IQNA

Myanmar yazidi kuwabagua, kuwakandamiza Waislamu

14:10 - January 04, 2017
Habari ID: 3470780
IQNA-Mabuddha wenye misimamo mikali na maafisa wa serikali ya Myanmar wamebuni mbinu mpya ya kuwabagua na kuwakandamiza Waislamu katika makazi na nyumba zao.
Ripoti zinasema meya wa eneo la Samuna lililoko kaskazini mwa mji wa Maungdaw katika jimbo la Rokhine amewaambia Waislamu wa jamii ya Rohingya kwamba wanapaswa kulipa kodi kwa ajili ya kuendelea kuishi katika eneo hilo. Meya huyo ametishia kwamba, iwapo Waislamu hao watang'ang'ania kuishi katika eneo hilo atatuma jeshi na askari usalama kwa ajili ya kuwabaka na kuwatesa.

Mbinu mpya za kuwafukuza Waislamu

Kwa sasa na baada ya kuongezeka mashinikizo ya kieneo na kimataifa dhidi ya ukandamizaji na mauaji ya Waislamu nchini Myanmar, viongozi wa nchi hiyo wamebuni mbinu mpya ya kuwafukuza Waislamu nchini humo kupitia njia ya kuwalazimisha kulipa kodi. Si hayo tu bali vingozi wa utawala wa Myanmar wameanza hata kuwaainishia Waislamu idadi ya watoto wanaopaswa kuzaa. 

Kuhusu mbinu hizo mpya dhidi ya Waislamu nchini Myanmar mchambuzi Hana Salim anasema: Ni jambo lisilowezekana kwa watu wa kabila la Rohingya ambao kimsingi ni wakulima maskini, kuweza kulipa kodi na ushuru wanaolazimishwa kutoa kama fidia ya kuendelea kuishi katika eneo la Maungdaw. Anasema lengo la sheria na hatua kama hizo ni kubadili muundo wa kijamii wa Waislamu katika jimbo la Rokhine na mpango huo umeanza kutekelezwa katika mji wa Maungdaw.  


Tangu mwaka 2012 Mabudha wenye misimamo mikali wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali za ukatili, mauaji na kubaka wanawake wa Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar kwa shabaha ya kuwalazimisha kuondoka katika nyumba na makazi yao hususan katika jimbo la Rokhine. Mabudha hao wanapora na kutwaa mashamba, milki na mali za Waislamu hao.

Mauaji ya Kimbari ya Waislamu

Mchambuzi wa siasa na mwandishi habari wa Myanmar, Sorub Kumar Shahi anasema: Mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu yanaendelea kufanyika nchini Myanmar huku nchi za Magharibi na za Kiarabu zikiendelea kunyamazia kimya jinai hiyo. Mchambuzi huo wa masuala ya kisiasa anaendelea kusema kuwa: Lau kungefanyika jinai ndogo zaidi ya mauaji yanayofanyika dhidi ya Waislamu nchini Myanmar katika maeneo mengine ya dunia basi dunia nzima ingesimama na kupaza sauti kubwa.  

Wakati huo huo meya wa mji wa Maungdaw amesema kumeanza ujenzi wa vijiji saba vya Mabudha katika eneo hilo la makazi ya Waislamu. Vilevile ripoti zinasema kuwa, jeshi la Myanmar na makundi ya Mabudha wenye misimamo mikali kama kundi linalojiita 969 la kiongozi mmoja wa kidini wa Mabudha wameshambulia kwa silaha makazi ya Waislamu wa Rohingya katika kijiji cha Nashaforo karibu na mji wa Maungdaw na kupora mali na milki zao. Mashambulizi makali ya mabudha dhidi ya Waislamu wa Rohingya katika mji huo yalianza sambamba na yale yanayofanywa na wanamgambo wa kundi la klabu moja iliyopo katika mpaka wa Myanmar na Bangladesh na hadi sasa makundi hayo yanaendelea kuvamia nyumba za Waislamu na kupora milki na mali zao.

Mabudhha waongoza kampeni dhidi ya Waislamu

Katika miaka ya hivi karibuni viongozi wa Mabudha wenye misimamo mikali kama Ashin Wirathu wamekuwa wakifanya kampeni kubwa dhidi ya Waislamu nchini Myanmar na wanawachochea wafuasi wao kufanya mashambulizi na hata kuwabaka wanawake wa Kiislamu. Katika mkondo huo mtawa huyo wa kibudha ameunda kundi linalojiita 969 linaloua Waislamu wa Rohingya na kupora mali zao. 

Kwa kutilia maanani hayo yote watetezi wa haki za binadamu wanasisitiza kuwa, kuna ulazima wa kuchukuliwa hatua za kivitendo za kukabiliana na kuzuia ukatili unaoendelea kufanwya na mabudha wenye misimamo mikali wakisaidiwa na jehi la Myanmar dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohinywa na kusitisha haraka mauaji ya kimbari katika nchi hiyo.  

3559656

http://www.iqna.ir/fa/news/3559656 



  • captcha