IQNA

Wasiwasi wa Waislamu Uhispania kuhusu chuki dhidi ya Uislamu

12:52 - August 20, 2017
Habari ID: 3471132
TEHRAN (IQNA)-Waislamu nchini Uhispania wana wasiwasi mkubwa kuhusu ongezeko la chuki dhidi ya Uislamu kufuatia hujuma ya kigaidi mjini Barcelona ambayo magaidi wa ISIS walidai kuhusika nayo.

Ili kukabiliana na wimbi la chuki dhidi ya Uislamu, Waislamu Jumamosi walijumuika katika eneo la Las Ramblas mjini Barcelona palipojiri hujuma hiyo iliyoua watu 14 siku ya Alhamisi na kusisitiza kuwa Uislamu na Waislamu waliowengi hawana uhusiano na ugaidi. Waandamanaji ambao walijumuisha jamii ya Waislamu mjini Barcelona walisisitiza kuwa "Sisi si magaidi” na "Uislamu ni Amani.”

Waislamu katika jimbo la Catalan ambalo mji wake mkuu ni Barcelona, hasa wenye asili ya Morocco, wamekuwa katika mashinikizo makubwa baada ya kubainika kwa washukiwa wanne wakuu wa hujuma hiyo ya kigaidi wana asili ya Morocco.

Shambulizi hilo lilifanyika baada ya gaidi kuwagonga kwa makusudi watu waliokuwa wakitembea kwa miguu katika eneo la kitalii la Las Ramblas katikati ya jiji la Barcelona na kukanyaga makumi ya watu.

Baada ya kila hujuma ya kigaidi barani Ulaya hushuhudiwa ongezeko la chuki dhidi ya Waislamu na Uislamu hasa pale kundi la kigaidi la ISIS linapodai kuhusika. Waislamu waliowengi kote duniani wanasisitiza kuwa hawana uhusiano na kundi la kigaidi na kitakfiri la ISIS au Daesh ambalo wanasema liliasisiwa na mashirika la kijasusi ya Kizayuni na madola ya magharibi.

3632246

captcha