IQNA

Waislamu kote duniani waadhimisha Mawlid ya Mtume SAW

12:17 - January 03, 2016
Habari ID: 3470001
Wiki ya Umoja wa Kiislamu inamalizika leo Jumanne huku Waislamu kote ulimwenguni wakiendelea kuadhimisha Maulidi ya kukumbuka kuzaliwa Mtume wa mwisho, Muhammad al Mustafa SAW.

Tarehe ya leo inasadifiana pia na kumbukumbu za siku ya kuzaliwa Imam Jafar Sadiq AS.

Mkutano wa 29 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu ambao umeshirikisha wanazuoni, wanafikra na wasomi kutoka nchi 70 duniani unatazamiwa kufunga pazia lake hii leo hapa mjini Tehran.

Siku kama ya leo yaani tarehe 17, mwezi wa Mfunguo Sita (Rabiul Awwal), miaka 1490 iliyopita kwa mujibu wa nukuu za maulama wengi wa Kiislamu, alizaliwa Mtume Muhammad SAW katika mji mtakatifu wa Makka. Hata hivyo baadhi ya wapokezi wa Historia wanaitakidi kuwa, Mtume huyo Uislamu alizaliwa tarehe 12 Rabiul Awwal.
Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Imam Khomeini MA alitangaza kipindi cha baina ya tarehe 12 na 17 Mfunguo Sita kuwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu, kwa lengo la kuwaleta pamoja Waislamu pasi na kujali madhehebu yao, ili kwa pamoja wayatafutie ufumbuzi matatizo yanayoukabili ulimwengu wa Kiislamu.

Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatoa mkono wa kheri na fanaka kwa Waislamu na wapenda haki kote duniani kwa mnasaba wa siku hii adhimu, ya kukumbuka kuzaliwa Mtume wa mwisho Muhammad al Mustafa SAW.

3470350

captcha