Ayatullah Ali Khamenei alisema hayo jana jioni hapa mjini Tehran mbele ya wahadhiri wa vyuo vikuu, watafiti na watu wenye vipaji vya kielimu aliowaalika kwenye dhifa ya futari.
Amesema, kuongezwa kasi ya ukuaji wa kielimu katika vyuo vikuu na vituo vya kielimu, kuleta na kutia nguvu utambulisho wa kujivunia wa Kiirani - Kiislamu ndani ya nyoyo za vijana na kuhakikisha vyuo vikuu vinakuwa vya kimapinduzi pamoja na wanavyuo wake, ni katika mambo ya lazima ya kuufanya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kuwa nguvu kubwa ya kielimu duniani na pia kuwa kigezo kizuri cha mfumo wa demokrasia iliyosimama juu ya mafundisho ya Uislamu na umaanawi, ulimwenguni.
Amesema, vyuo vikuu nchini Iran vinapaswa kujipamba kwa sifa hizo na
kulea vijana waumini na wenye itikadhi thabiti kama tunataka kulifanya
taifa hili kuwa na mustakibali unaotakiwa wa Iran yenye nguvu, huru,
iliyoshikamana na dini, tajiri, yenye uadilifu na yenye utawala wa
wananchi, safi, yenye uchungu na dini, yenye watu wema na yenye kupigana
jihadi katika nyuga zote. huku akichora na kubainisha malengo ya miaka 20 ya mfumo wa Jamhuri ya
Kiislamu kwa ajili ya kuifanya Iran kuwa yenye nguvu, yenye heshima,
huru, iliyoshikamana na dini, tajiri, yenye uadilifu na utawala wa
wananchi, safi, inayopigana jihadi, yenye uchungu na dini na ya watu
wanaojiweka mbali na maasi, amesema kuwa, vyuo vikuu ni msingi mkuu wa
kufanikishia malengo hayo na kusisitiza kuwa: Kuongeza kasi ya ustawi na
ukuaji wa kielimu katika vyuo vikuu na vituo vya kielimu nchini, kuleta
na kutia nguvu hisia za kujali utambulisho wa kujivunia wa Kiirani -
Kiislamu kati ya vijana, vyuo vikuu kuwa vya kimapinduzi na wanafunzi wa
vyuo hivyo nao kuwa wanamapinduzi pamoja na kutoa mchango wa kweli
unaotakiwa wa makamanda na maafisa wa vita laini, ni miongoni mwa mambo
ya lazima ya kuufanya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kuwa dola lenye nguvu
kubwa ya kielimu na kigezo cha demokrasia iliyosimama juu ya msingi wa
mafundisho ya Kiislamu na umaanawi duniani.
Kiongozi Muadhamu wa
Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza katika mkutano huo juu ya wajibu wa
kufanyika vikao zaidi kati yake na wahadhiri wa vyuo vikuu kwa lengo la
kuonyesha heshima yake na kuenzi elimu na wahadhiri wa elimu nchini.
Vile vile amegusia mambo mbali mbali yanayomuunganisha na watu wa vyuo
vikuu, watu wenye vipaji vya kielimu na wanachuo na kuongeza kuwa:
Kufanyika vikao vya namna hiyo mbali na uzuri wake wa dhahihiri,
kunaonesha pia taswira jumla ya anga nzuri ya mijadala ya kielimu na
kifikra ya vyuo vikuu.
Baada ya hapo Ayatullah Udhma Khamenei amesema
kuwa, mtazamo kuhusu mustakbali wa nchi ni katika daghadagha na
wasiwasi mkubwa wa weledi wa mambo, watu wenye hekima na watu wenye
vipawa katika kila nchi. Ameongeza kuwa: Suala la kuchora malengo ya
mustakbali lina umuhimu mkubwa kwani uongozi wa nchi katika miaka ijayo
uko mikononi mwa wanafunzi wa vyuo vikuu ambao hivi sasa wako katika
masomo wakifanya juhudi mbali mbali za kujiimarisha kielimu.
Amesema,
suala hilo linaonesha ukubwa wa nafasi na hadhi ya wahadhiri na wakuu
wa vyuo vikuu na kusisitiza kuwa: Kupewa umuhimu silisila ya elimu na
maarifa, kuanzia Wizara ya Elimu na Malezi hadi vyuo vikuu ndilo jukumu
kuu la kuwezesha kufikia mustakbali unaotakiwa na nchi.
