Sayyid Hassan Nasrallah ameongeza kuwa Saudia inahuisha uhusiano wake na utawala haramu wa Israel na kupuuza maslahi ya Wapalestina. Kiongozi wa Hizbullah amesema utawala wa Aal-Saud unatoa mfano mbaya
kwa mataifa mengine na haswa ya Kiislamu katika kufufua uhusiano wake na
utawala haramu wa Israel. Akizungumza Ijumaa kwa njia ya televisheni katika
marasimu ya kukumbuka kifo cha Ahmad Zahri, mmoja wa makamanda wa
harakati hiyo ya Kiislamu, Sayyid Nasrallah amesema sio jambo la mbali
kwa utawala wa Riyadh katika hatua yake ya pili ya kufufua uhusiano wake
na Israel, kutangaza kuutambua rasmi utawala huo bandia unaokalia kwa
mabavu ardhi za Wapelestina.
Kauli ya Katibu Mkuu wa harakati ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon imekuja siku chache baada ya ujumbe wa ngazi za juu wa serikali ya
Riyadh ukiongozwa na Jenerali Anwar Eshki, kamanda mkuu wa zamani wa
Saudia kuutembelea utawala ghasibu wa Israel na kukutana na kufanya
mazungumzo na wakuu wa utawala huo katili wakiwemo wabunge wa bunge la utawala huo,
Knesset.
Eshki ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Kituo cha Mafunzo ya Kiistratejia
na Sheria cha Mashariki ya Kati kilichoko Jeddah alikutana na kufanya
mazungumzo na Dore Gold, Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya
Israel na Mshirikishi wa Masuala ya Harakati za Israel katika ardhi za
Palestina zinazokaliwa kwa mabavu Yoav Mordechai miongoni mwa maafisa
wengine wa utawala huo wa Kizayuni.
Katika miezi ya hivi karibuni kumefuchuliwa mazungumzo ya siri baina ya maafisa wa ngazi za juu wa Saudia na Utawala wa Israel, jambo ambalo limeamsha hasira za Waislamu wengi duniani.
3460541