Miaka mingi iliyopita, Hayati Imam Khomeini MA, Kiongozi mwanzilishi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, ambaye binafsi alikuwa mstari wa mbele kulingania umoja wa Kiislamu alipendekeza kuwa, muda uliopo baina ya tarehe hizo mbili uwe ni "Wiki ya Umoja wa Waislamu" kwa lengo la kuimarisha mashikamano na udugu baina ya madhehebu za Kiislamu. Kwa hivyo wiki hii ni fursa munasibu ya kukutana na kuchunguza udharura wa daima wa kuwepo umoja wa Kiislamu hasa katika kipindi hiki cha fitina na ghasia. Waislamu wa madhehebu mbali mbali wanahitilafiana kuhusu baadhi ya masuala lakini wana nukta nyingi za pamoja kwani wote wana imani sawa kuhusu nukta za kimsingi kama vile Tauhidi au kuabudu Mungu Mmoja, Qur'ani Tukufu, Mtume na qibla. Aidha wana mtazamo sawa kuhusu utekelezwaji wa ibada muhimu kama vile Sala, Saumu, Hija, Zaka n.k. Tunachukua fursa hii kutoa salamu zetu za pongezi, kheri na fanaka kwa mnasaba wa kuanza Wiki ya Umoja ambayo inasadifiana na kuzaliwa Mtumu Mtukufu wa Uislamu. Makala hii fupi inaangazia kuhusu msingi wa umoja katika Qur'ani na Sira ya Mtume wa Uislamu SAW.
Shikamaneni na Kamba ya Mwenyezi Mungu
Tukiangazia Qur'ani Tukufu na Sunna ya Mtume SAW, tutaona kuwa katika
vyanzo hivyo viwili vyenye thamani kubwa zaidi katika Uislamu kumetiliwa
mkazo mkubwa umoja wa Waislamu. Qur'ani Tukufu katika aya kadhaa
imesisitiza kuhusu umoja na kuutaja kuwa ni neema kubwa. Katika Surat
Al-I'mran aya ya 103, Allah SWT anasema: "Na shikamaneni kwa Kamba ya
Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya
Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu: vile mlivyo kuwa nyinyi kwa nyinyi maadui
naye akaziunganisha nyoyo zenu; kwa neema yake mkawa ndugu. Na mlikuwa
ukingoni mwa shimo la Moto, naye akakuokoeni nalo. Namna hivi Mwenyezi
Mungu anakubainishieni Ishara zake ili mpate kuongoka."
Katika aya hiyo Mwenyezi Mungu SWT anazungumzia kuhusu kushikamana na
kamba yake. Katika tafsiri nyingi, misdaki ya wazi kabisa ya kamba hii
imara imetajwa kuwa ni Qur'ani Tukufu. Allama Tabatabai kati ya
mufasirina wakubwa wa Qur'ani ameandika hivi: "Habl (kamba) ya Mwenyezi
Mungu ni Qur'ani iliyoteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu… Kushikamana
hapa kusudio lake ni kushikamana na Aya za Mwenyezi Mungu na kumfuata
Mtume wake, yaani kufungamana na Kitabu (Qu'rani) na Sunna ambapo kwa
kufuata viwili hivyo, kunakuwepo dhamana na kuongoka."
Kushikamana Waislamu na Kitabu cha Allah SWT kwa kudumisha umoja baina
yao kumefananishwa na mtu ambaye anapita katika njia hatari sana ambapo
anakabiliwa na hatari ya kuanguka katika bonde lenye kina kirefu na
hivyo daima anahofia kuanguka, lakini iwapo atashikilia kwa nguvu kamba
zilizo katika pande mbili , ataweza kupita eneo hilo hatari na kufika
alikokusudia. Ni kwa sababu hii ndio katika Qur'ani Tukufu mifarakano
ikatajwa kama ukingoni mwa shimo la Moto. Katika aya tuliyoitaja hapo
juu, Mwenyezi Mungu anawataka Waumini wakumbuke zama chungu za
mifarakano na machafuko. Ukumbusho huo unatolewa ili Waislamu wapate
hima ya kudumisha umoja. Hii ni kwa sababu moja kati ya faida za umoja
katika jamii ni kudumishwa amani, utulivu na usalama na kuwa mbali na
vita na umwagaji wa damu. Kwa msingi kuwa kushukuru na kuilinda neema
hii ya Mwenyezi Mungu ni moja kati ya majukumu muhimu ya Waislamu wote.
