IQNA

Mashindano ya Qur'ani Tukufu

Washindi wa Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani ya Moscow watunukiwa zawadi

19:57 - November 11, 2023
Habari ID: 3477874
MOSCOW (IQNA) - Mashindano ya 21 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Moscow yalimalizika Ijumaa huku mwakilishi wa taifa mwenyeji, yaani Russia, akitwaa tuzo ya kwanza.

Ayomiddin Fakhruddin kutoka Russia alishinda taji la mashindano ya kimataifa yaliyoanza Jumatano. Hossein Khani-Bidgoli wa Iran na Ismail Mohammed Yahya Maniar wa India wameshika nafasi ya pili.

Hafla ya kutunukiwa tuzo hiyo ilifanyika katika ukumbi wa tamasha wa Hoteli ya Cosmos huku maafisa wengi wa Russia wakihudhuria.

Mashindano hayo, ambayo yaliandaliwa na Idara ya Kiroho wa Waislamu wa Shirikisho la Russia na Baraza la Mufti wa Russia, yalivutia washiriki 31 kutoka Mashariki ya Kati, Afrika, Kati na Kusini Mashariki mwa Asia.

Chuo Kikuu cha Mohammed bin Zayed, mojawapo ya vyuo vikuu vikubwa zaidi katika Umoja wa Falme za Kiarabu, pia kilifadhili mashindano hayo.

Kulingana na shirika la habari la TASS, Fakhruddin, 21, alikulia Aleksin, eneo la Tula. Alianza kujifunza Quran kwa moyo akiwa na umri wa miaka 6 na akaimaliza akiwa na umri wa miaka 10. Hivi sasa anasoma katika Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Madina na anazungumza Kirusi, Tajiki, Kiarabu na Kiingereza. Amekuwa akishiriki katika mashindano mbalimbali ya usomaji wa Qur'ani nchini Urusi na nje ya nchi kwa miaka 10.

Toleo la 20 la tukio hili lilifanyika Novemba mwaka jana, kufuatia kusitishwa kwa miaka miwili kwa sababu ya janga la kimataifa la COVID-19.

Habari zinazohusiana
captcha