IQNA

Waislamu Russia

Waislamu wa Russia hawana vizingiti katika shughuli zao za Qur’ani

19:42 - March 09, 2024
Habari ID: 3478475
IQNA – Hafidh wa Qur'ani kutoka Russia amesema Waislamu nchini humo hawana kikomo katika shughuli zao za Qur'ani.

Burhanddin Rahimov ambaye alishiriki katika Awamu ya 40 ya Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Iran mwezi uliopita aliyasema hayo katika mahojiano na IQNA na kuongeza kuwa tangu kuanguka kwa Umoja wa Kisovieti, shughuli za Qur'ani zimekuwa zikiongezeka nchini Russia.

Serikali ya Usovieti ilizzuia shughuli za Qur’ani na harakati zingine zozote za kidini ambapo wafuasi wa dini mbali mbali walikabiliwa na matatizo mengi katika shughuli zao za kidini katika enzi hiyo, alibainisha.

Hata hivyo, baada ya kuanguka kwa Umoja wa Kisovieti, wimbi la shughuli za Qur'ani zilianza nchini Russia, alisema.

Sasa kuna tarjuma na tafsiri nyingi za Qur’ani Tukufu  katika lugha ya Kirusi, aliendelea kusema.

Pia Waislamu wanaweza kwenda kwenye misikiti na vituo vya Kiislamu bila matatizo yoyote na kufundisha kozi za Qur’ani na Kiislamu, alibaini Rahimov.

Alisema shughuli za Qur'ani katika nchi yake zinaweza kugawanywa katika makundi matatu makubwa, la kwanza likiwa ni ufundishaji wa Qur'ani.

Watoto wa Kiislamu wanaanza kujifunza Qur;ani wakiwa na umri mdogo, alisema, akibainisha kwamba yeye mwenyewe, alianza kuhifadhi Qur’ani Tukufu  akiwa na umri wa miaka 5. Pia kuna kozi za Qur’ani kwa watu wazima .

Aidha  pia kuna mashindano ya Qur'ani, huku mashindano ya kimataifa ya Qur'ani ya Moscow yakiwa tukio muhimu zaidi la Qur'ani nchini Russia, aliongeza.

Na ya tatu inahusisha shughuli zinazohusiana na uchapishaji wa Qur’ani ikiwa ni pamoja na tarjuma na tafsiri, Rahimov alisema.

Kwingineko katika matamshi yake, mwanaharakati huyo wa Qur'ani wa Russia alipongeza tukio la kimataifa la Iran na kupongeza kiwango cha juu cha usomaji wa Qur'ani wa wasomoja qurani au maqari wa Iran.

Hatua ya mwisho ya Awamu ya 40 ya Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Iran ilifanyika mjini Tehran kuanzia tarehe 15 hadi 21 Februari kwa kushirikisha wasomaji na wahifadhi 69 kutoka nchi 44.

Hafla hiyo ya kila mwaka inayoandaliwa na Shirika la Masuala ya Wakfu na Misaada ya Iran, inalenga kukuza utamaduni na maadili ya Qur'ani miongoni mwa Waislamu na kuonyesha vipaji vya wasomaji na wahifadhi Qur'ani.

Russia ni nchi kubwa yenye watu milioni 146. Uislamu ni dini ya wachache nchini Urusi ambapo kuna takriban Waislamu milioni 25.

Nchi hiyo ina Waislamu wengi zaidi barani Ulaya. Watu wengi wa Russia ni Wakristo wa madhehebu ya Orthodox.

/3487484

captcha