Abdullah Yusuf Ismail mwakilishi wa wa Kenya na ambaye alifika katika fainali ya mashindano hayo amefanya mahojiano maalumu na mwandishi wa IQNA na kusema: "Ni mara ya kwanza nashiriki mashindano ya Qur'ani nchini Iran, na nina furaha kuweza kufika katika fainali ya mashindano haya."
Kuhusiana na jopo la majaji katika mashindano hayo amesema: "Kwa mtazamo wangu, jopo la majaji limefanya jitihada na kutoa maamuzi ya uadilifu."
Hafidh huyo wa Qur'ani kutoka Kenya amesema kuhudhuria kwa wingi wananchi Wairani katika ukumbi wa mashindano ya Qur'ani ni jambo ambalo limempa motisha katika kuweza kufanikiwa kufika fainali.
Abdullah Yusuf Ismail amesema amewahi kushiriki katika mashindano ya Qur'ani nchini Misri ambapo alishika nafasi ya pili katika kategoria ya kuhifadhi Qur'ani kikamilifu. Halikahdlika amesema kiwango cha mashindano ya kimataifa ya Qur'ani Iran ni kizuri sana.
Aidha anasema amewahi kushiriki katika mashindano mengi ya Qur'ani nchini Kenya na kushika nafasi ya kwanza na kwa msingi huo aliteuliwa kuwa mwakilishi wa nchi hiyo katika Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Iran mwaka huu.
Mashindano ya 33 ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yalizinduliwa rasmi Jumatano iliyopita na kumalizika jana Jumanne katika Ukumbi Mkubwa wa Sala wa Imam Khomeini MA mjini Tehran.
Nchi zaidi ya 70 zilituma wawakilishi katika Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ambayo yalikuwa na washiriki 130. Kaulimbiu ya mashindano ya mwaka huu ilikuwa ni "Kitabu Kimoja Umma Moja”.