Kiongozi
Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameuliza swali kwamba, mustakbali
unaotakiwa na Iran baada ya miaka 20 ni upi? Ameendelea kusema: Kama
mustakbali unaotakiwa kwa ajili ya Iran ni kuwa na nchi yenye nguvu,
yenye heshima, huru, iliyoshikamana na dini, tajiri, yenye uaduilifu,
yenye utawala wa wananchi, safi, inayopigana jihadi, yenye uchungu wa
dini na ya watu wanaojiweka mbali na maasi, basi kuna udharura kwa vyuo
vikuu nchini kujipambana kwa sifa hizo na kulea kizazi cha vijana wenye
itikadi za kidini na waumini wa kweli.
Ayatullah Udhma Khamenei
amesisitiza kuwa: Kama vielelezo hivyo vitapewa kipaumbele katika vyuo
vikuu, basi katika siku za usoni; Iran haitokuwa tegemezi katika upande
wa kiutamaduni na itapata kinga mbele ya matatizo ya kijamii, kikaumu,
kimadhehebu na kisiasa na pia itaepukana na utawala wa kibwanyenye na wa
viongozi wapenda anasa na starehe.
Aidha amesema: Matunda ya
mustakbali wa viongozi mabanyenye na wapenda anasa na starehe ni kuwa na
nchi ambayo itakuwa katika vilele vya utajiri, lakini wakati huo huo
itakuwa na watu maskini kupindukia, wenye shida na matatizo mengi ambapo
mfano wa jamii kama hiyo ni jamii ya Marekani na mfumo wa Wall Street
wa Kimarekani (wa uchumi uliohodhiwa na watu wachache huku idadi kubwa
ya watu wakiwa hawana dhamana ya mustakbali mzuri katika maisha yao).
Kiongozi
Mudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Katika mustakbali wa
nchi yenye viongozi wa aina hiyo, matabaka yote ya watu katika jamii
yatashindwa kuwa na maisha mazuri na ustawi katika maisha yao, na wakati
huo nchi yetu itakuwa na Wall Street ya Kiirani (ya mfumo wa kidhulma
wa kiuchumi).
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa
muhtsari wa matamshi yake hadi kufikia hapo kwa kusema: Ni kwa sababu
hii ndio maana mimi mara zote huwa ninasisitizia mno suala hilo kupewa
umuhimu mkubwa vyuo vikuu, wahadhiri wa vyuo vikuu na wizara ya sayansi
kwani ili kuweza kufikia kwenye mustakbali wa Iran inayotakiwa, kuna
wajibu wa kulea watu wasomi, wenye subira, wanaopigana jihadi katika
njia ya Mwenyezi Mungu, weledi wa mambo na mashujaa, ambapo sehemu kubwa
ya watu wa namna hiyo hulelewa katika vyuo vikuu.
Ayatullah Udhma
Khamenei ameendelea kubainisha mambo ya lazima ya kulea vijana wa namna
hiyo katika vyuo vikuu na kusema: Maendeleo ya kielimu, nidhamu ya
kimaadili, kuwa na subira na uvumilivu wa kidini, kuwa na busuri na
muono wa mbali wa kisiasa na kuleta hisia za kuheshimu utambulisho wa
Kiirani - Kiislamu na kujifakharisha nao katika vyuo vikuu, ni miongoni
mwa mambo ya lazima ya jukumu hilo muhimu.
Amma kuhusiana na
maendeleo ya kielimu, Ayatullah Udhma Khamenei amesisitizia ulazima wa
kuongezwa kasi ya ustawi wa kielimu nchini na kuongeza kwa kusema: Hivi
karibuni nilitoa ukumbusho kuhusu kupungua kasi ya ustawi wa kielimu,
kwani kasi hiyo ni kweli imepungua na hakuna njia nyingine ya kuweza
kufidia kubakishwa nyuma kielimu isipokuwa kuongeza kasi yetu ya ustawi
wa kielimu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia
matamshi ya baadhi ya wanafikra kuhusiana na kupungua kasi ya ustawi wa
kielimu katika nchi za Magharibi na kuongeza kuwa: Kama kasi ya ukuaji
wa kielimu imepungua katika nchi za Magharibi sababu yake ni kuwa, nchi
hizo tayari zimeshatumia sehemu kubwa ya uwezo wao wa kuhimili kasi
hiyo, lakini sisi tuna wajibu wa kuziba pengo la kubakishwa nyuma
kielimu kwa kipindi cha miaka sitini hadi sabini jambo ambalo limefanywa
na tawala za wasaliti na zilizokuwa zimekumbwa na mghafala nchini
(kabla ya ushindi Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran), ili kwa kuziba
pengo hilo tuweze kujiweka kwenye nafasi ya juu na katika vilele vya juu
katika mashindano haya ya kimataifa.
