IQNA

Wanawake Waislamu wenye kuvaa Hijabu Australia wahujumiwa

12:24 - July 10, 2017
Habari ID: 3471059
TEHRAN (IQNA)-Watu wenye chuki dhidi ya Uislamu nchini Australia wanawalenga zaidi wanawake wenye kuvaa Hijabu, ripoti mpya imebaini.

Kwa mujibu wa ripoti kuhusu Chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) nchini Australia, kati ya matukio 243 ya hujuma dhidi ya Waislamu, asilimia 67.7 ya waliolengwa walikuwa ni wanawake na karibu asilimia 75 ya waliotekeleza hujuma hizo walikuwa ni wanaume.

Ripoti hiyo ambayo ni ya kwanza nchini Australia imechapishwa kwa ushirikiano na vyuo vikuu kadhaa, Akademia ya Sayansi za Kiislamu na Utafiti Australia na Baraza la Tamaduni Anuai Australia. Linda Briskman ambaye ni msomi wa masuala ya kijamii katika Chuo Kikuu cha Western Sydney anasema kuhujumiwa wanawake Waislamu ni jambo linalotia wasiwasi sana. Halikadhalika ripoti hiyo imesema kuna uhusiano baina ya vitendo vya ugaidi unaotekelezwa na watu wanaodai kuwa eti ni Waislamu au wenye majina ya Kiislamu na ongezeko la chuki dhidi ya Uislamu. Vitendo vya kuwahujumu Waislamu huongezeka punde baada ya kujiri tukio la ugaidi sehemu yoyote duniani.

Ripoti hiyo imebaini kuwa asilimia 79.6 ya wanawake Waislamu huhujumiwa wakiwa wamevaa Hijabu na asilimia 30 wakiwa na watoto wao.

Waliotayarisha ripoti hiyo wanasema ripoti hiyo imeashiria tu sehemu ya tatizo lililopo ambalo ni kubwa kuliko inavyoripotiwa. Aidha wasomi wanasema kwa kuzingatia matokeo ya uchunguzi wao, wakuu wa Australia watachukua hatua za dharura kukabiliana na wimbi la chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini humo.
3617200
captcha