IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Magaidi wa ISIS waliibuliwa kuiangamiza Iran lakini kwa nguvu zake imewalemaza

8:04 - June 26, 2016
Habari ID: 3470415
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Jumamosi amesema magaidi wa ISIS waliibuliwa kuiangamiza Iran lakini kwa nguvu zake, Iran imeweza kuwalemaza.

Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo Jumamosi mjini Tehran aliponana na majimui ya familia za mashahidi zikiwemo familia za mashahidi wa tarehe Saba Tir (Juni 28) na familia za mashahidi wanaolinda Haram. Sambamba na kuwaenzi mashahidi kutokana na imani, jihadi, uongofu na maarifa yao aali na matukufu pamoja na subira na kutotetereka familia za mashahidi hao amesema kuwa, mashahidi na familia zao ni misingi na nguzo za nguvu na uwezo na uimara wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Amesisitiza kuwa: Njia pekee ya kuweza Iran ya Kiislamu kupiga hatua za kimaendeleo katika kila uwanja ni kuhuishwa roho ya kimapinduzi ya wanajihadi wake.
Mwanzoni mwa hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei ametoa mkono wa pole kwa kukumbuka siku za kuuawa shahidi Amirul Muminin Imam Ali (Alayhis Salaam) na kusema kuwa, mtukufu huyo ni shahidi mkubwa zaidi katika historia ya mwanadamu, ni shahidi wa mihrabu na ni shahidi wa njia ya haki, ya istikama na ya kutotetereka. Baada ya hapo ameashiria namna ilivyopita miaka 35 tangu ulipotokea mripuko wa bomu katika ofisi ya chama cha Jamhuri ya Kiislamu hapo tarehe Saba Tir 1360 (Juni 28, 1981) na kusema kuwa, waliofanya shambulio huo ni genge khabithi la kigaidi ambalo halikuwa na chembe ya huruma na kwamba wanachama wa genge hilo la kiafiriti baada ya kutoroka nchini Iran, kwa miaka mingi wanaishi chini ya himaya ya nchi za Ulaya na Marekani zinazojigamba kuwa ni viranja wa kupambana na ugaidi na watetezi wakuu wa haki za binadamu duniani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, suala hilo ni kashfa kubwa ya kihistoria kwa nchi za Ulaya na Marekani na kuongeza kwamba: Wanachama wa genge hilo la kigaidi ni watu ambao walianzisha mashambulizi yao makali kwa madai ya kuwahami wananchi bali hata kuulinda Uislamu lakini kadiri siku zilivyopita ndivyo walivyofanya jinai kubwa kama vile mashambulizi ya tarehe Saba Tir (Juni 28) na kuwaua kigaidi wananchi wa kawaida na hatimaye kushirikiana na watu kama Saddam (kufanya mashambulizi dhidi ya wananchi wa Iran na hata wa Iraq) na hivi sasa wanaungwa mkono kikamilifu na Marekani.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja shambulio la bomu la Juni 28, 1981 nchini Iran kuwa ni tukio kubwa lenye masomo na ibra za kila namna na huku akielezea masikitiko yake kutokana na kutofanyika juhudi za kutosha za kuyatangaza na kuwaelimisha vijana matukio muhimu ya Mapinduzi ya Kiislamu na masuala yanayohusiana na mashahidi, amesema kuwa: Licha ya kupita miaka 38 tangu lilipotokea tukio hilo, lakini hadi leo hii hakuna hata filamu moja au tamthilia moja au riwaya angalau moja ya kuzungumzia tukio la Tir Saba na shahidi Beheshti na mashahidi wengine wa tukio hilo, na kama tunaona kuwa tukio hilo limebakia hai hadi hivi sasa, jambo hilo halitokani na kitu kingine ila moyo wa kimapinduzi wa wananchi wenyewe wa Iran.