Ayatullah Udhma Khamenei
amegusia pia nafasi ya wahadhiri wa vyuo vikuu katika kuleta na kutia
nguvu utambulisho wa Kiirani na Kiislamu ndani ya wanafunzi wa vyuo
vikuu na kusema kuwa: Wahadhiri wa vyuo vikuu wanapaswa kuwabainisha
wanachuo maendeleo yaliyopigwa na nchi yao katika nyuga za anga za
mbali, teknolojia za Nano na nyuklia pamoja na teknolojia za masuala ya
kibiolojia ya kimatibabu, ili kwa njia hiyo tuweze kuwajengea wanachuo
hao utambulisho wa kujivunia wa Kiirani na Kiislamu.
Vile vile
amesisitiza kuwa, hatua yoyote ile ya kuleta hisia za kujiona duni na
kuwavunja moyo wanachuo ni usaliti na kuongeza kwamba: Wanafunzi wa vyuo
vikuu wanapaswa wakati wote kujivunia na kuona fakhari kuwa kwao
Wairani, Waislamu na wanamapinduzi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya
Kiislamu amesisitiza pia kwamba: Ijapokuwa sisi tumebakishwa nyuma
kihistoria katika maendeleo ya kielimu, lakini kwa jitihada na jitihada
kubwa za vijana wetu wenye vipawa vya kila aina nchini, tunaweza kufidia
na kuziba pengo hilo bila ya wasiwasi wowote ule.
Ayatullah Udhma
Khamenei ameashiria pia ripoti za baadhi ya taasisi za nyaraka na
takwimu pamoja na majarida yenye itibari duniani yaliyothibitisha
kupigwa hatua kubwa za maendeleo ya kielimu nchini Iran na kuongeza
kuwa: Katika ripoti hizo, taasisi na majarida hayo maarufu na yenye
itibari duniani yanapozungumzia maendeleo mbali mbali ya kielimu ya Iran
huwa yanatumia maneno kama "maendeleo ya kustaajabisha ya Iran," "Iran
dola linalochipua lenye nguvu za kielimu," "Iran katika juhudi za
kubadilisha uchumi unaotegemea maliasili kuwa uchumi unaotegemea
uzalishaji wa elimu" na "maendeleo ya Iran katika seli shina, sayansi ya
teknolojia, anga za mbali, kubadilisha nishati na teknolojia ya
mawasiliano." Amesema, inabidi uhakika huo ufikishwe vizuri kwa kizazi
cha vijana nchini ili sambamba na kupata hisia za kupenda utambulisho
wao, waweze kujivunia na kuona fakhari kuwa kwao Wairani.
Amesema,
ubunifu mpya uliokuja nao mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran duniani
katika nyuga za demokrasia ni kitu kingine muhimu cha kujivunia na
kusisitiza kwamba: Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndio utawala
pekee duniani ambao umekuja na demokrasia iliyosimama kwenye msingi wa
Uislamu na umaanawi.
Kiongozi Mudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu
ameongeza kuwa: Demokrasia ya nchi za Magharibi kwa hakika ni utawala wa
vyama, na vyama katika nchi za Magharibi badala ya kuwa kanali
iliyojitanua na yenye uungaji mkono wa wananchi, kimsingi ni klabu za
kisiasa ambazo zimezoundwa na baadhi ya wanasiasa na mabepari, bila ya
kujali nafasi ya wananchi na maamuzi yao.
Ayatullah Udhma Khamenei
amekumbusha pia kuwa: Kama uhakika huo wa kujivunia utafikishwa vizuri
kwa mwanafunzi wa chuo kikuu, mwanafunzi huyo hatoweza kujiona duni wala
kukata tamaa, na hata kama atakwenda nje ya nchi kwa ajili ya kuendelea
na masomo, bila ya shaka yoyote atarejea nchini kwake kwani atakuwa
tayari amejengeka vizuri kwa hisia za kujali utambulisho wake na
kujifakharisha nao.
