IQNA

Mwanamke Mwislamu kuwania Useneta Marekani

12:05 - August 01, 2017
Habari ID: 3471096
TEHRAN (IQNA)- Bi. Deedra Abboud, ni mwanamke Mwislamu ambaye anawania kiti katika Bunge la Senate nchini Marekani huku akilalamika kuwa anakabiliwa na chuki dhidi ya Uislamu ambazo sasa ni jambo la kawaida katika nchi hiyo.

Bi. Abboud wa chama cha Democrat analenga kumuondoa seneta wa sasa wa jimbo la Arizona Jeff Flake wa chama wa Republican. Anasema hatua yake ya kugombea inanasibishwa na imani yake ya Kiislamu na kuongeza kuwa: "Siwezi kuificha dini yangu na kamwe sitafanya hivyo.”

Abboud alipongezwa Jumatatu wakati alipokabiliana na watu waliotuma maoni yenye chuki katika intaneti kuhusu imani yake ya Kiislamu. Akizungumza na waandishi habari katika makao makuu ya chama cha Democrat huko Arizona, alibainisha kuhusu uraia wake wa Marekani na imani yake ya Kiislamu. Bi. Abboud ambaye ni mwanasheria na mwanaharakati amesisitiza umuhimu wa ustaarabu katika mijadala ya kisiasa nchini Marekani na kubainisha masikitiko yake kuwa, hujuma za chuki dhidi ya Uislamu anazokabiliana nazo sasa ni jambo la kawaida Marekani.

Akifafanua zaidi alisema: "Kuwa Mwislamu Marekani ni kuwa huru. Kuwa huru kuvaa hijabu na kuwa huru kupambana dhidi ya magaidi wa ISIS (Daesh) ambao si Waislamu na wengine wote wanaotekeleza ugaidi kwa jina la Uislamu.”

Hadi sasa Abboud ndie mgombea pekee wa chama cha Democrat katika mchujo wa chama hicho na yamkini ni mgombea wa kwanza Muislamu kuwania useneta katika historia ya Arizona.

3625546

captcha