Vile vile amegusia namna kulivyoandikwa vitabu mbali mbali kuhusiana na operesheni za mashahidi wa kipindi cha vita vya kujihami kutakatifu (vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa wakati huo wa Iraq dhidi ya mfumo mchanga wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran) na kuwataka wananchi wote hususan vijana nchini Iran kutalii na kuvisoma kwa kina vitabu hivyo. Amesema: Ijapokuwa kuna vitabu vingi vimeandikwa na kuhaririwa katika uwanja huo, lakini bado wigo wa kuandika vitabu vingine vingi zaidi ni mpana sana kwa ajili ya kuelezea vipengee na kona mbali mbali za vita vya kujihami kutakatifu na mashahidi watukufu wa vita hivyo, kwani mienendo, matamshi na namna ya harakati za kila shahidi ni mlango mpana wa kuingia kwenye dunia pana ya maarifa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, moja ya sifa za kipekee za kipindi cha vita vya kujihami kutakatifu ni kushiriki vikosi vya kujitolea vya wananchi vikiwa na msukumo wenye nguvu kutoka katika matabaka na daraja mbali mbali za wananchi na kufanikiwa wananchi hao kuvitoa vita hivyo katika kuhodhiwa na vikosi rasmi tu vya kijeshi. Amesisitiza kuwa: Nasaha zetu leo hii pia kwa viongozi wa serikali ni kwamba wana wajibu wa kuwashirikisha vizuri wananchi katika nyuga mbali mbali zilizopo nchini hususan uwanja wa kiuchumi.
Ayatullah Udhma Khamenei ameendelea na hotuba yake kwa kuzungumzia mashahidi wa kulinda heshima ya Ahlul Bait (Alayhimus Salaam) pamoja na mashahidi wa Haram na kusema: Suala hilo ni katika maajabu ya kihistoria kwamba vijana wa Iran na nchi nyingine na vijana wa nchi nyingine kutokana na imani yao thabiti na msukumuo wao wa hali ya juu, wanasamehe maisha yao mazuri, wake zao vijana na watoto wao wadogo na kwenda kwenye nchi nyingine ajnabi kwa ajili ya kupigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu na hatimaye kufa shahidi katika njia hiyo tukufu.
Amesema, imani imara na thabiti ya mashahidi wa kulinda Haram na subira na uvumilivu wa familia zao ni vipengee vingine vya maajabu hayo ya kihistoria na kusisitiza kuwa: Upeo mwingine wa suala hilo, ni vile vitu vinavyoufanya imara mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambao umesimama thabiti juu ya msingi wa imani, azma na nia ya kweli pamoja na irada ya watu waumini, wanajihadi na mashahidi wenye imani thabiti.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, maadui wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu hawana uwezo kabisa wa kuelewa na kufahamu misingi ya uimara na nguvu za mfumo huu wa Kiislamu na kusema kuwa: Mashahidi na familia zao ni nguzo madhubuti kama jiwe ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na ni kwa sababu hiyo ndio maana mfumo huu umekuwa ukifanikiwa kukabiliana na kuzishinda changamoto za kila namna unazokabiliana nazo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Kila wakati tulipoegemea kwenye Mainduzi ya Kiislamu na moyo wa kimapinduzi, tumeweza kufanikiwa, na kila wakati tulipojaribu kuwafurahisha mabeberu, tumeporomoka kwenye matukufu yetu na kila wakati tulipoona muhali kutangaza misimamo yetu ya kimapinduzi kwa uwazi, tumekuwa tukikwama na kupata hasara katika mambo yetu.
Amesisitiza kuwa, inabidi tukabiliane na mabeberu na waistikbari kwa roho ya kimapinduzi na kuongeza kwamba: Kuwa na imani na Mwenyezi Mungu, kuwa na imani na kushikamana na jihadi na kuwepo msukumo mkubwa wa vijana waumini na wanapinduzi ni katika vyanzo vya nguvu na uimara wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika vita vyake visivyo na mlingano sawa vya kupambana na kambi ya kiistikbari, na kwamba, licha ya mabeberu hao kuviona vyanzo hivyo vya nguvu za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, lakini hawana uwezo wa kuvichanganua vizuri, hivyo wanaishia kwenye kutumia mbinu za mabavu na za ukatili.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, njama za mabeberu za kuunda magenge ya kigaidi na kitakfiri kama vile Daesh ni mfano wa mbinu hizo za kikatili na za mabavu zinazotumiwa na mabeberu katika kukabiliana na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Amesema: lengo kuu la kuanzishwa magenge hayo ya kigaidi na kitakfiri na vitendo vyao huko Iraq na Syria lilikuwa ni kuivamia na kuishambulia Iran, lakini nguvu za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu zimepelekea mabeberu hao wakwame huko huko katika nchi za Iraq na Syria.