Ni wazi kuwa kuibua fitina na mifarakano baina ya Waislamu ni jambo
ambalo linaweza kutajwa kuwa sawa na kukufuru neema kubwa ya Mwenyezi
Mungu.
Waislamu waishi pamoja kama ndugu
Mwenyezi Mungu SWT katika Aya ya 105 ya Surat Al I'mran pia
anatahadharisha Waislamu kwa kusema: Wala msiwe kama wale waliofarikiana
na kukhitalifiana baada ya kuwafikia hoja zilizo wazi. Na hao ndio
watakao kuwa na adhabu kubwa." Qur'ani Tukufu pia inatoa wito kwa
Waislamu wote watambuane kama ndugu. Katika aya ya 10 ya Surat Al
H'ujuraat Mwenyezi Mungu SWT anasema: Hakika Waumini ni ndugu, basi
patanisheni baina ya ndugu zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu ili
mrehemewe." Ayah hii inawataka Waislamu waishi pamoja kama ndugu katika
imani na wawe na mwenendo ambao utadumisha mfungamano na mshikamano wao
ili kwa njia hiyo wawezu kuvutia rehema za Mwenyezi Mungu.
Kwa mtazamo jumla, Qu'rani Tukufu inataka kuwaleta pamoja wanaadamu
wote duniani. Qur'ani inatoa wito wa umoja wa watu wote wa kitabu au
Ahul Kitab na dini za mbinguni. Inawataka wawe chini ya kivuli cha kauli
na itikadi moja na Waislamu na wawe na umoja. Katika Aya ya 60 ya Surat
Al I'mran, Allah SWT anasema: Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Njooni kwenye
neno lilio sawa baina yetu na nyinyi: Ya kwamba tusimuabudu yeyote ila
Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe na chochote; wala tusifanyane sisi
kwa sisi kuwa Waola Walezi badala ya Mwenyezi Mungu. Na wakigeuka basi
semeni: Shuhudieni ya kwamba sisi ni Waislamu.'
Ayah hii inataja Tauhidi kuwa chimbuko la mshikamano wa dini mbali
mbali na inawataka wafuasi wa dini hizo kuja pamoja katika mhimili huo
ili jamii iwe na utulivu. Hakuna shaka kuwa Waislamu ni chimbuko kuu la
mshikamano huu na hivyo wanaweza kuwa na nafasi muhimu katika hilo.
Kulinda nguzo za jamii ni kati ya taathira nzuri za umoja ulioashiria
katika Qur'ani Tukufu. Wakati jamii inapojiepusha na mifarakano na
kushikamana, basi hakutakuwa na pengo la adui kuingia na kuvuruga jamii
kama hiyo. Tab'an umoja na mashikamano wa Waislamu utaweza kupatikana tu
kwa kuwepo kiongozi mmoja wa Ummah. Katika sehemu ya Aya ya 46 ya Surat
al-Anfaal tunasoma kuwa: Na mt'iini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala
msizozane mkaingiwa woga, na zikapotea nguvu zenu.
Mwenyezi Mungu SWT amemtaja Mtume wake kuwa ni mhimili wa umoja wa
kivitendo baina ya Waislamu. Mhimili huu unajumuisha maneno na vitendo
vyote vya Bwana Mtume SAW.
Mtume Muhammad SAW alikuwa mliganiaji wa kwanza wa Umoja
Kwa hakika Mtume Mtukufu wa Uislamu SAW alikuwa mlinganiji wa kwanza wa
umoja wa Kiislamu na ili kufikia lengo hilo alistahamili masaibu na
machungu mengi. Mara kwa mara alikuwa akionya kuhusu hatari
zinazoukabili umma wa Kiislamu. Historia ya Uislamu inashuhudia namna
Bwana Mtume SAW alivyojitahidi kuzuia mifarakano sambamba na kuimarisha
safu za Waislamu. Alitumia faida za umoja kwa maslahi ya Uislamu na
kuimarisha misingi ya kisiasa na kijamii katika umma wa Kiislamu.
