IQNA

Watetezi wa Palestina

Mufti wa Tajikistan: Umoja wa Waislamu ni muhimu kuikomboa Palestina

11:59 - January 30, 2024
Habari ID: 3478277
IQNA - Mufti Mkuu wa Tajikistan amesisitiza ulazima wa kuwepo umoja katika ulimwengu wa Kiislamu ili kuiokoa Palestina kutokana na ukandamizaji na kukaliwa kwa mabavu.

Katika mahojiano na IQNA, Sheikh Saidmukarram Abdulkadirzoda alisema kuwa zaidi ya wakati wowote, Palestina inahitaji umoja wa ulimwengu wa Kiislamu leo.

Alipoulizwa kuhusiana na hali mbaya ya Palestina hususan katika Ukanda wa Gaza na ukosefu wa jibu sahihi kutoka kwa ulimwengu wa Kiislamu amesema sababu ya kimsingi ni udhaifu wa ulimwengu wa Kiislamu unaotokana na mifarakano na mizozo baina ya Waislamu

Kama rais wa Iran alivyosema kwa busara katika mkutano wa kimataifa wa hivi majuzi mjini Tehran, kama Umma wa Kiislamu utaamua kuweka kando tofauti na kusaidiana, hakutakuwa na dhuluma dhidi ya Waislamu popote duniani, msomi huyo amebainisha.

Katika hali hiyo, Waislamu watakuwa na nguvu kubwa, lakini leo, kwa bahati mbaya, kuna tofauti za kisiasa na baadhi ya migogoro kati ya Waislamu, alibainisha.

Sheikh Abdulkadirzoda alisema nguvu za uovu hutumia tofauti hizi na kuwasababishia Waislamu mateso makubwa.

Alitumai Waislamu watageuza mwelekeo huo na kuelekea kwenye mshikamano na umoja na kusaidiana.

Amesisitiza kuwa tofauti hizo ziko katika sehemu ndogo tu ya imani ambapo Waislamu wote wana imani ya pamoja katika masuala mengi mno kama  vile imani na Qur'ani Tukufu na Mtume (SAW) na wanaswali kuelekea Kibla kimoja.

Mufti Mkuu wa Tajikistan amesema wanazuoni wa Kiislamu ambao ni watumishi wa Uislamu pamoja na wanasiasa na wasomi wa fani nyingine wanapaswa kufanya kazi ili kuwaongoza Waislamu kwenye njia ya umoja.

Vile vile ameashiria fikra za hayati muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Imam Khomeini (RA) na shakhsia wengine wa Kiislamu ambao waliwahamiza Waislamu duniani kote kuimarisha umoja wao na kusema hayo ni mafundisho yenye msingi wa Qur'ani Tukufu.

Kwa mujibu wa Aya ya 92 ya Sura Al-Anbiya, “Kwa hakika huu umma wenu ni umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu Mlezi. Kwa hivyo niabuduni Mimi.”

Kwa msingi huo amesema Waislamu ni Ummah mmoja na wanapaswa kuungana hata kama wana tofauti za kifiqhi, akamalizia.

4194891

captcha