IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiisalmu

Marekani ni kinara wa wanaoibua ugaidi, vita katika Ulimwengu wa Kiislamu

20:19 - July 06, 2016
Habari ID: 3470437
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema chanzo kikuu cha vita, ukosefu wa usalama katika eneo la Kusini mwa Asia na Ulimwengu wa Kiislamu ni madola makubwa ya kiistikbari yakiongozwa na Marekani.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo leo mjini Tehran wakati alipokutana na maafisa wa ngazi za juu wa mfumo wa Kiislamu, mabalozi wa nchi za Kiislamu walioko Iran na wananchi wa matabaka mbali mbali katika Baraza la Idul Fitr. Katika kikao hicho, amesisitiza kuwa, lengo la madola ya kibeberu na kiistikbari ni kuibua mazingira ya kuuwezesha utawala wa Kizayuni kupumua sambamba na kusahauliwa kadhia muhimu ya Palestina. Amesema njia pekee ya kukabiliana na njama hizi, ni kumfahamu vyema adui halisi na kusimama kidete.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametuma salamu zake za pongezi kwa munasaba wa Idul Fitr huku akiashiria hali ya hivi sasa ya Ulimwengu wa Kiislamu hasa mauaji, ukosefu wa usalama na hujuma za umwagaji damu na kusema: "Moja ya masuala muhimu ni kufahamu chanzo cha ukhabithi na mushkili uliopo katika Umma wa Kiislamu na mikono iliyo nyuma ya pazia yenye kuhimiza na kuchochea ugaidi.

Ayatullah Khamenei ameashiria hatua ya nchi zote kuchukizwa na ugaidi kidhahiri na kisha kuunda muungano bandia wa eti kupambana na ugaidi na kusema: "Kinyume na madai yao ya kidhahiri, madola makubwa duniani ndiyo yenye kuchochoea na kuunga mkono ugaidi."

Huku akiashiria kushiriki balozi wa Marekani katika maandamano ya siku za awali za kuanza mgogoro wa kisiasa Syria sambamba na kuandaa mazingira ya kubadilisha mzozo wa kisiasa kuwa vita vya ndani nchini humo, Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa: "Mgogoro wa kisiasa ulibadilishwa kuwa vita vya ndugu kuua ndugu na kisha baada ya hapo, kupitia uungaji mkono wa kifedha na kisilaha na kwa mapato haramu ya uuzaji mafuta, watu walikusanywa kutoka maeneo mbali mbali na kupelekwa Syria na Iraq na kisha kulitumbukiza eneo katika machafuko."

Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, kinyume na madai ya baadhi, Iran haijaingilia masuala ya ndani ya Bahrain na wala haitafanya hivyo na kwamba iwapo busara ya kisiasa itakuwepo nchini humo, malumbano ya kisiasa hayatageuka na kuwa vita vya ndani.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia ameashiria hali ya Yemen na kuendelea kudondoshewa mabomu kila siku nyumba za raia, mahospitali, misikiti na miundo msingi ya nchi hiyo na kusema: "Wavamizi wanapaswa kusitisha hujuma dhidi ya ndugu zao na pia ulimwengu wa Kiislamu unapaswa kuwaadhibu wavamizi."

3513324

captcha