Waandamanaji wametangaza mfungamano wao na wafungwa wa kisiasa akiwemo Sheikh Ali Salman Katibu Mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya Al-Wifaaq.Kadhalika katika maandamano hayo Wabahrain wamesisitizia umuhimu wa
kufanyiwa marekebisho mfumo wa utawala nchini. Wakati huo huo
wanaharakati wametangaza kuachiliwa huru Mahdi al-Musawi, mmoja wa
viongozi wa Harakati ya Kiislamu ya al-Amal, baada ya kupitisha kipindi
cha miaka mitano katika jela za utawala wa Aal-Khalifa. Al-Musawi akiwa
na baadhi ya viongozi wa harakati ya al-Amali, akiwemo pia Muhammad Ali
al-Mahfudh walihukumiwa na mahakama ya nchi hiyo kutumikia kifungo jela.
Hii ni katika hali ambayo wafungwa wa kisiasa nchini Bahrain wamefanya
mgomo wa chakula kulalamikia miamala mibaya ya utawala wa Aal-Khalifa
dhidi yao. Katika fremu hiyo wafungwa wa jela ya al-Howdh al-Jaf
wameanzisha mgomo wa chakula usio na kikomo. Inasemekana kwamba wafungwa
nchini humo, wamekuwa wakiadhibiwa kwa kupigwa na kutukanwa. Kabla ya
hapo pia, idara ya kupigania uhuru na shirika la kutetea haki za
binaadamu zilizo chini ya harakati ya Kiislamu ya Al-Wifaaq zilitangaza
kuwa, jumla ya watu 798 wanaendelea kushikiliwa katika korokoro za
polisi na vituo vya uchunguzi wa makosa ya jinai, ambapo wamekuwa
wakiteswa kwa kupewa adhabu mbalimbali. Mwaka jana viongozi wa Bahrain
walitangaza kuwa, kwa akali watu 1765 walitiwa mbaroni ambapo 120 kati
yao walikuwa ni watoto na 22 wakiwa ni wanawake. Aidha viongozi wa
utawala huo wa Aal-Khalifa waliongeza kuwa, watu wengine 829 walikuwa
wakizuiliwa katika majumba yao. Itafahamika kuwa, Bahrain imekuwa
ikishuhudia maandamano ya amani ya wananchi tokea mwezi Februari mwaka
2011, ambapo utawala wa kidikteta wa nchi hiyo umekuwa ukishirikiana na
askari wa Aal-Saud kuyakandamiza maandamano hayo. Katika mazingira hayo
wanaharakati wa Bahrain kwa kuzingatia kuendelea maandamano hayo ya
wananchi dhidi ya utawala wanasema kuwa, hivi sasa Aal-Khalifa wamefika
kwenye mkwamo. Licha ya utawala wa Aal-Khalifa
na Aal-Saud kutumia askari wa kigeni katika kukandamiza harakati ya
wananchi, lakini bado wameshindwa kumaliza maandamano hayo na badala
yake Wabahrain wamezidi kuwa na irada thabiti ya kuendeleza mwamko wa Kiislamu katika nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi.
3459682