Rais Rouhani amesema kuwa, mwaka huu kwa kuweko mshikamano na umoja zaidi ulimwengu utashuhudia maandamano makubwa zaidi katika Siku ya Kimataifa ya Quds nchini Iran na katika nchi nyingine ulimwenguni.
Amesema kuwa, wananchi wa Iran watajitokeza katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds kwa shabaha ya kuitikia wito wa Imam Ruhullah Khomeini MA muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliyeitangaza na kuianisha Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds.
Rais Rouhani amesema kuwa, mbali na kuitikia wito wa Imam Khomeini MA
wananchi wa Iran watajitokeza katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya
Quds kusaidia kupaza sauti ya kudhulumiwa ya wananchi wa Palestina
ambao kwa takribani miaka 70 wametimuliwa katika nyumba zao na
kulazimika kuwa wakimbizi.
Rais wa Iran amebainisha kuwa, Waislamu wataendelea na njia yao ya
kuwaunga mkono wananchi wa Palestina kama ambavyo watadumisha harakati
zao za kuikomboa Quds Tukufu kutoka mikononi mwa Wazayuni maghasibu.
Ijumaa Julai Mosi ni Siku ya Kimataifa ya Quds ambapo watu kutoka matabaka mbalimbali duniani wanatazamiwa kuandamana na kujumuika kwa lengo la kuonesha mfungamano wao na mapambano ya ukombozi wa Palestina sambamba na kuulani utawala wa Kizayuni wa Israel na waitifaki wake.