IQNA

Wazayuni wenye misimamo mikali wauhujumu Msikiti wa Al Aqsa

17:30 - May 30, 2016
Habari ID: 3470347
Genge la Wazayuni wenye misimamo ya kufurutu ada wakipata himaya ya askari wa utawala haramu wa Israel wameuhujumu na kuuvunjia heshima Msikiti wa Al Aqsa.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, katika kitendo hicho kilichojiri Jumatatu aktika mji wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na Israel, Wazayuni waliuhujumu msikiti huo kupitia lango la Maghareba.

Askari wa utawala wa Israel waliwazuia Wapalestina wakiwemo waliokuwa hapo kukabiliana na Wazayuni hao. Aidha askari wa Israel pia waliwazuia Wapalestina kusalia ndani ya msikiti huo wakati wa hujuma hiyo.

Weledi wa mambo wameonya kuhusu njama za hivi karibuni za Israel za kuyahudisha Quds Tukufu hatua ambayo italitumbukiza eneo la Magharibi mwa Asia (Mashariki ya Kati) katika machafuko.

Tangu mwanzoni mwa mwezi Oktoba mwaka uliopita wa 2015 hadi sasa maeneo mbalimbali ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu yamekuwa yakishuhudia wimbi la malalamiko ya upinzani dhidi ya siasa za kichokozi za utawala wa Kizayuni na njama za utawala huo za kuvuruga utambulisho wa Baitul Muqaddas pamoja na mpango wake wa kuugawa kiwakati na kimahali msikiti mtukufu wa Al-Aqsa. Wimbi hilo la malalamiko limekuwa maarufu kwa jina la Intifadha ya Quds.

Wapalestina zaidi 215 wameshauawa shahidi tangu ilipoanza Intifadha ya Quds mwezi Oktoba mwaka jana hadi hivi sasa.

Inafaa kuashiria hapa kuwa, Masjidul Aqswa ni kibla cha kwanza cha Waislamu na kituo cha mwanzo cha safari ya Mi'iraji ya Mtume Mtukufu SAW, lakini umekuwa ukishambuliwa na kuvunjiwa heshima na magenge ya Kizayuni yenye misimamo mikali huku yakipata uungaji mkono wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Wapigania ukombozi wa Palestina wanasisitiza kuwa, Quds i ndio mji mkuu wa dola huru la Palestina litakaloundwa katika mustakabali.

captcha