IQNA

Iran yatumai uhusiano mwema na Saudia utasaidia kutatua matatizo ya Ulimwengu wa Kiislamu

17:08 - February 04, 2022
Habari ID: 3474889
TEHRAN (IQNA)- Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, Iran na Saudi Arabia ni nchi muhimu katika eneo na Ulimwengu wa Kiislamu na akaeleza kwamba ana matumaini ushirikiano baina ya nchi hizo mbili utasaidia kutatua matatizo ya eneo na ya Ulimwengu wa Kiislamu.

Hossein Amir-Abdollahian ameyasema hayo katika mazungumzo aliyofanya kwa njia ya simu na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC, Hussein Ibrahim Taha, ambapo wawili hao wamejadili na kubadilishana mawazo kuhusu masuala ya Ulimwengu wa Kiislamu na Umma wa Kiislamu, mwenendo wa uhusiano na ushirikiano wa pande mbili na pande kadhaa kati ya Iran na OIC, kufunguliwa tena ofisi ya uwakilishi wa Iran katika jumuiya hiyo na baadhi ya masuala mengine ya kikanda yanayopewa umuhimu na pande mbili.

Aidha, Amir-Abdollahian amepongeza na kushukuru jitihada zilizofanywa na Katibu Mkuu wa Jumuiya Ushirikiano wa Kiislamu kwa ajili ya kufanikisha kufunguliwa tena ofisi ya uwakilishi wa Iran katika Sekretarieti ya jumuiya hiyo mjini Jeddah.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa OIC Hussein Ibrahim Taha amekaribisha kufunguliwa tena ofisi ya uwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika jumuiya hiyo na kuanza shughuli zake kwa uamilifu na akasema, mchango wa Iran, ambayo ni mwanachama hai na mwasisi katika OIC, ni athirifu na wenye umuhimu mkubwa.

Halikadhalika, Ibrahim Taha amesisitiza, "bila ushiriki na kutoa mashirikiano amilifu nchi zote za Kiislamu, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu haitakuwa na uwezo wa kutatua matatizo ya Ulimwengu wa Kiislamu; nasi tunawataka ndugu zetu na wanachama waiunge mkono kikamilifu jumuiya hii."

Katibu Mkuu wa OIC vilevile amesema, anaunga mkono mchakato wa mazungumzo kati ya Iran na Saudi Arabia na akasisitiza kuwa, kujitokeza matatizo kati ya nchi za Kiislamu kunaumiza na kunasikitisha na kwamba jumuiya hiyo inazitolea mwito nchi ndugu za Waislamu kuzungumza na kufikia suluhu.

668877

captcha