IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Nchi za Waislamu zipewe jukumu la kupambana na magaidi

12:48 - May 24, 2016
Habari ID: 3470332
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, amesema nchi za Waislamu zinapaswa kupewa jukumu la vita dhidi ya ugaidi kwani ugaidi unanasibishwa kimakosa na Uislamu.

Ayatullah Ayatullah Seyyed Ali Khamenei ameyasema hayo Jumatatu jioni mjini Tehran alipoonana na Waziri Mkuu wa India, Bw. Narendra Modi. Kiongozi Muadhamu aliongeza kuwa, madola ya Magharibi si wakweli katika madai ya kupambana na ugaidi, bali hata yanahusika katika kuzuka magenge ya kigaidi katika nchi kama za Afghanistan, Iraq na Syria.

Ayatullah Khamenei amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalipa uzito mkubwa suala la vita dhidi ya ugaidi na itatumia uwezo wake wote kukabiliana na uovu huo.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa India amesema, Uislamu ni dini ya kupendana, ni dini ya kuishi salama na watu wote na haina uhusiano wowote na vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na baadhi ya watu kwa jina la dini hiyo.

Jana pia Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alionana na Rais wa Afghanistan pamoja na Waziri Mkuu wa India hapa mjini Tehran.

Katika mazungumzo yake na Rais Mohammad Ashraf Ghani wa Aghanistan, Ayatullah Khamenei alisema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikilipa umuhimu mkubwa suala la maelewano na usalama wa Afghanistan na inayahesabu maendeleo ya kila upande ya Afghanistan kuwa ni sawa na maendeleo yake.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, tofauti na zinavyofanya baadhi ya nchi kama vile Marekani na Uingereza, daima Iran imekuwa ikiwaangalia wananchi wa Afghanistan kwa heshima, kwa udugu na kwa mapenzi, na kwamba Tehran iko tayari kutoa msaada wowote ule wa kiufundi, kiuhandisi na ujenzi wa miundo mbinu kwa nchi ndugu ya Afghanistan.

Kwa upande wake, Rais wa Afghanistan amesema, nchi yake itaendelea kulishukuru taifa la Iran kwa mapenzi yake makubwa kwa wananchi wa Afghanistan.

3500511
captcha