Aidha amesema kuhusiana na kupewa kipaumbele
utambulisho wa Kiislamu katika vyuo vikuu nchini kuwa: Viongozi wa vyuo
vikuu wana wajibu wa kusimama imara kukabiliana na pia kuzuia hatua au
jambo lolote lile lisilokubaliwa na Uislamu kama vile kupigwa kambi
tofauti za wanachuo ambazo zinatia doa utambulisho wa Kiislamu.
Kuwa
na busuri na muono wa mbali wa kisiasa na kupewa nafasi kazi za kisiasa
katika vyuo vikuu ni jambo jingine la lazima la kuweza kuwa na Iran
yenye mustakbali unaotakiwa jambo ambalo limezungumziwa na Kiongozi
Muadhamu katika matamshi yake hayo na kuongeza kwa kusema: Mimi nimekuwa
nikisisitizia mara zote umuhimu wa kujadiliwa masuala ya siasa ndani ya
vyuo vikuu na hata katika miaka ya huko nyuma niliwahi kusema kuwa,
Mungu awalaani watu ambao walipiga marufuku upanuzi wa fikra na
kufanyika kazi za kisiasa kwenye vyuo vikuu.
Ayatullah Udhma Khamenei
ameongeza kwamba: Wakuu wa wakati huo walikasirishwa sana na maneno
yangu hayo, lakini itikadi ya viongozi hao ilikuwa ni kupigwa marufuku
na kuzuiwa masuala ya siasa ndani ya vyuo vikuu ingawa leo hii watu hao
hao wanajitoa kimasomaso na kutoa matamshi tofauti na itikadi zao za
huko nyuma kuhusiana na vyuo vikuu.
Vile vile amesisitiza kuwa, anga
ya vyuo vikuu ni anga ya kuchuanisha mitazamo, mijadala na kutoa
changamoto za kila namna na kuongeza kuwa: Kuweko anga hiyo katika
kipindi ambacho damu za wanachuo vijana zinachemka mwili, hakuna tatizo
lolote, tatizo linakuja pale anga hiyo inapotumika kwa ajili ya kupiga
vita Mapinduzi ya Kiislamu na kutumiwa vibaya kukabiliana na matukufu ya
Mapinduzi ya Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu
ameongeza kuwa: Hakuna tatizo kuweko mitazamo na mirengo tofauti ya
kisiasa katika vyuo vikuu, lakini maafisa na viongozi wa vyuo hivyo -
iwe ni viongozi wa ngazi za juu au wizara au marais au wahadhiri - kila
mmoja ana jukumu la kuielekeza anga hiyo ya michuanisho ya hoja katika
vyuo vikuu, upande wa kutia nguvu misingi na malengo ya Mapinduzi ya
Kiislamu na kamwe wasiruhusu kuweko mitazamo ya kupinga Mapinduzi ya
Kiislamu katika vyuo vikuu.
Ayatullah Udhma Khamenei aidha amesisitiza kuwa: Vyuo vikuu na wanachuo, wanapaswa kuwa wanapinduzi daima.
Vile
vile ameashiria baadhi ya ripoti zinazoonesha kuweko fikra za kuunga
mkono mirengo inayopinga mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu katika baadhi ya
vyuo vikuu na kuongeza kuwa: Wakuu wa Wizara ya Sayansi na Elimu ya Juu
wanapaswa kuwa macho sana, na wasiruhusu vyuo vikuu kugeuzwa kuwa maeneo
ya kupotosha na kupiga vita uhakika na matukufu ya Mapinduzi ya
Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia
kuwa: Kuweko anga ya kimapinduzi na ya kushikamana na dini na kupewa
nafasi kubwa Imam (Khomeini - Rahimahullah) kwenye vyuo hivyo, ni katika
mambo ya lazima ya wazi kabisa kwa vyuo vikuu.
Ayatullah Udhma
Khamenei ameendelea na hotuba yake kwa kusema: Tab'an si sahihi pia
kuleta anga ya kulazimisha na kutenza nguvu katika vyuo vikuu, lakini
anga ya vyuo hivyo inapaswa kuwa ya kimapinduzi na kidini, na hilo
linapaswa kufanikishwa kwa hekima, kwa utulivu na kwa busra ya hali ya
juu.
Kiongozi Mudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea na hotuba
yake kwa kutoa nasaha kadhaa kwa maafisa na wakuu wa Wizara ya Sayansi
na Elimu ya Juu pamoja na wakuu wa vyuo vikuu nchini.
