IQNA

Zarif: Iran haitaki vita lakini iko tayari kujilinda

17:06 - January 01, 2021
Habari ID: 3473512
TEHRAN (IQNA) - Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameionya vikali Marekani kwa kupiga ngoma ya vita na kusisitiza kuwa, taifa hili lipo tayari kujilinda.

Katika ujumbe wa Twitter, Mohammad Javad Zarif ameandika: Badala ya kupambana na Covid-19 nchini Marekani, Donald Trump na wapambe wake wanapoteza mabilioni ya dola kurusha ndege za kijeshi aina ya B52 na kutuma msafara wa manowari za kivita katika eneo letu.

Dakta Zarif ameeleza bayana kuwa, duru za kiitelijensia kutoka Iraq zimeashiria kuwa, Marekani inapika jungu la kutaka kuhalalisha njama zake za kuanzisha vita katika eneo hili la Asia Magharibi.

Amebainisha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitaki vita lakini iko tayari kuwalinda wananchi wake, usalama na maslahi yake muhimu katika eneo.

Indhari hii ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran imetolewa katika hali ambayo, duru za kiusalama zimeripoti kuwa ndege za kivita za Marekani zimeonekana zikiruka katika eneo la Ghuba ya Uajemi, huku kukiwa na mpasuko baina ya maafisa wa Ikulu ya White House juu ya kuanzisha au kutoanzisha vita dhidi ya Iran.

3944719

Kishikizo: iran vita zarif marekani
captcha