IQNA

Katibu Mkuu wa Hizbullah

Mapambano (Muqawama) ya Hizbullah yalivuruga njama za Wazayuni mwaka 2000

19:16 - October 03, 2016
Habari ID: 3470595
Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kuwa, wakati muqawama ulipoweza kuzuia kufanikishwa malengo ya adui, ulipata ushindi, na zaidi ya hayo ni kuwa, muqawama uliweza kufanikisha malengo yake.

Sayyid Hassan Nasrallah alisema hayo jana usiku kwa mnasaba wa kuanza mwezi wa Muharram na kuongeza kuwa: Mwaka 2000 muqawama ulifanikiwa kuvuruga malengo yote ya adui Mzayuni ambayo alikuwa akiyafuatilia huko Lebanon tangu mwaka 1982, na wakati huo huo ukafanikiwa kutimiza malengo yake.

Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon ameongeza kuwa, katika mapambano ya Imam Husain AS huko Karbala, kulikuwa na kambi mbili zenye malengo tofauti, na ni wakati tunapochanganua milingano ya kidunia na ya Akhera ndipo tutakapoweza kujua mshindi hasa ni nani katika mapambano hayo.

Aidha amesema, Daesh au ISIS na makundi mengine ambayo yanatumia mauaji, uchinjaji wa watu na maovu mengine kuupaka matope Uislamu kwa madai ya eti kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, kwa hakika ni wajukuu wa Muslim bin 'Aqaba. 

Sayyid Hassan Nasrallah ameongeza kuwa, Uislamu na madhehebu yake yote umeweza kubakia na kuimarika kwa baraka za damu ya Imam Husain AS, na lau kama Imam asingelisimama imara huko Karbala kuilinda na kuitetea dini Kiislamu aliyokuja nayo babu yake yaani Bwana Mtume Muhammad SAW, leo hii kusingelikuwa na hata chembe ya Uislamu.

Amesema, Imam Husain AS amewafunza walimwengu kwamba kama umma utatekeleza vilivyo majukumu yake basi utapata ushindi na hata katika zama hizi pia tunaweza kushuhudia damu inavyoushinda upanga.

3534947

captcha