Kulindwa na
kuhifadhiwa moyo wa matumaini na nishati na uchangamfu katika maeneo ya
kielimu na kiutafiti, kuzipa kipaumbele na umuhimu elimu za kimsingi,
kuelekeza makala za kielimu upande wa mahitaji ya nchi, ulazima wa
kubainishwa na kutolewa ufafanuzi ramani kuu ya kielimu nchini kwa ajili
ya watu wa vyuo vikuu na kuifanya ramani hiyo kuwa ajenda yao na
kutiliwa mkazo umuhimu wa kuweko masomo ya Sayansi ya Jamii yaliyosimama
kwenye msingi wa dini tukufu ya Kiislamu, ni katika nasaha zilizotolewa
na Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei kwenye hotuba yake hiyo.
Kupewa
umuhimu udiplomasia ya kielimu ni nasaha nyingine zilizotolewa na
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika hotuba yake hiyo
ambaye wakati huo huo amesisitiza kwa kusema: Udiplomasia na uhusiano wa
kielimu ni jambo muhimu, nami ninaliunga mkono jambo hilo, lakini
inabidi tuwe macho tusije tukatekwa na hila za maadui na kugeuzwa
uhusiano huo wa kielimu kuwa bwawa la kujipenyeza na kutia doa maadui
katika masuala yetu ya usalama kwani adui anatumia kila njia ikiwa ni
pamoja na uhusiano na mawasiliano ya kielimu kwa ajili ya kujipenyeza
nchini na kwamba jambo hilo limewahi kutokea huko nyuma na madhara yake
yanaonekana leo hii katika baadhi ya mambo.
Katika sehemu nyingine ya
hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei amezungumzia uchumi wa kimuqawama
na kusema kuwa uchumi huo utaandaa uwanja wa kupatikana heshima ya
kitaifa na kutatua matatizo yote yaliyopo hivi sasa nchini. Ameongeza
kuwa: Kuna baadhi ya watu wanasema, vipi utaweza kutatua matatizo na
shida za hivi sasa katika jamii kupitia kusisitizia mara kwa mara suala
la kulindwa heshima ya taifa? Majibu ya watu wanaotoa maneno hayo ni
kwamba: Utatuzi pekee wa jambo hilo ni kutekelezwa vilivyo na kwa njia
sahihi siasa za uchumi wa kimuqawama.
Nasaha nyingine zilizotolewa na
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni umuhimu na kuyafanya kuwa
jambo la kimsingi masuala ya kiutamaduni kwenye vyuo vikuu.
Ameongeza
kwa kusema: Tab'an masuala ya kiutamaduni hayana maana ya kufanya mambo
madogo madogo ya pembeni au kupeleka wanafunzi kwenye kumbi za muziki
na tamthilia, bali viongozi wa vyuo vikuu wanapaswa kuwafunguliwa uwanja
wanachuo na wahadhiri wa vyuo hivyo wanaojali mambo ya thamani na ya
maana, ili waweze kufanya kazi zao vizuri kwa ajili ya kuzijaza akili na
nyoyo za wanafunzi wa vyuo vikuu, utamaduni wa Kiislamu na wa
kimapinduzi.
Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amewalenga moja kwa
moja katika maneno yake wahadhiri wanamapinduzi ambao ni makamanda
katika vita laini pamoja na wanachuo wanamapinduzi ambao ni maafisa
katika vita hivyo laini akiwasisitizia kwa kuwaambia: Jukumu lenu ni
kutoa mchango wa kweli na unaotakiwa katika shauri hili kwani ugumu na
ukali wa vita laini vinavyoendeshwa na adui hivi sasa ni mkubwa zaidi
kwa mara kadhaa ikilinganishwa na miaka ya huko nyuma.
Kutoruhusu
kujiingiza na kutumiwa watu wasioaminika katika vyuo vikuu, ni nasaha
nyingine zilizotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu
ambaye amesisitiza kuwa: Mtu yeyote ambaye atatumia kisingizio chochote
kile kama vile uchaguzi na mfano wake ili kuutia kwenye matatizo mfumo
wa Jamhuri ya Kiislamu, mtu huyo haaminiki, na hana sifa za kuweko
katika vyuo vikuu, na hilo si jambo jipya kwani hakuna nchi yoyote
duniani inayoruhusu mfumo wake wa utawala utiwe katika matatizo.
Mwanzoni
mwa mkutano huo, baadhi ya wahadhiri, wanafikra na wataalamu wa fani za
sayansi ya uhandisi, sayansi ya tiba na sayansi ya jamii wametoa hotuba
fupi fupi na kubainisha mitazamo yao kuhusiana na masuala tofauti.