Baada ya kuhamia Madina, Mtume Mtukufu wa Uislamu aliyaleta pamoja
makundi mbali mbali kupitia utiwaji saini mikataba. Mikataba hii inaweza
kutajwa kuwa moja kati ya njia za wazi kabisa za kuleta umoja katika
jamii. Mkataba wa kwanza ulikuwa baina ya Mtume na makabila na kaumu
zilizokuwepo Madina. Tadbiri na busara hii ilikuwa njia bora zaidi
iliyokuwepo ya kuleta umoja wa kitaifa na mshikamano wa kidini. Kati ya
ubunifu muhimu zaidi wa Mtume katika uga wa Umoja ni kuleta mshikamano
wa kijamii baina ya Waislamu na kuwaunganisha kama ndugu. Mikataba hiyo
ilijengeka katika kupinga ukabila na ukaumu na mkabala wake kuhimiza
imani ya pamoja na mshikamano wa kijamii. Mtume SAW alileta muafaka na
mkataba wa udugu baina ya Muhajirin au waliohajiri kutoka Makka na
wenyeji wa Madina yaani Ansar.
Kwa kuwepo mshikamano huo wa kidugu baina ya Waislamu, Mtume wa Uislamu
aliondoa uaadui uliokuwa umebaki miongoni mwa Waislamu tokea zama za
Ujahili na kubadilisha hali hiyo kuwa ya kurehemeana na upendo. Mkataba
wa udugu haukuja kwa dinari au thamani za kifedha bali mkataba huo
ulikuwa umejawa na imani ya kimaanawi. Kama ambavyo Qur'ani Tukufu
inavyosema katika Sura Anfal Aya ya 63: 'Na akaziunga nyoyo zao. Na lau
wewe ungeli toa vyote viliomo duniani usingeli weza kuziunga nyoyo zao,
lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliye waunganisha. Hakika Yeye ndiye Mtukufu
Mwenye nguvu na Mwenye hikima.'
Fikra asili ya Mtume SAW ilikuwa ni kuwauganisha Waislamu katika safu
zao na kuondoa kila aina ya shubha ambayo ingeweza kuwasha moto wa chuki
na uhasama uliokuwapo huko nyuma. Kwa msingi huo aliweza kuwaungaisha
na kuleta mahaba miongoni mwa Waislamu kupitia muafaka wa udugu.
Mtume SAW alifanikiwa kusambaratisha vigezo vilivyokuwa vikileta
mifarakano katika zama za ujahilia na mahala pake kuchukuliwa na
mafundisho ya Qur'ani Tukufu. Kwa msingi huu kupambana na taasubu na
kupinga ubaguzi wa rangi na ukabila ni kati ya mbinu muafaka
zilizotumiwa na Mtume SAW katika kuleta umoja wa Waislamu. Mtume SAW
alipinga kujifaharisha kwa rangi ya ngozi na ukabila na alisema: "Iwapo
katika moyo wa mtu kutakuwa na tone la kujifakharisha kikabila, Mwenyezi
Mungu atamhuisha siku ya Kiyama akiwa na Waarabu wa zama za Jahiliya."
Kwa mtazamo wa Mtume SAW kukiuka mipaka na haki za watu wengine na
kuvuruga utulivu ni moja ya sababu kuu ambazo hupelekea kuibuka
mifarakano na utengano. Kwa msingi huo Bwana Mtume SAW aliwataka
Waislamu kuhuisha moyo wa udugu na kupinga dhulma kwa kusema: "Mwislamu
ni Ndugu ya Mwislamu. Hadhulumu, hamlaani wala kumtukana (Mwislamu
mwenzake)."
Mtume Mtukufu wa Uislamu hata katika wasia wake, aliutahadharisha Umma
wa Kiislamu kwa kusema: "Enyi watu, sikilizeni maneno yangu. Sijui,
pengine sitawaona baada ya hapa. Enyi watu mumeharamishiwa kumwaga damu
au kuchukua mali za wenzenu. Mfahamu kuwa kila Mwislamu ni ndugu ya
Mwislamu mwingine na Waislamu ni ndugu baina yao."
Leo ambapo ni fakhari kwa Waislamu wote kufuata Qur'ani na kumfuata
shakhsia mkuu wa Uislamu, Mtume Muhammad SAW, inastahiki kuona Waislamu
wote wakiegemea katika nukta za kidini zinazowaleta pamoja ili kwa mara
nyingine tushushudie ufanisi na mafanikio ya Waislamu kote duniani.