IQNA

Vijana Waislamu wasomaji wa Qur'ani Afrika Mashariki Wapinga mauaji ya kimbari

15:42 - July 17, 2016
Habari ID: 3470458
Vijana wasomaji wa Qur'ani kutoka nchi kadhaa za Afrika Mashariki wamekutana Kigali Rwanda na kubainisha wazi kuwa wanapinga idiolojia ya mauaji ya kimbari.

Kwa mujibu wa gazeti la New Times, vijana hao Waislamu wamesisitiza kuwa Uislamu ni dini ya amani na hivyo wametoa wito wa kuwepo umoja na amani ili dunia izuie mauaji ya kimbari kurudiwa tena.

Vijana hao waliyasema hayo mjini Kigali Jumamosi walipotembelea eneo la kumbukumbu ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda dhidi ya Watutsi.

Zaidi ya vijana 60 kutoka nchi tiasa wako nchini Rwanda kushiriki katika mashindano ya siku tatu ya kusoma Qur'ani.

Washiriki katika mashindano hayo ni kutoka Kenya, Burundi, Uganda, Tanzania, Zanzibar, Ethiopia, Misri, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na mwenyeji Rwanda.

Wakiwa katika eneo la kumbukumbu ya mauaji ya kimbari, walielimishwa kuhusu historia ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 Rwanda ambapo Watutsi karibu milioni moja waliuawa kwa siku 100.

"Safari hii leo imetusaidia kupata maelezo ya moja kwa moja kuhusu namna mauaji hayo yalivyotekelezwa. Hiki kilikuwa ni kitendo kilicho dhidi ya binadamu na sisi kama vijana Waislamu tunapaswa kujiepusha na ushawishi wa kutenda kitendo kama hiki na tujitahidi kuzuia kujiri mauaji kama hayo popote pale duniani. Idiolojia ya mauaji ya kimbari inapaswa kupingwa kwa nguvu zote," amesema Ahmad Sedky kutoka Misri."

Hamza Muhyidin Rage kutoka Kenya amesema, "Kumbukumbu hii inashtua na naamini kuna mengi ya kujifunza kutoka historia mbaya ya Rwanda. Vijana ndio wenye jukumu la kuifanya dunia iwe mahala bora pa kuishia na hili linaweza kufanyika kupitia kupinga itikadi ya mauaji ya kimbari na kustawisah umoja na Amani katika nchi zetu na kote duniani."

"Tunashukuru kupata fursa ya kutembelea sehemu hii. Kilichojiri Rwanda ni dhidi ya mafundisho ya Kiislamu," amesema Ali Saleh wa Zanzibar.

Kwa upande wake Sheikh Ismail Maniriho wa Mkuu wa Kuutangaza Uislamu aktika Jumuiya ya Waislamu Rwanda amesema kuna haja ya kuwaelimisha vijana kuhusu mauaji ya kimbari ili kuzuia ukatili huo kujiri kwingineko duniani.

3515632

captcha