa kuwa rais, Bi Halima, mwanamke Mwislamu anayevaa Hijabu, amesema ingawa mfumo maalumu umetumiwa kumchagua lakini atakuwa rais wa Wasingapori wote.

Uzoefu wa Bi. Halima kama spika wa bunge unatazamiwa kumsaidia kuiongoza nchi hiyo tajiri ya Asia ya Kusini-Mashariki ingawa kwa mujibu wa sheria za Singapore waziri mkuu ndie mwenye mamlaka zaidi.

Mmalay wa mwisho kushika urais Singapore alikuwa ni Yusof Ishak ambaye alitawala kati ya mwaka 1965 hadi 1970, miaka ya awali ya uhuru wa nchi hiyo ambayo ina muundo wa dola-mji (city state) yaani dola ambalo eneo lake ni mji mmoja pekee.

Kati ya wakazi milioni tano na nusu walio wengi (kama robo tatu) ni wa asili ya China. Mababu wao walihamia huko wakitafuta kazi bandarini.

Wengine ni wakazi asilia Wamalay (13.4%) na Watamil na wengineo waliotokea Uhindi (9.2%).

Kuna lugha 24 ambazo huzungumzwa nchini Singapuri. Lugha rasmi ni Kiingereza (32%), Kimalay (12%), Kichina (50%) na Kitamil (3%). Upande wa dini, 33% ni Wabuddha, 18% ni Wakristo, 15% ni Waislamu, 11% ni Watao, 5% ni Wahindu.

3463901

Name:
Email:
* Comment: