IQNA

Magaidi wa ISIS waua watu 47 makanisani Misri, Al Azhar yalaani hujuma

19:40 - April 09, 2017
Habari ID: 3470926
TEHRAN (IQNA) Kundi la kigaidi la ISIS limetekeleza hujuma za mabomu dhidi ya makanisa mawili ya Kikhufti (Coptic) katika miji ya Tanta na Alexandria Misri na kuua Wakristo wasiopungua 47.

Magaidi wakufurishaji wa ISIS au Daesh wametoa taarifa kupitia mtandao wao wa habari wa Amaq na kudai kuhusika na hujuma hizo ambazo pia zimewajeruhiwa watu zaidi ya 100.

Hujuma ya kwanza leo Jumapili ilipelekea watu 29 kuuawa na wengine zaidi ya 70 kujeruhiwa katika wa bomu dhidi ya Kanisa la Kikhufti katika mji waTanta, eneo laNile Delta. Kanisa lililolengwa linajulikana kama Mar Girgis au Mtakatifu George na lilikuwa limejaa waumini wa Kikristo waliokuwa wakiadhimisha siku ijulikanayo kama Jumapili ya Matawi.

Masaa kadhaa baada ya hujuma hiyo ya Tanta bomu jingine liliripuka nje ya kanisa la Mtakatifu Mark mjini Alexandria ambapo watu 18 wameuawa na wengine karibu 30 kujeruhiwa. Imearifiwa kuwa kiongozi wa Kanisa la Kikhufti Misri alikuwa ndani ya kanisa hilo lakini hakujeruhiwa.

Wakati huo huo Kituo cha Kiislamu cha Al Azhar nchini Misri kimetoa taarifa na kulaani vikali hujuma hizo mbili za kigaidi dhidi ya makanisa nchini humo. Taarifa hiyo imesema lengo la hujuma hizo ni kuvuruga usalama, uthabiti na umoja wa taifa la Misri na kwa msingi huo Wamisri wanapaswa kulinda umoja wao na kukabiliana na jinai hiyo. Al Azhar imetangaza kufungamana na kanisa la Misri katika kukabiliana na ugaidi. Aidha wakuu wa Al Azhar wamewaombea rehema za Mwenyezi Mungu waliopoteza maisha katika hujuma hizo.

Inafaa kukumbusha hapa kuwa, magaidi wa ISIS sawa na wenzao wa Al Qaeda, Boko Haram na Al Shabab wanafuata itikadi yenye misimamo mikali ya Uwahhabi  ambao ni itikadi inayotawala Saudia. Hii ni itakadi ambayo inapigiwa debe na watu wanaopata himaya ya Saudia ambao wanawavutia magaidi kote duniani. Magaidi wa ISIS wanatumia itikadi ya Uwahhabi kuwatuhumu Waislamu wengine kuwa ni makafiri na pia kuwalenga wasiokuwa Waislamu na hivyo kuwaua kiholela.

3588254
captcha