IQNA

Tamasha la Qur'ani lafanyika Ukanda wa Ghaza

19:44 - November 03, 2017
Habari ID: 3471245
TEHRAN (IQNA)-Tamasha la 'Waumini wa Qur'ani Tukufu na Ukombozi wa Msikiti wa Al Aqsa' limefanyika katika Msikiti wa Ammar ibn Yasir katika eneo la Palestina la Ukanda wa Ghaza.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, tamasha hilo lilihudhuriwa na maafisa wa ngazi juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, pamoja na watu kutoka matabaka mbali mbali.

Nasim Yasin, afisa wa Hamas, amesema waumini misikitini na makundi ya kusoma Qur'ani wana nafasi muhimu katika kuandaa njia ya uhuru na ukombozi wa Palestina. Aidha amesema kuna umuhimu kwa vijana kufunzwa Qur'ani Tukufu.

Wakati huo huo hafla nyingine yenye anuani ya , "Umoja, Njia ya Uhuru" imefanyika katika Msikiti wa Hamza ibn Abdul Muttalib mashariki mwa Ghaza ambapo waliohifadhi Qur'ani Tukufu walienziwa na kutunukiwa zawadi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mahir Sabra, afisa wa harakati ya Hamas, amesisitiza kuhusu ulazima wa kuwapa mafunzo zaidi wanaohifadhi Qur'ani ili wajiimarishe katika taaluma hiyo.

Tokea mwaka 2007, utawala haramu wa Israel uliweka mzingira wa anga, nchi kavu na baharini dhidi ya Ukanda wa Ghaza baada ya Wapalestina katika eneo hilo kuichagua kidemokrasia harakati ya Hamas kuongeza eneo hilo. Mzingiro huo umelifanya eneo hilo lenye watu karibu milioni moja na nusu kutajwa kuwa gereza kubwa zaidi la wazi duniani.

Mbali na mzingiro huo, utawala haramu wa Israel pia umeanzisha vita mara tatu dhidi ya Ghaza tokea mwaka 2008 ambapo maelfu ya Wapalestina wakiwemo wanawake na watoto wameuawa.

Pamoja na hayo wakaazi wa Ghaza, hawajapoteza matumaini, na kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu, wanaendeleza harakati zao za kila siku huku wakiapa kuendeleza mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

3658241/

captcha