IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Nchi inahitaji usalama kustawi

22:55 - May 08, 2016
Habari ID: 3470301
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, usalama katika jamii una nafasi muhimu katika ustawi wa kiuchumi.
Ameongeza kwamba, kama katika jamii hakutakuwa na umasikini lakini kukawa hakuna usalama, basi maisha yatakuwa machungu.
Ayatullah Udhma Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyasema hayo Jumapili mjini Tehran alipoonana na makamanda na maafisa wa jeshi la polisi na kusema kuwa, suala la kulinda usalama lina umuhimu wa kwanza na wa juu kabisa na huku akisisitizia wajibu wa maafisa wa Jeshi la Polisi kusimamia kikamilifu na kwa uzito wa hali ya juu suala la usalama wa kifikra, kikazi na kimaadili wa wafanyakazi na kudhamini usalama wa kijamii na kimaadili amesema: Hakikisheni mnapangilia mipango yenu yote juu ya msingi wa akili na mantiki, nia na uwezo wa kweli, huruma na kuchunga sheria ili kwa njia hiyo muweze kuzivutia hisia nzuri za wananchi na kuzifanya zikite mizizi katika nyoyo zao na wawe na taswira nzri inayotakiwa kuhusu thamani ya jeshi hilo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia matukio kadhaa muhimu yaliyotokea katika miezi ya hivi karibu yanayoonesha kazi nzuri inayofanywa na jeshi hilo licha ya kuwa na mashaka na usumbufu mwingi kazi hizo na kuwashukuru makamanda na maafisa wa Jeshi la Polisi pamoja na mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kulinda amani wakati wa maadhimisho ya Alfajiri Kumi na maandamano ya Bahman 22 (wakati wa sherehe za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran), kuendesha na kusimamia kwa amani na utulivu duru mbili za uchaguzi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) na vile vile uchaguzi wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu pamoja na kutekeleza vizuri majukumu ya kulinda usalama katika njia zinazounganisha miji mbali mbali wakati wa safari za sikukuu za Nairuzi.

Ayatullah Udhma Khamenei amekumbushia nukta nyingine kuhusu safari za sikukuu za Nairuzi na kusema kuwa, licha ya kwamba idadi ya hasara zilizotokana na ajali za barabarani zimepungua mwaka huu lakini pamoja na hayo hasara za ajali hiyo bado ziko juu na kwamba Jeshi la Polisi pamoja vyombo husika vinapaswa kuongeza juhudi za kuhakikisha kuwa hasara hizo zinazidi kupungua.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, suala la usalama ni muhimu mno na linapaswa liweke katika daraja ya kwanza ya vipaumbele na huku akisisitiza kuwa, bila ya usalama haiwezekani kuendelea na maisha ya kila siku, wala harakati za kielimu, wala za vyuo vikuu na wala siasa za uchumi na uendeshaji nchi ameongeza kuwa: Hatua na vitendo katika masuala ya uchumi wa kimuqawama na kumea mti mwema wa uchumi unaotokana na nguvu za ndani ya nchi nayo ni mambo yanayohitajia kuwepo usalama.

Ayatullah Udhma Khamenei ameitaja kazi ya kuchunguza kwa kina jeshi la polisi na vyombo husika na kugundua chanzo cha ukosefu wa usalama kuwa ni jambo lenye umuhimu mkubwa na huku akisisitizia ulazima wa vyombo vyote nchini kulisaidia jeshi la polisi ameongeza kwamba: Usalama, umakini, kuweko hisia za hali ya juu za kupenda kutekeleza vilivyo majukumu yao kati ya makamanda wa ngazi za juu wa Jeshi la Polisi na miamala mizuri sana ya mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ambaye anatekeleza majukumu yake kama baba ni fursa nzuri sana ya kuweza kutumiwa kwa njia bora kabisa sifa na mambo hayo kwa ajili ya kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.

Vile vile amesisitizia ulazima wa kusaidiwa serikali katika juhudi zake za kulistawisha kiubora na kiidadi jeshi la polisi na amegusia pia ulazima wa kuzingatiwa kwa hali ya juu suala la misaada ya wananchi na kuongeza kuwa: Jeshi la Polisi na Wizara ya Mambo ya Ndani zinapaswa kufanya uchunguzi wa kina kuhusu nyuga na sehemu ambazo wananchi wanaweza kutoa misaada yao na sambamba na kuziainisha nyuga hizo, zizitangaze wazi pia kwa wananchi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia upana wa wigo wa ushirikiano wa Jeshi la Polisi na matabaka mbali mbali ya wananchi na kusema kuwa usalama wa jeshi hilo ni jambo muhimu sana. Ameongeza kuwa: Usalama wa fikra, kazi na maadili ndani ya Jeshi la Polisi, sambamba na kuwafanya wananchi wajitolee kulisaidia jeshi hilo, aidha huufanya uhusiano baina ya jeshi hilo na matabaka mbali mbali ya wananchi kuwa wa kimapenzi, wa kushibana na wa kidugu.

Ayatullah Udhma Khamenei vile vile amesema, ni jambo la lazima kwa Jeshi la Polisi kuwa na usimamiaji wa kina, wa pande zote na wa daima wa mambo ya usalama na hapo hapo amesisitizia wajibu wa kupanuliwa wigo wa uwezo wa Jeshi la Polisi katika kona zote za nchi na kulinda usalama katika maeneo yote ya makazi ya raia na maeneo yanayopakana na makazi ya watu; iwe ni maeneo ya pembeni mwa miji, maeneo ya mbali pamoja na miji midogo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, suala la usalama wa kimaadili na daghadagha na wasiwasi wa wananchi katika uwanja huo na ni miongoni mwa masuala muhimu ambayo inabidi Jeshi la Polisi liyazingatie. Amesema: Uraibu wa madawa ya kulevya, uhalifu na uvunjaji wa amani ni tishio kwa usalama wa mwili, roho na maadili ya jamii; hivyo inabidi kuwekwe mikakati mizuri na itumike mitazamo wa kiutaalamu ya wanafikra na weledi wa kutoa nadharia hususan ndani ya Jeshi la Polisi katika kukabiliana na jambo hilo.

Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kwamba: Kuhusu masuala yanayohusiana na usalama wa kimaadili; baada ya kuweka mikakati ya kina, makini, ya kimantiki na sahihi, haipasi kushughulishwa tena na upinzani wa baadhi ya watu au malalamiko ya baadhi ya vyombo vya habari, bali inabidi kuendelea na kazi ya kufanikisha jambo hilo kwa kutawakali kwa Mwenyezi Mungu.

Vile vile amesema ni jambo muhimu sana kuhakikisha kuwa sura nzuri na inayotakiwa kikamilifu inajengeka ndani ya akili za wananchi kuhusiana na Jeshi la Polisi na kusisitiza kuwa: Inabidi kuhakikisha kuwa, picha na taswira inayojengeka ndani ya akili za wananchi kuhusiana na Jeshi la Polisi ni ya kuliona jeshi hilo ni rafiki wa kuaminika wa wananchi, mwenye huruma na mwenye nguvu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Kutumia nguvu na kutotetereka bila ya kufanya ukatili, kulinda usalama wa ndani ya jeshi, uwepo wa jeshi hilo katika muda unaotakiwa na kwa haraka sana katika tukio, huruma na kuwasaidia wananchi pamoja na kuchunga na kuheshimu sheria ni katika mambo ambayo yanapelekea kujengeka sura nzuri kwa Jeshi la Polisi ndani ya nyoyo na akili za watu.

Ayatullah Udhma Khamenei amesema, iwapo hayo yatatekelezwa yatazaa mazingira ya kupiga hatua Jeshi la Polisi na kulifanya litoe mchango jeshi hilo katika maendeleo ya umma na nchi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja mwenendo wa maendeleo ya Iran licha ya kuweko njama za miaka 37 za maadui kuwa ni mzuri na wenye kuendelea na kuongeza kuwa: Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kwa uungaji mkono wa wananchi, umewarambisha mchanga maadui na kwamba njama za maadui za kujaribu kupandikiza ukataji tamaa na ukosefu wa matumaini, kuwa na mtazamo mbaya na mizozo ndani ya Iran ni mambo yanayofanywa na maadui hivi sasa kutokana na kukasirishwa kwao na maendeleo ya kila namna ya Iran.

Ayatullah Udhma Khamenei aidha amewataka viongozi na wananchi wote nchini Iran kuchunga na kuulinda umoja na mshikamano uliopo nchini na kuongeza kuwa: Kuzusha mirengo miwili, kambi mbali na makundi mawili ni katika mambo yenye madhara ya kuangamiza ambayo yanafuatiliwa na adui kwa muda mrefu sana.

Aidha amelitaja suala la kuwepo baadhi ya mambo yasiyo sahihi na potofu katika jamii kuwa ni jambo la kawaida kwa kila nchi na kuongeza kwamba: Kama mtu anataka kuwa na tathmini nzuri kuhusiana na hali ya Iran anapswa kuangalia harakati kuu ya wananchi ambayo kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu na taufiki Yake, harakati hiyo kwa mtazamo wa walio wengi, ni nzuri sana.

Vile vile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezitaja kazi zinazofanyika katika kitengo cha itikadi na siasa cha Jeshi la Polisi kwa ajili ya kuimarisha misimamo ya kidini na kulifanya jeshi hilo lifanye kazi kwa ufanisi zaidi; kuwa ni muhimu sana na zinazopaswa kupongeza.

Pia amezishukuru familia za makamanda na maafisa wa Jeshi la Polisi kwa subira na uvumilivu wao mkubwa ambao unachangia sana katika ufanisi wa kazi za jeshi hilo.

Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Brigedia Jenerali wa Polisi Hossein Ashtari, Mkuu wa Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa sikukuu za mwezi mtukufu wa Shaaban na kusema kuwa, miongoni mwa kazi muhimu zinazofanywa na jeshi hilo ni pamoja na kusimamia na kudhibiti vizuri usalama wa mipakani, kuongeza uwezo wa operesheni kwa ajili ya kupambana na wahalifu, magaidi na wafanya magendo, kutumia zana na vifaa vya kisasa vya kufanyia kazi, kupunguza idadi ya watu wanaopoteza maisha na ajali za barabarani, kuzingatia nidhamu katika nyuga zote, kulinda usalama wa nguvu kazi na kusaidia katika ufanikishaji wa siasa za uchumi wa kimuqawama.

Brigedia Jenerali Ashtari ameongeza kuwa: Kutoa majibu kuhusu daghadagha na wasiwasi pamoja na matakwa ya umma kuhusiana na kupambana vilivyo na uhalifu na ufisadi unaofanywa kitaasisi ni katika vipaumbele vya kazi za Jeshi la Polisi na tab’an ufanikishaji wa jambo hilo unahitajia msaada wa kuendelea wa wananchi, ushirikiano baina ya Mihimili Mitatu Mikuu wa dola (Serikali, Bunge na Mahakama) pamoja na vyombo tofauti vinavyohusika na suala hilo nchini.

3495971

captcha