Amesema kuwa, magenge ya kigaidi na kitakfiri hayatofautishi baina ya Waislamu wa Kishia na Kisuni na kwamba kila Muislamu anayeunga mkono Mapinduzi ya Kiislamu na ambaye ni adui wa Marekani huwa analengwa na magenge hayo ya kigaidi na kitakfiri. Vile vile amegusia masuala ya Bahrain na kusema: Huko Bahrain pia tatizo la nchi hiyo si suala la Ushia na Usuni bali tatizo lake hasa ni utawala wa madiktekta walio wachache, mabeberu na wanaojivutia kila kitu upande wao ambao wanawakandamiza wananchi walio wengi wa nchi hiyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kitendo cha watawala wa Bahrain cha kumvunjia heshima na kuchukua hatua dhidi ya alimu na mwanachuo mwanajihadi Sheikh Isa Qasim ni ishara ya upumbavu wa viongozi hao na kusisitiza kuwa: Sheikh Isa Qasim ni mtu ambaye alikuwa akijitihadi kadiri ya uwezo wake kuzungumza na wananchi wa Bahrain na kuwazuia kutumia misimamo mikali na silaha dhidi ya watawala wa nchi hiyo, lakini watawala wa Bahrain hawajui kwamba kumvunjia heshima alimu humo mwanajihadi kuna maana ya kuondoa kizuizi kilichokuwa kinawadhibiti vijana wenye hamasa na wenye shauku kubwa wa Bahrain ambao wako tayari kuchukua hatua yoyote ile kukabiliana na utawala wa nchi hiyo.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza kuwa, madola ya kibeberu na vibaraka wao mara zote wanashindwa kuwaelewa wananchi na imani ya jamii za watu hao na mara zote wanafanya makosa katika mahesabu yao. Ameongeza kuwa: Njia sahihi ya harakati ni kufanya harakati hizo katika njia ya Uislamu na kutawakali kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na kwamba ni taifa lenye imani na la watu wanajihadi na wenye nia na azma ya kweli isiyotetereka ndilo linaloweza kuvishinda vizuizi vyote na kusonga mbele katika mambo yake.
Ameendelea na hotuba yake kwa kuzungumzia umuhimu wa kustafidi vizuri na kadiri inavyowezekana na mikesha ya Laylatul Qadr katika siku hizi za mwishoni mwa mwezi huu mtukufu wa Ramadhani na kusema kuwa: Katika mikesha hiyo na nyakati zake za usiku wa manane ambazo ni nyakati bora kabisa za tawassul na kunyenyekea kwa Mwenyezi Mungu, inabidi kuomba msaada wa roho tukufu zikiwemo roho za mashahidi na kuomba kutushufaia mbele ya Mwenyezi Mungu na kuzihudhurisha vilivyo nyoyo zetu katika ibada ya Mwenyezi Mungu Mmoja Asiye na mshirika na tuombe dua kwa namna ambayo Mola wetu Mtukufu atatutakabalia.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam Walmuslimin Shahidi Mahallati, mwakilishi wa Fakihi Mtawala (Waliyyul Faqih) ambaye pia ni mkuu wa Taasisi ya Mashahidi na Masuala ya Watu Wanaojitolea katika Njia ya Haki, ameashiria wajibu wa kukielewesha kizazi cha vijana hamasa na kujitolea wanamapambano wa Kiislamu katika nyakati tofauti na kusema kuwa: Kuasisiwa na kuanza kufanya kazi sekretarieti ya Baraza Kuu la Kueneza na Kustawisha Utamaduni wa Kujitolea na Kuwa Tayari Kufa Shahidi katika Njia ya Haki, kuanzisha kambi maalumu ya mitandao ya Intaneti, kuimarisha na kustawisha vyama na taasisi za watu wanaojitolea katika njia ya haki, kuanza kutekelezwa mpango wa kuwaenzi watu wanaojitolea katika njia ya haki pamoja na kuanzishwa kamati maalumu ya uchumi wa kimuqawama kwa shabaha ya kuongeza na kuimarisha nguvu na uwezo wa kujitolea katika njia ya haki kwenye jamii, ni miongoni mwa hatua na kazi kuu za taasisi hiyo ya mashahidi.


3510359
captcha